Siku yako kuwa nzuri au kuwa mbaya, huwa haitegemei sana na jinsi siku inavyokuwa imeanza au inavyoenda, bali inategemea sana mtazamo ambao wewe unakuwa nao.
Tuangalie mfano wa watu wawili, ili tuweze kuelewana vizuri.
Mtu wa kwanza ametoka nyumbani asubuhi kuwahi kwenye shughuli zake. Amepanga usafiri wa umma, ambapo kwa hiyo asubuhi unakuwa umejaa watu wengi wanaoenda kwenye shughuli zao. Akiwa amesimama ndani ya gari, mtu mwingine anamkanyaga. Kwa upole anamuuliza mtu huyo mbona umenikanyaga? Mtu huyo anaanzwa kutokwa na maneno mengi akimwambia; “Kwani hujui hili ni daladala, kama ungetaka starehe ungekodi teksi au kuwa na gari yako.” Anakasirishwa na majibu hayo, wanazozana sana na anaposhuka kwenye gari anakuwa amepatwa na hasira. Siku nzima inakuwa imeathiriwa na hicho kilichotokea.

Mtu wa pili naye anawahi kwenye shughuli zake, amepanda daladala na mtu anamkanyaga. Anamuuliza kwa upole mbona umenikanyaga? Mtu huyo anamjibu; “Kwani hujui hili ni daladala, kama ungetaka starehe ungekodi teksi au kuwa na gari yako.” Naye anakaa kimya hamjibu chochote, hakuna mabishano na anaposhuka anaendelea na shughuli zake bila kuvurugwa.
Tukio ni moja, lakini jinsi ambavyo watu hao wamelichukulia imeathiri siku yao nzima. Kwa mmoja siku imevurugika, wakati mwingine siku imekwenda vizuri. Ambaye siku imevurugika ni yule anayeona hastahili kile alichofanyiwa na hivyo kutaka kuhakikisha anasahihisha hilo. Ambaye hajavuruga siku yake ni yule aliyepuuza lile lililotokea, kwa sababu tayari alijua kwenye siku yake atakutana na watu waliovurugwa hivyo hakuruhusu nao wamvuruge.
Iwapo utakuwa na siku ambayo umevurugwa, lazima ujue kabisa ni wewe mwenyewe umeruhusu siku yako kuvurugwa. Na kwa bahati mbaya sana, siku yako huwa inavurugwa na wale ambao tayari siku zao zimevurugwa. Hivyo ukijua kwamba utakutana na watu ambao siku zao zimevurugwa na ukawazuia wasiathiri siku yako, kila siku utakuwa na siku tulivu.
Hilo ndilo ambalo Mwanafalsafa wa Ustoa Marcus Aurelius anatufundisha kwenye kitabu cha pili cha Meditations. Anaandika; “Ianze siku yako ukijiambia leo naenda kukutana na watu waliovurugwa, wabinafsi, wasiojali na wadhalimu. Wanafanya hayo yote kwa sababu hawajui mema na mabaya, ila mimi najua mema na mabaya hivyo sitaruhusu wanisumbue.” Rafiki, hebu fikiria kama utaianza kila siku yako kwa mtazamo wa aina hii, nini ambacho kitakusumbua? Hakuna, kwa sababu kila unachokutana nacho, tayari ulishatarajia kukutana nacho.
Marcus anaendelea akisema, pamoja na changamoto ambazo watu wanaweza kuwa nazo, bado tunawahitaji kwenye maisha yetu, kama ambavyo mikono miwili inafanya kazi pamoja, macho mawili na hata masikio mawili. Licha ya changamoto ambazo watu wanazo, bado ni muhimu kwenye maisha yetu, hivyo tunapaswa kuwachukulia kama walivyo. Hapa Marcus ametuongezea silaha nyingine ya kuendesha siku zetu kwa utulivu, siyo tu watu hawatatuvuruga, bali pia tutawachukulia vile walivyo. Hatutahangaika kuwataka wabadilike wawe vile wanavyotaka.
Kitu kingine kikubwa ambacho Marcus anakieleza kwenye kitabu hicho cha pili ni mambo matano ambayo huwa yanawavuruga watu na kuwakosesha utulivu. Mambo hayo yanapaswa kuepukwa sana kama mtu anataka kuwa na maisha tulivu kila siku.
Mambo hayo ni kama ifuatavyo;
1. Kulalamikia asili. Kulalamika kwa mambo yanayotokea kwa asili ambayo huwezi kuyabadili. Kuondokana na hili unapaswa kupokea kila kinachotokea kwenye asili na kukitumia kwa manufaa.
2. Kuwaumiza wengine kwa hasira. Hapa mtu unasukumwa na hasira kuwaumiza wengine. Kuondokana na hii unapaswa kudhibiti hasira zako kwa kutokuziruhusu ziwafikie wengine.
3. Kufanya maamuzi kwa hisia za tamaa au maumivu. Unapofanya maamuzi kwa kusukumwa na hisia, iwe ni tamaa ya kupata au kukwepa maumivu, yanakuwa siyo maamuzi sahihi. Kuondokana na hilo, fanya maamuzi kwa kufikiri na siyo kwa hisia.
4. Kupata vitu kwa udanganyifu. Hapa unadanganya kwa maneno au matendo ili kupata vitu unavyotaka, kitu ambacho siyo sahihi. Kuondokana na hili kuwa mkweli mara zote, sema kweli na fanya kilicho sahihi, itakupa utulivu mkubwa.
5. Kufanya mambo yasiyo na tija. Hapa mtu unachukua hatua ambazo hazina mchango wowote kwenye kusudi na malengo uliyonayo, inakuwa ni upotevu tu wa muda na nguvu zako. Kuondokana na hili jua kusudi na malengo yako kisha orodhesha mambo utakayoyafanya, ambayo yana mchango kwenye kusudi na malengo hayo. Usifanye kitu chochote ambacho hakina mchango wa kule unakotaka kufika.
Haya ndiyo mambo matano ambayo ukiyafanya kwa uhakika, utakuwa na siku tulivu kila siku, kwa sababu utapokea mambo kama yalivyo, utadhibiti hasira, utafanya maamuzi kwa kufikiri, utakuwa mkweli na utafanya yale yenye tija tu.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina mambo mengine ya msingi kutoka kwenye kitabu hicho na ambayo ukiyafanyia kazi kila siku utakuwa na maisha bora. Karibu usikilize kipindi hicho ili uweze kunufaika zaidi.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.