Habari njema rafiki na muuzaji bora kuwahi kutokea,
Karibu sana katika mwendelezo wa makala zetu za ushawishi.
Leo, ikiwa ni jumamosi ya ushawishi, tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Kila jumamosi hapa tunajifunza mbinu za ushawishi, na kama utakua unazitumia, zitumie kwa manufaa chanya na siyo hasi.
Ili tupate kibali cha kuendelea na somo la leo, tujikumbushe kidogo wiki iliyopita tulijifunza nini. Kwenye somo lililopita, tulijifunza kwamba njia ya tano ya kuwafanya watu wakukubali kwenye kila eneo la maisha yako, ni kuongelea kile ambacho mtu anapendelea zaidi. Hivyo basi, kama unataka kutaka mioyo ya watu, ongelea yale ambayo mtu anapendelea na utaweza kuwateka.
Na kwenye mauzo, jua wateja wako wanapendelea nini na kisha ongelea yale ambayo wateja wako wanayapendelea.
SOMA;
Njia Ya Tano Ya Kuwafanya Watu Wakukubali Kwenye Kila Eneo La Maisha Yako
Habari njema ni kwamba kwenye somo letu la leo, tutajifunza njia ya sita ya kuwafanya watu wakukubali kwenye maisha yako ni ; mfanye mtu mwingine ajione ni wa muhimu na fanya hivyo kwa dhati.
Kuna sheria kuu moja muhimu sana kwenye mahusiano ya wanadamu. Kama ukiijua na kuiheshimu sheria hiyo, kamwe hutaingia kwenye changamoto na watu.
Kwa kufuata tu sheria hiyo, utajijengea marafiki wengi na kuwa na mahusiano bora. Lakini pia, unapovunja sheria hiyo, unakaribisha matatizo ya kila aina.
Sheria yenyewe ni hii hapa; mara zote mfanye mtu mwingine ajione yeye ni wa muhimu zaidi.
Kujiona wa muhimu ndiyo hitaji kuu ambalo kila mtu analo. Unapompatia mtu nafasi hiyo, anaona unamthamini na kuwa tayari kukubaliana na wewe.
Tukiangalia wanafalsafa kama Confuncius, buddha walihubiri sheria hiyo kabla ya Yesu.
Naye Yesu alijumuisha sheria hii kwa kusema; watendee wengine, kile ambacho ungependa wakutendee wewe.

Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea, hiyo ndiyo sheria ambayo ukiifuata kila siku kwenye maisha yako, mauzo na kwa kila unayekutana naye, utaweza kuwa na mahusiano bora na ushawishi kwa wengine.
Je, unapenda kuonekana wa muhimu? Wafanye wengine kuwa wa muhimu na watakubaliana na wewe.
Kwenye mauzo na hata maeneo mengine, wafanye watu kuwa wa muhimu kwa kutumia kauli kama, naomba unisaidie, tafadhali, samahani kwa kukusumbua, asante,karibu ni kauli ambazo zinamfanya mtu ajione yeye ni wa muhimu na umemthamini.
Kitendo tu hata cha mteja kununua na kumwambia aasante ni ishara ya kumthamini na kumuona yeye ni wa muhimu.
Kauli kama asante sana, karibu sana zina nguvu sana licha ya kuonekana za kawaida. Kauli hizi zina nguvu za kuwafanya watu wajione ni wa muhimu hasa kwenye mazingira ambayo hayawapi nafasi ya kuona ni wa muhimu. Kwa mfano, umeenda kupumzika mahali na kuagiza kinywaji chako, sasa mhudumu kakuletea soda aina ya mirinda lakini wewe unataka fanta.
Badala ya kumwambia umekosea na hujamwagiza hivyo, mwambie, “samahani kwa kukusumbua, huwa napendelea zaidi fanta kuliko mirinda.”
Atakuwa tayari kubadili huku akiwa na furaha kwa sababu umemfanya ajione yeye ni wa muhimu.
Kitu kimoja zaidi, ukweli unaopaswa kuujua ni kwamba, kila mtu unayekutana naye, anajichukulia yuko juu zaidi kwenye kitu fulani.
Sina uhakika kama itakufaa lakini njia rahisi ya wewe kuingia kwenye mioyo yao ni kuwaonesha kweli wako juu kwenye kitu hicho na kuwa tayari kujifunza kutoka kwao.
Na ukifanya hivyo kwa dhati kabisa na watakuwa tayari kukubaliana na wewe.
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mkufunzi wa mauzo.
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz