Rafiki yangu mpendwa,

Ukiiona mbegu ya harage ambayo imekaa mahali, unaweza kuidharau na kuona kama haina kitu kikubwa ndani yake. Lakini mbegu hiyo inapowekwa kwenye ardhi yenye rutuba, ikapata maji na mbolea, inatoa mmea ambao unatoa mbegu nyingi za maharage.

Hivyo ndivyo kila kiumbe hai kilivyo, bila ya kujali mwonekano wake wa nje, ndani kinakuwa na uwezo mkubwa sana. Kwa bahati mbaya sana, viumbe hai wengi huwa hawawezi kutumia huo uwezo mkubwa ulio ndani yake.

Na kiumbe anayeongoza kwenye hilo ni sisi binadamu. Angalau wanyama wengine huwa wanaishi uhalisia wao, hawajidanganyi kama binadamu. Hutamkuta simba akila nyasi kwa sababu amekosa swala, atawinda mpaka apate nyama. Lakini kwa binadamu, ni rahisi watu kuendea kitu tofauti na kile wanachotaka, kwa sababu tu wanachokitaka kimekuwa kigumu.

Lakini ambacho watu wamekuwa hawapati nafasi ya kujua ni kwamba ndani yao wana uwezo mkubwa sana, uwezo wa kufanya makubwa na kupata chochote kile wanachokitaka.

Kwa bahati mbaya sana, huo uwezo mkubwa huwa umelala ndani ya watu na kutokutumika vizuri. Lakini habari njema ni kwamba uwezo huo huwa haupotei, hata kama mtu hajautumia kabisa, hauondoki, unakuwa bado upo, ila umekuwa umelala.

Hiyo ina maana kwamba, mtu, katika wakati wowote ule wa maisha yake, anapoamua kutumia uwezo huo, anaweza kufanya hivyo. Anachohitaji kufanya ni kuuamsha uwezo huo na kuutumia kwa namna anavyotaka yeye mwenyewe.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimekushirikisha kwa kina kuhusu uwezo huo mkubwa ulio ndani yako na jinsi unavyoweza kuufikia na kuutumia kufanya makubwa. Ndoto zote kubwa ambazo umewahi kuwa nazo kwenye maisha yako, zinawezekana kabisa kama utafikia na kutumia uwezo huo.

Karibu ujifunze kwenye kipindi hiki cha ONGEA NA KOCHA na uache kujidhulumu wewe mwenyewe kwa kuacha uwezo huo mkubwa kuendelea kulala ndani yako. Kipindi kipo hapo chini, jifunze na uchukue hatua ili uweze kufanya makubwa na kuyabadili kabisa maisha yako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.