Matajiri Wawekezaji,

Tunaendelea na masomo ya uwekezaji wa mifuko ya pamoja ya uwekezaji. Tumechagua kufanya uwekezaji huo kupitia UTT AMIS ambayo ina mifuko sita ya uwekezaji wa pamoja.

Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza mfuko wa kwanza wa UTT ambao ni mfuko wa Umoja.

Mfuko wa Umoja ni mfuko wa kwanza kuanzishwa na UTT AMIS mnamo tarehe 16 Mei 2005. Umoja ni mfuko wa wazi ambao tangu kuanzishwa kwake mwezi Mei 2005 una zaidi ya miaka 18 sokoni. Mfuko unawekeza katika hisa zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa na maeneo yenye vipato vya kudumu kama hatifungani za serikali.

Malengo Ya Mfuko

Mfuko wa Umoja unalenga zaidi wawekezaji wenye malengo ya muda wa kati na mrefu, jambo ambalo huwawezesha kupata muda wa kutosha kujiwekea akiba na kukuza mtaji kupitia uwekezaji.

Mfuko wa Umoja humpa mwekezaji hamasa na kumjengea desturi ya kujiwekea akiba na kupata faida itokanayo na uwekezaji kwenye soko la mitaji na dhamana nchini.

Ukwasi/Kuuza Vipande

Mfuko wa Umoja ni mfuko wa wazi ambao mtu anaweza kujiunga na kujitoa kwa wakati wowote anaotaka yeye. Mtu anajiunga kwa kununua vipande na kujitoa kwa kuuza vipande. Bei ya vipande wakati wa kununua na kuuza inatokana na thamani ya mfuko kwa wakati huo.

Malipo ya mauzo ya vipande yatashughulikiwa ndani ya 10 za kazi baada ya kupokelewa. Fedha zitatumwa moja kwa moja katika akaunti ya benki ya mwekezaji.

Nani Anaruhusiwa Kuwekeza

Wawekezaji wote ikiwa ni pamoja na watu binafsi, taasisi, makampuni, na vikundi vya jumuiya ya Afrika mashariki (EAC).

Sera Ya Mfuko

Mfuko unaruhusiwa kuwekeza kwenye hisa zilizoorodheshwa, ikizingatiwa kuwa kiasi cha pesa kitakachowekezwa kwenye sehemu hiyo kisizidi 50% ya uwekezaji wote wa mfuko na 50% inayobaki itawekezwa kwenye dhamana mbalimbali za serikali zenye ukomo tofauti, hatifungani za kampuni binafsi, na kwenye akaunti za amana.

Huu ni mfuko ambao unafanya uwekezaji wa mseto kwenye hisa, hatifungani na akaunti za amana. Mseto huo wa uwekezaji unaufanya mfuko kuwa salama zaidi, licha pia ya kufanya faida yake kuwa ndogo ukilinganisha na mifuko mingine.

Sifa Za Mfuko Wa Umoja

1. Vipande vinauzwa kwa thamani halisi [hakuna gharama za kujiunga].

2. Umiliki wa mtu mmoja au umiliki wa pamoja unaruhusiwa katika mfuko huu.

3. Kiwango cha chini cha kujiunga ni vipande 10 tu.

4. Gharama ya kujiondoa inayotozwa ni 1% ya thamani halisi ya kipande.

5. Urahisi wa kujiunga na kutoka – manunuzi na mauzo hufanyika kila siku ya kazi.

6. Mauzo ya vipande yanaruhusiwa na mwekezaji atapata fedha ndani ya siku 10 za kazi baada ya ombi la kuuza vipande kupokelewa katika ofisi za UTT-AMIS.

7. Mfuko unaruhusu uhamishaji wa vipande kutoka mwekezaji mmoja kwenda kwa mwekezaji mwingine.

8. Mwekezaji akifariki, mrithi, mwakilishi, au mwombaji wa pili ataruhusiwa kuendeleza uwekezaji huo.

9. Vipande vinaweza kutumika kama dhamana ya mkopo katika taasisi za fedha.

10. Hakuna kiwango cha juu cha uwekezaji.

Jinsi Ya Kuwekeza/Kununua Vipande

Kupitia simu yako ya mkononi piga *150*82# kufungua akaunti na kisha kamilisha usajili kwa kujaza fomu na kuifikisha katika ofisi za UTT AMIS au kutuma kwa barua pepe uwekezaji@uttamis.co.tz. Endelea kuwekeza kupitia benki au mitandao ya simu kama M-PESA, TIGOPESA, AIRTEL MONEY, HALOPESA na T-PESA.

Jinsi Ya Kutoa fedha/Kuuza Vipande

1. Kutumia menu ya simu au aplikesheni na kwenda sehemu ya kuuza vipande.

2. Kupakua fomu kwenye mtandao na kuijaza kisha kutumwa kwa barua pepe; uwekezaji@uttamis.co.tz.

3. Kufika ofisi za UTT AMIS au mawakala wake (benki) na kujaza fomu ya kuuza vipande.

Hali Ya Utendaji Kwa Mfuko Wa Umoja

Kwa miaka 18 ambayo mfuko wa Umekuwepo sokoni, umekua thamani ya kipande kutoka Tsh 70 kwa kipande mwezi Mei 2005 mpaka kufikia thamani ya Tsh 986 mwezi Januari 2024.

Hiyo ina maana mtu aliyewekeza Tsh milioni 1 mwaka 2005 angepata vipande 14,285 (1,000,000 /70). Mwaka 2024 uwekezaji huo ungekuwa umefikia Tsh 14,085,714 (14,285 x 986). Huo ni ukuaji wa mara 14 bila ya kufanya kitu chochote kile.

Kama mtu angeanza na mpango wa kuwekeza buku kila siku, yaani elfu 30 kila mwezi, tangu 2005 mpaka 2023, matokeo yangekuwa hivi;

Kiasi ambacho mtu atakuwa amewekeza ni; 6,480,000/=

Thamani ya uwekezaji inakuwa; 22,735,818/=

Ongezeko la thamani ni; 16,255,818/=

Hujachelewa.

Kwa kuangalia namba za nyuma kama hivi ni rahisi kuona labda umechelewa. Kwamba kama ungeanza zoezi hili mapema basi ungekuwa umenufaika sana.

Lakini ukweli ni hujachelewa, kwa sababu wakati sahihi kwako kunufaika na hili ilikuwa mwaka huo 2005. Lakini wakati mwingine sahihi ni sasa.

Kwa kuwa umeshakuwa na uelewa, sasa fanya kwa msimamo bila kuacha.

Tahadhari muhimu ya uwekezaji.

Kwenye mafunzo au ushauri wowote wa uwekezaji, tahadhari muhimu hupaswa kutolewa. Tahadhari hiyo ni; utendaji wa nyuma siyo dhamana ya  utendaji ujao (Past performance doesn’t guarantee future perfomance).

Hivyo pamoja na mwenendo mzuri wa mfuko huu wa umoja kwa miaka 18 ambayo umekuwepo, haiufanyi kuwa kitu cha uhakika wa asilimia 100. Bado hatari za uwekezaji zipo na hivyo kila mwekezaji anapaswa kuelewa hilo.

Kwa Nini Tumechagua Mfuko Wa Umoja.

 Kwenye programu ya NGUVU YA BUKU tumechagua mfuko wa Umoja kuwa ndiyo mfuko wa kipaumbele kwa uwekezaji kwa sababu zifuatazo;

1. Ukongwe wa mfuko na ufanisi wake mzuri wa kipindi chote ambacho umekuwepo. Kitu ambacho kimeweza kudumu kwa muda mrefu, kinadhihirisha kuna usahihi ambao upo.

2. Urahisi wa kila mtu kuweza kufanya uwekezaji hata kama kipato ni kidogo kabisa. Hakuhitajiki kianzio kikubwa mwanzoni kama ilivyo kwa mifuko mingine.

3. Sera ya mfuko ya uwekezaji wa mseto inapunguza hatari ya kutegemea eneo moja tu ambapo likipata changamoto hasara inakuwa kubwa.

Mjadala Wa Somo.

Karibu ushirikishe yale uliyojifunza kwenye somo hili kwa kujibu maswali yafuatayo;

1. Mfuko wa Umoja unafanya uwekezaji mseto. Nini maana yake na zipi faida zake kwa mwekezaji?
2. Kwa nini tumechagua mfuko wa umoja kama kipaumbele cha kwanza kwenye programu ya NGUVU YA BUKU?

3. Umekuwa unafanya shughuli za kuingiza kipato kwa miaka mingapi sasa? Kama kwa miaka hiyo yote ungekuwa unawekeza UTT kwa mpango wa NGUVU YA BUKU, ungekuwa na uwekezaji mkubwa kiasi gani? (tumia kikokotoo hiki; https://www.uttamis.co.tz/tools/monthly-calculator) Monthly Investment weka 30000, Expected Annual Return (%) weka 12 na Period (Years) weka miaka ambayo umekuwa unaingiza kipato.

Shirikisha majibu ya maswali hayo ili uendelee kuelewa kwa kina uwekezaji tunaofanya na kunufaika zaidi.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.