Nidhamu binafsi ni moja ya vitu muhimu sana ambapo kila binadamu anapaswa kuwa nacho. Nidhamu binafsi ndiyo inayokuwezesha kufanya maamuzi na kuweza kusimamia maamuzi hayo hata kama mambo yatakuwa magumu kiasi gani. Nidhamu binafsi itakuwezesha kuepuka kuwa na uteja wa tabia fulani, kuondoa uvivu na kukufanya uweze kuendelea kufanya kitu mpaka mwisho.
Nidhamu binafsi ndio msingi wa mafanikio.
Bila ya nidhamu binafsi hakuna mafanikio. Nidhamu binafsi ni muhimu sana kwako kuweza kufikia mafanikio makubwa, ndio msingi mkuu wa kufikia mafanikio.
Ukiwa na nidhamu binafsi utaweza kuvumilia na kuendelea na mipango yako hata kama mambo yakiwa magumu. Kumbuka katika jambo lolote unalofanya au unalotegemea kufanya kuna changamoto nyingi. Na changamoto nyingine zinaweza kuwa kubwa kiasi cha kuweza kukata tamaa. Unapokuwa na nidhamu binafsi inakusaidia kuwa na uvumilivu na hatimaye kuzila mbivu. Watu wote waliofanikiwa walikuwa wavumilivu na hawakukata tamaa.
Nidhamu binafsi itakusaidia uweze kujidhibiti kitu ambacho ni muhimu sana ili kuweza kufikia mafanikio. Japokuwa una uhuru wa kufanya chochote unachotaka na maisha yako ikiwa ni halali, sio kila kitu unaweza kukifanya na ukaweza kufikia mafanikio. Kuna baadhi ya vitu ukivifanya vinaweza kukuzuia kufikia mafanikio. Nidhamu binafsi inakufanya uweze kujidhibiti wewe mwenyewe, japo unapenda kupumzika basi upumzike kwa kiasi, japo unapenda kupata starehe, basi ustareheke kwa kiasi na memngine mengi.
Nidhamu binafsi inakuwezesha kuepuka usumbufu na majaribu. Kuna usumbufu mkubwa sana kwenye dunia ya sasa. Kuna kila aina ya teknolojia ambayo inaweza kupoteza muda wetu kwa kiasi kikubwa sana. Kwa mfano ukichukulia hii mitandao ya kijamii, ina mvuto mkubwa sana wa kutaka kuwepo kwenye mitandao hii na kupiga soga na watu wengine. Lakini usipokuwa makini utajikuta muda mwingi unaumaliza kwenye mitandao hii na hivyo kushindwa kufanya mambo yatakayokuletea mafanikio. Pia kuna majaribu mengi sana na hata tamaa za hapa na pale. Nidhamu binafsi ndio itakuwezesha kuachana na vitu hivi na kuelekeza akili yako kwenye kufikia mafanikio makubwa.
Unapokuwa na nidhamu binafsi inakufanya uweze kujiamini, kujithamini na hatimaye kuweza kuwa na furaha na kuweza kufikia mafanikio makubwa. Ukosefu wa nidhamu binafsi unasababisha kushindwa, kupoteza, afya mbovu, matatizo kwenye mahusiano na hata kuondoa furaha.
Faida za nidhamu binafsi.
Pamoja na kuwa nidhamu binafsi ndio msingi wa mafanikio, pia nidhamu binafsi inaweza kukusaidia katika mambo yafuatayo;
1. Kuepuka kufanya maamuzi ya haraka yanayoendeshwa na hisia. Kama umekosa nidhamu binafsi inakuwa rahisi kwako kufanya maamuzi pale unapokuwa na hisia za furaha sana au hasira sana. Mara zote maamuzi ya aina hii hukufanya ujutie baadae.
2. Kutimiza ahadi ulizotoa kwa wengine. Nidhamu binafsi itakusukuma uweze kutimiza ahadi ulizotoa kwa wengine na hii itakujengea heshima kubwa na kukuwezesha kufikia mafanikio. Kukosa nidhamu binafsi kutakufanya uahidi mambo ambayo huwezi kuyatekeleza na hivyo kupoteza uaminifu na heshima.
3. Kuishinda uvivu na kuepuka kufanya mambo. Mara nyingi sana kuna mambo ambayo tunayojua ni muhimu kufanya ila bado tunakwepa kuyafanya. Unapokuwa na nidhamu binafsi unaweza kufanya kile ulichopanga kufanya iwe unajisikia kufanya au hujisikii kufanya. Kwa njia hii utaweza kufikia mafanikio makubwa.
4. Kuweza kufanya mazoezi, au kukaa chini na kusoma badala ya kuangalia tv au kuzurura kwenye mitandao ya kijamii. Ili uweze kufikia mafanikio makubwa ni lazima kujifunza kila siku, na pia ni muhimu kuwa na afya imara. Unapokuwa na nidhamu binafsi unaweza kufanya mambo hayo licha ya kwamba kuna mambo mengine yanayoshawishi uyafanye ambayo yanaonekana kuwa na raha zaidi.
5. Kuweza kula vizuri na kwa afya. Nidhamu binafsi inakuwezesha kufuata utaratibu wako wa chakula utakaokuhakikishia kuwa na afya nzuri. Kwa mfano chipsi ni tamu na kila mtu anapenda kula chipsi. Lakini chipsi hizi sio nzuri kwa afya yako. Kama umekosa nidhamu binafsi, kila utakapokuwa na njaa na ukaona chipsi itakuwa rahisi kwako kutaka kula.
6. Kuweza kuamka asubuhi na mapema. Kuamka asubuhi na mapema ni moja ya mahitaji ya kuweza kufikia mafanikio. Lakini usingizi nao ni mtamu sana. Je ni kitu gani kitakuwezesha uamke asubuhi na mapema na kuuacha usingizi mtamu? Ni nidhamu binafsi ndio inayoweza klukusukuma kufanya hivyo.
Nidhamu binafsi ni muhimu sana kwenye maisha ya kila binadamu na ndio hitaji la msingi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Anza kujenga na kuendeleza nidhamu binafsi ili uweze kudhibiti maisha yako na hatimaye uweze kufikia mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri kwenye safari ya kufikia mafanikio makubwa.
TUKO PAMOJA.