Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Hongera sana kwa kuendelea kuwa msomaji mzuri wa makala za ukamilishaji ambazo ni mwendelezo wa kila wiki.
Kabla hatujaendelea, kwanza tujikumbushe kidogo kauli mbiu yetu ya ukamilishaji inayosema, ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.
Kwenye somo lililopita tulijifunza mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo na tulijifunza mbinu namba 19 na 20.
Natumaini ulizifanyia kazi na ukapata mrejesho mzuri.
Kama ulizifanyia kazi mbinu namba 19 na 20 au yoyote ile kati ya zile ambazo umejifunza hapa tafadhali shirikisha maoni yako.
Rafiki, ni wajibu wako wa kimaadili kabisa kuuza na ili uweze kuuza unapaswa umshawishi mteja kukamilisha malipo ya kile unachotaka kumuuzia.
Usione aibu kumwambia mteja lipia, kwa sababu kitendo cha mteja kulipia na wewe kupata hela, ndiyo ushindi wa mauzo.
Mbinu Mbili Za Uhakika Za Ukamilishaji Wa Mauzo 19-20
Unapaswa kufanya mauzo yako kuwa kitu unachopenda kwa sababu kuuza ni raha. Kupitia kukamilisha mauzo, unapata kile unachotaka kwenye maisha yako.
Huoni kukamilisha ni raha? Kama ni ndiyo, msukumo wa kukamilisha unapaswa uanzie ndani ya kabisa, upambane kwa namna namna yoyote ile kuhakikisha unauza.

Pata picha, hicho unachouza ni kitu kinachokwenda kuokoa maisha ya mtu na kuyafanya kuwa bora. Usimwambie mteja kuhusu kile unachouza maana yake unafanya makusudi kufanya maisha ya wengine yasiwe bora kupitia wewe.
Kwenye mbinu ya 21 na 22 tunakwenda kujifunza mbinu nyingine mbili za uhakika zitakazokwenda kukusaidia wewe kuweza kukamilisha wateja wengi.
Hizi ni mbinu za ukamilishaji ni kali, unapaswa uzitumie kwa kujiamini na wakati mwingine unapaswa kuwa mbabe na siyo mnyonge kwenye ukamilishaji. Hii ni vita rafiki, ni vita isiyoruhusu umwagaji wa damu.
Mteja akapokupa vipingamizi, wewe vitumie hivyo kumshawishi kununua kulingana na aina ya mbinu ya ukamilishaji.
- Ukamilishaji wa kufanya tu.
Huu ni ukamilishaji mkali unaoweza kuonekana ni wa kumlazimisha mteja.
Lakini ni wa kumsaidia afanye maamuzi bila hata sababu yoyote, kwa sababu kwa vyovyote vile watu huwa wanafanya manunuzi nje ya bajeti zao.
Kwa mfano, unakutana na mteja ambaye anakuambia ni fedha nyingi, wewe mjibu hivi;
“Naelewa ni fedha nyingi kuliko bajeti uliyokuwa nayo, lakini fanya tu.”
Unapotumia ukamilishaji wa aina hii, wanunuaji wanakuheshimu.
Hivyo utumie vizuri sana ukamilishaji huu ili ukapatie matokeo mazuri.
- Ukamilishaji wa ugonjwa.
Ukamilishaji huu unaweza kuonekana wa kushinikiza, lakini msingi wake ni mapingamizi mengi ambayo wateja wanakupa siyo halisi, ni malalamiko tu, hivyo hupaswi kuyapa uzito, kubaliana nao kisha wape sababu ya kukamilisha.
Kwa mfano, unamwambia mteja;
“Najua ni zaidi ya unavyohitaji na ulivyopanga kutumia, lakini huu siyo ugonjwa. Siyo kwamba utakufa ukifanya haya maamuzi. Weka sahihi yako hapa, tukamilishe hili, nahitaji ulipie sasa ili uende ukafurahie uwekezaji wako au bidhaa yako”.
Rafiki na muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea, ukikutana na mteja kukupa malalamiko mengi, wewe chagua silaha kati ya hizi za kumkamilisha.
Mpaka leo tuko mbinu ya 22, hivyo unazo mbinu nyigi, je, mpaka sasa unakumbuka mbinu gani kichwani kiasi kwamba akija mteja, wewe ni kuzitumia na kukamilisha mauzo.
Hatua ya kuchukua leo; nenda leo katumie mbinu hizi za ukamilishaji ambazo ni ukamilishaji wa kufanya tu, mteja anapokupa pingamizi, mwambie naelewa ni fedha nyingi kuliko bajeti uliyokuwa nayo, lakini fanya tu.
Na pale mteja anapokuwa anakupa pingamizi lolote lile ambalo siyo halisi bali ni malalamiko tu hupaswi kuyapa uzito bali wewe kukubaliana naye kisha mwambie,
Najua ni zaidi ya unavyohitaji na ulivyopanga kutumia, lakini huu siyo ugonjwa.
Siyo kwamba utakufa ukifanya haya maamuzi.
Tafadhali, tukamilishe hili, nahitaji ulipie sasa.
Kitu kimoja zaidi, watu huwa wanafanya manunuzi ya kununua kwa hisia na siyo mantiki.
Kwa kila unachouza, jua hisia zinazowasukuma wateja kwenye hicho unachowashawishi kununua.
Jua tamaa na hofu ambazo wateja wanazo na zitumie kuwashawishi Kununua.
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mkufunzi wa mauzo.
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz