Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Hongera sana kwa kuendelea kuwa msomaji mzuri wa makala za ukamilishaji ambao huwa unaupata hapa kila siku ya jumatano.
Karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ukamilishaji.
Kwenye jumatano ya leo ya ukamilishaji, tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.
Habari njema ni kwamba leo katika mbinu za ukamilishaji wa mauzo, tunakwenda kujifunza mbinu namba 19 na 20 zitakazokusaidia kukamilisha mauzo yako pale mteja anapokuwa anakuwekea mapingamizi mbalimbali ya kukuzuia wewe usimuuzie.
19. Ukamilishaji wa kuwa na shukrani.
Huu ni ukamilishaji mkali ambao unahitaji mtu ujiamini na kujikubali pale unapoutumia.
Mteja anakuwa na pingamizi kuhusu kile unachotaka kumuuzia lakini mteja huyo unajua wazi anao uwezo wa kukamilisha hayo mauzo ila anakuwa analalamika tu. Hapo ndipo unapotumia hii mbinu na kumwambia mteja,
“Nakubaliana na wewe, unapaswa kuwa na shukrani unaweza kuwekeza kiasi hiki cha fedha.
Siyo watu wote wanaweza kumudu. Kuna watu hawana hata kitu cha kula, lakini wewe una nafasi ya kuweza kuwekeza kwenye hili. Nahitaji uthibitisho wako hapa, nahitaji tukamilishe hili, kinachofuata baada ya hapa lipia uchukue bidhaa au huduma yako. Lipia ili ukafurahie uwekezaji wako.
Muuzaji bora kuwahi kutokea, huu ni ukamilishaji mkali ambao unahitaji mtu ujiamini na kujikubali. Ni ukweli ambao unaweza kumuumiza mtu na siyo watu wote wapo tayari kuukabili ukweli. Lakini ni ukamilishaji wenye nguvu kubwa, kuwa imara kwenye kuutumia.
20. Ukamilishaji wa pongezi.
Wakati mwingine unapouza, mteja anaweza kulalamika kuhusu gharama au chochote kile kinachuhisiana na mapingamizi ya mteja.
Badala ya kuona mteja kama ni msumbufu, wewe mpongeze kwenye kile anachotaka kununua. Tumia uwekezaji mkubwa aliofanya kumsifia na kukamilisha mauzo.
Na pale unapouza pendelea sana kutumia neno uwekezaji, hii itamfanya mteja aone anawekeza na si vinginevyo.
Kwa mfano, unamwambia mteja,
“Najua ni uwekezaji mkubwa na unapaswa kujipongeza kwa kuweza kufanya uwekezaji mkubwa kiasi hiki. Siyo kila mtu anaweza kufanya uwekezaji wa aina hii. Nahitaji uthibitisho wako hapa, nahitaji tukamilishe hili, nahitaji ulipie sasa ili uende ukafurahie uwekezaji wako.
Ukamilishaji huu unatumia pingamizi lao kama sababu ya wao kukamilisha mauzo. Kwa kuwataka wajipongeze unawafanya waone ni kitu sahihi wanafanya.
Tumia mapingamizi mbalimbali wanayokupa wateja na kuyatumia mapingamizi hayo kuwashawishi kununua kupitia kile unachouza.
Pale unapokutana na mteja ambaye anakupa pingamizi la bei juu, mpongeze kwa uwekezaji mkubwa anaotaka kufanya kwa sababu ni watu wachache ambao wanaweza kuwekeza kama yeye.
Lakini pia, kuwataka wateje wawe na shukrani kwa kuwa wanao uwezo wa kumudu kulipia kiasi hicho cha uwekezaji kupitia kile unachouza.
Hatua ya kuchukua leo; chagua mbinu moja au zote mbili, nenda kazitumie mbinu hizi mbili kwenye mchakato mzima wa kukamilisha mauzo na utaweza kufanikiwa kwenye mauzo yako.
Kikubwa, tumia mbinu hizi kwa kujiamini na utaweza kuuza sana.
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mkufunzi wa mauzo.
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz
