Ukilinganisha matokeo unayopata sasa na uwezo mkubwa uliopo ndani yako, ni kama hujafanya kitu kabisa. Yaani unayoweza kufanya ni makubwa sana ukilinganisha na ambayo umeshafanya sasa.
Na kinachokuzuia usiweze kufanya hayo makubwa wala hata siyo mambo ya nje, bali ni mambo ya ndani yako. Unajizuia wewe mwenyewe kufanya makubwa kwa breki ambazo umezishikilia.
Breki hizo umeziweka kwenye maeneo makuu manne ambayo ndiyo yanakujenga wewe. Maeneo hayo ni mwili, akili, roho na hisia. Mwili ndiyo unaotenda, akili inafikiri, roho inanuia na hisia zinakupa msukumo. Vikwazo kwenye maeneo hayo manne ndivyo vimekuwa vinawazuia wengi kufanikiwa.

Kuna njia nyingi za kuachilia breki ili uweze kufanya makubwa. Kwenye somo la nyuma tumejifunza kutumia tahajudi kuachilia breki zinazokuzuia kufanikiwa. Unaweza kusoma hapa; Tahajudi (Meditation) Ya Kuachilia Breki Zinazokuzuia Kufanikiwa.
Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza jinsi ya kutumia malengo kuachilia breki zinazokuzuia kufanikiwa. Malengo ni muhimu kwenye maisha ya kila mtu, kwa sababu ndiyo yanayoelekeza nini mtu afanye na asifanye.
Wale ambao hawana kabisa malengo wamekuwa wakihangaika na mambo mengi, wanapoteza nguvu na muda na hawapati wanachotaka. Kutokuwa na malengo kabisa ni upotevu ambao umewakwamisha watu. Kwa nje wanaweza kuonekana wanaweka juhudi kubwa, lakini kwa ndani juhudi hizo hazina maana kabisa.
Kwa upande wa pili kuna ambao huwa wanaweka malengo, lakini bado pia wanashindwa kufanya makubwa. Hawa ni wale ambao kila mwanzo wa mwaka huwa wanaweka malengo mbalimbali, lakini haiwachukui muda mrefu kabla hawajaachana na malengo hayo na kurudi kwenye mazoea yao.
Wengi hushindwa licha ya kuweka malengo kwa sababu jinsi wanavyoweka malengo hayo hawawajibiki kuyatekeleza. Inakuwa ni kama kitu tu cha kujifurahisha, lakini hakipewi uzito ambao unastahili kuwekwa ili matokeo yaweze kupatikana.
Katika kuweka malengo ambayo yatakuwezesha kuachilia breki zinazokuzuia kufanikiwa, kuna mabadiliko makubwa unayopaswa kuyafanya. Mabadiliko hayo ni kuyageuza malengo kuwa ahadi. Wote tunajua kauli ya ahadi ni deni, kwamba ukiahidi basi lazima utimize. Unapoyageuza malengo kuwa ahadi, unalazimika kuyatekeleza ili kutimiza ahadi hiyo.
Kwenye kuyageuza malengo kuwa ahadi, unapaswa kuyapanga kwenye hatua saba ambazo zitakuwezesha kuachilia breki kwenye maeneo yote manne ya mwili, akili, roho na hisia.
Hatua ya kwanza ni kueleza NINI hasa unachotaka. Hii ni hatua muhimu ya kueleza kwa uhakika kile unachotaka. Hapa hupaswi kutumia kauli za jumla kama kuongeza kipato, bali unapaswa kueleza kwa uhakika ni kipato kiasi gani unataka kuongeza.
Hatua ya pili ni kueleza LINI utakuwa umepata unachotaka. Malengo na ahadi unayoweka lazima yawe na tarehe ya ukomo, la sivyo hakutakuwa na msukumo wa kufikia. Kwenye lini unaweka tarehe ya ukoko ambayo kufikia hiyo utakuwa umekamilisha malengo hayo.
Hatua ya tatu ni WAPI utatekeleza ahadi na malengo yako. Hapa unaeleza kabisa ni wapi utakapofanyia utekelezaji wa malengo unayoweka. Hii inahakikisha kwamba hubahatishi, unaweka mpango ambao unaufanyia utekelezaji wa uhakika.
Hatua ya nne ni KWA NINI upate kile unachotaka. Hapa unaeleza msukumo mkubwa unaokufanya ufikie kile unachotaka. Safari ya kufikia malengo haitakuwa rahisi, kwani ina vikwazo na changamoto mbalimbali. Bila ya kwa nini kubwa inayokusukuma, utaishia njiani.
Hatua ya tano ni NANI utakaoshirikiana nao kutimiza malengo. Huwezi kufanikiwa peke yako, unahitaji ushirikiano na msaada wa wengine ili kuweza kujenga mafanikio unayoyataka. Kwenye malengo na ahadi unayoweka, lazima uainishe kabisa watu watakaohusika katika kukamilisha.
Hatua ya sita ni VIPI unakwenda kukamilisha kutimiza malengo na ahadi. Huu ndiyo mpango mzima wa utekelezaji ili kuweza kufikia malengo uliyoweka. Ni hatua kwa hatua za jinsi ya kufikia malengo uliyoweka.
Hatua ya saba ni HISIA utakazokuwa nazo baada ya kufikia malengo. Unapaswa kuanza na hisia hizo kabla hata hujayafikia malengo hayo ili uweze kuwa na msukumo wa kuyaendea licha ya kukutana na vikwazo.
Kwa kufanyia kazi hatua hizi saba, utaweza kufikia uwezo mkubwa ulio ndani yako na kuutumia kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina zaidi zoezi zima la kutumia malengo kuachilia breki na kufanya makubwa. Karibu usikilize kipindi, uelewe kwa kina na kuweza kufanya makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.