3335; Hujui unachotaka?
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Hakuna kitu kinachoshangaza kama idadi kubwa ya watu ambao unakuta wanaomba ushauri wafanye nini na maisha yao.
Na wengine wengi ambao wamekuwa wanachukua na kufanyia kazi kila aina ya ushauri unaotolewa bure wa nini mtu anapaswa kufanya kwenye maisha yake.
Ni jambo la kushangaza kwa sababu hakuna mtu wa nje yako ambaye anaweza kukuambia kwa usahihi nini unachopaswa kufanya.
Watu wanaweza kubahatisha tu kuhusu vitu unavyoweza kufanya.
Lakini kujua kile hasa unachopaswa kufanya, ambacho ndiyo kimebeba mafanikio yako yote, inaanzia ndani yako.
Hayupo mtu wa nje anayeweza kujua hilo kwa uhakika, ni wewe mwenyewe.
Tukienda upande wa kuchukua chukua kila aina ya ushauri unaotolewa juu ya nini mtu anapaswa kufanya, na ambao unabadilika kila mara, imekuwa ni mahangaiko kwa wengi.
Kila wakati unawakuta watu wakikimbizana na fursa mpya ambazo hata hawadumu nazo kwa muda mrefu.
Kutafuta urahisi na njia za mkato za kupata mafanikio makubwa bila ya kuweka kazi ni kitu kingine ambacho kimekuwa kinawakwamisha watu.
Mwanzo wanaanza na kile hasa kinachotoka ndani yao. Lakini wanapokutana na ugumu, hatua ambayo lazima kila mtu anaipitia, wanaacha na kwenda kwenye mengine wanayoona ni rahisi.
Huko nako mambo hayawi rahisi kama yalivyoona, bali vikwazo na changamoto zinakuwepo pia.
Rafiki, kama bado unahangaika na hayo maswali ya nini ufanye au unakimbizana na kila ushauri wa fursa mpya, swali langu ni hujui unachotaka?
Pale ambapo sauti inakuja ndani yako ikikueleza kila unachopaswa kufanya, kwa nini huwa unaipuuza?
Pale unapopata msukumo wa kipekee kwenye baadhi ya mambo, kwa nini unauhamishia msukumo huo kwenye nambo mengi yasiyo na tija.
Rafiki, ukijiheshimu, ukajisikiliza na kujikubali, tayari una kila unachohitaji kwa ajili ya mafanikio yako makubwa.
Unapojikwamisha ni kwenye kuhangaika na mambo mengi yasiyokuwa na tija kwako.
Utaendelea kupata mafunzo, ushauri na usimamizi wa karibu kwenye kufanyia yale uliyochagua kufanya.
Lakini maamuzi ya mwisho ni yako peke yako, kwa kuhakikisha maamuzi yanaendelea kubaki kuwa yako
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, kila mtu anapaswa kujisikiliza hasa kile anachotaka.
Haipaswi mtu kujiuma uma katika kujieleza nini hasa anacho anakitaka kwenye maisha yake yote.
Unapokuwa kwenye jamii hii, unakuwa ni mtu unayejua ni wapi hasa unakwenda.
Huwi tena mtu wa kujaribu vitu visivyofanya kazi.
Tayari unakuwa umetingwa sana na kile hasa unachotaka kiasi cha kutokuwa na nafasi ya kuhangaika na mengine.
Hiyo ina maana kwamba, kama unapata muda wa kuhangaika na mambo yasiyokuwa na tija kwako, ni kiashiria kwamba huna makubwa unayopambania.
Kama huna makubwa unayoyapambania, hakuna matokeo mapya utakayoweza kuyazalisha.
Isikilize vizuri sauti iliyo ndani hako, hiyo tayari inajua nini hasa unachotaka.
Pata mafunzo na ushauri wa namna ya kuendelea na kile ambacho ndiyo chaguo lako kuu.
Pambana hasa mpaka kukamilisha hilo.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe