3323; Kuona thamani ya kitu.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Mwandishi mmoja amewahi kuelezea mazoea ya vitu tulivyonavyo kwa kutumia mfano wa samaki.
Aliandika kwamba samaki mzee alikuwa anapita na kukutana na samaki vijana wawili.
Samaki huyo mzee akawauliza; “Habari vijana, mnayafurahiaje maji leo?”
Samaki hao vijana wakamjibu kwa mshangao; “Maji! Ndiyo nini hicho?”

Mara nyingi sana huwa tumezoea vitu tulivyonavyo mpaka tunasahau kama vipo.
Ni mpaka pale tunapovipoteza vitu hivyo ndiyo tunagundua thamani yake.
Mfano mzuri na ambao tunaishi nao kila siku ni pumzi.
Ukiwa huna changamoto yoyote ya upumuaji, huwezi kuona kabisa thamani ya pumzi.
Unaweza kusahau kabisa kwamba kuna kitu kinaitwa pumzi, maana utaona maisha yanaenda tu.
Ni mpaka pale unapopata changamoto ya upumuaji na kukosa pumzi ndiyo unagundua jinsi kitu ambacho ulikuwa unakichukulia poa kina umuhimu mkubwa.
Hivyo ndivyo binadamu tulivyo kwenye mambo mengi ambayo yamekuwepo kwa uhakika.
Tunayazoea na kusahau thamani yake.
Ni mpaka pale tunapoyapoteza ndiyo tunagundua yalikuwa ya thamani.
Kuna watu tunakuwa nao kwenye maisha na kuwachukulia poa, tunapowapoteza ndiyo tunaona umuhimu wao.
Unaweza kuichukulia poa kazi au biashara unayofanya, kwa sababu haikulipi sana. Lakini utakapoipoteza ndiyo utagundua ilikuwa muhimu.
Kila kitu tulichonacho kwenye maisha tunapaswa kukithamini sana, kwa sababu kina mchango mkubwa kwa pale tulipo kwenye maisha yetu.
Iwe tunaona moja kwa moja au la, lazima tujue hakuna kitu ambacho ni cha ziada tu.
Na tunapaswa kuthamini vitu kabla hatujavipoteza na kuanza kujutia.
Tukiwa navyo tuna nafasi nzuri ya kuvithamini na kuvitumia kwa manufaa makubwa.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA ni wajibu wetu kuthamini kila kitu tulichonacho.
Tunafanya hivyo kupitia zoezi la shukrani tunalolifanya kila siku.
Kwa zoezi hilo, kila siku tunashukuru kwa vitu mbalimbali tulivyonavyo kwenye maisha yetu.
Zoezi hilo linatupa nafasi ya kupitia kila tulichonacho kwenye maisha yetu na kuona thamani na mchango wake kwa pale tulipofikia kwenye maisha.
Ni zoezi dogo lakini lenye nguvu kubwa sana.
Unapaswa kulifanya kila siku kama mwanajamii wa KISIMA CHA MAARIFA ili upeleke thamani sahihi kwenye vitu vyote ulivyonavyo.
Mara kwa mara jikumbushe maji ambayo upo ili uweze kuyafaidi wakati unayo na siyo kuja kujutia baada ya kuwa umeyapoteza.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe