KAMA UNATAKA KURAHISISHA MAISHA YAKO FANYA HIVI.

Jitihada nyingi tunazofanya hapa duniani ni kwa sababu ya kutaka kurahisisha maisha. Mabadiliko makubwa na uvumbuzi wa kisayansi unafanyika kwa sababu binadamu tunatafuta njia za kufanya maisha yawe rahisi na bora.
  Hata wewe unaweza kurahisisha na kuboresha maisha yako na ya wenzako bila ya kuwa mgunduzi ama mwanasayansi mkubwa. Kuna kitu kimoja ambacho ukiweza kufanya basi maisha yako yatakuwa rahisi, bora na ya kufurahia siku zote.
  Binadamu tunafuga wanyama mbalimbali kwa sababu mbali mbali. Tunafuga kuku ili kupata mayai na nyama, tunafuga ng’ombe na mbuzi ili kupata maziwa, nyama na ngozi. Kila mnyama anaefugwa na binadamu kuna kitu ambacho binadamu anafaidika kutoka kwake. Umewahi kujiuliza ni faida gani binadamu anaipata kwa kufuga mbwa? Unaweza kusema tunafuga mbwa kwa sababu ya ulinzi ila kwa nini tusigefunga simba ama chui ambao ni wakali zaidi wawe walinzi? Kuna watu wengi sana wanaofuga mbwa na sio kwa sababu ya ulinzi.

  Sababu kuu ya binadamu kufuga mbwa ni upendo na urafiki. Mbwa ni rafiki mkubwa wa binadamu, ni kiumbe anaetoa upendo wa kweli kwa rafiki yake. Kama umewahi kufuga mbwa ama kuna mtu anaefuga mbwa umewahi kuna jinsi mbwa anavyofurahia anapomwona mmiliki wake anamkaribia. Hata sababu kuu ya mbwa kuwa mlinzi ni kwa sababu ya kumpenda sana binadamu na hivyo kumlinda yeye na mali zake. Hana ubinafsi wa kujipenda yeye mwenyewe, bali anampenda sana rafiki yake ambae ni binadamu. Hata mbwa koko wanaozunguka mitaani wamekuwa vile baada ya kufundishwa chuki na binadamu, kwa kupigwa na kutopewa upendo wowote.

 Ni somo gani unaloweza kujifunza kutoka kwa mbwa? Mbwa anapata maisha yake kwa kutoa tu upendo. Mbwa anakula, analala na kupata huduma nyingine kwa kutoa upendo wa kweli kwa wanadamu.
  Hii ina maana kwamba hata sisi tukiweza kutoa upendo wa kweli kwa wanaotuzunguka tutakuwa na maisha rahisi na bora. Tunaweza kuishi duniani bila ya gharama kubwa kwa kutoa tu upendo kwa wanaotuzunguka iwe kwenye familia, kazi au jamii inayotuzunguka.
  Hakuna kinachoweza kushinda upendo, hakuna tatizo lolote linaloshindwa kutatuliwa kwa upendo. Na upendo ni moja ya vitu ambavyo hutopungukiwa kwa kuvitoa na kila mtu hata awe masikini kiasi gani anaweza kutoa.(soma; vitu vitatu unavyoweza kutoa na usipungukiwe)
  Jamii na dunia inahitaji upendo kuliko kitu kingine chochote. Tuanze kwa kutoa upendo na maisha yetu yatakuwa bora na rahisi hapa duniani. Matatizo makubwa tunayokutana nayo yanasababiswa na kukosekana kwa upendo.(soma; dunia haihitaji silaha wala vita)
  Kama kuna kitu kimoja unachoweza kutoa sasa na ukabadili maisha ni upendo. Anza sasa kuonesha upendo kwako na kwa wanaokuzunguka.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: