Kwa kawaida binadamu tumepewa saa 24 tu kwa siku. Huu ni muda ambao kila binadamu amepewa kuutumia kwa kadri anavyotaka. Kwa wale wanaotumia muda huu vizuri wa saa 24 kwa siku  matokeo makubwa ya maisha yao huonekana ,lakini kwa wale wanao tumia muda huu vibaya, kuharibikiwa na kuishi maisha ya utupu, maisha yasiyokuwa  na pesa siku zote hutokea.
Ili sasa tuwe na mafanikio makubwa na kufikia ndoto zetu kubwa tulizojiwekea hatuna budi kutunza  muda wetu kila siku. Muda ni kila kitu katika maisha yako kama utapoteza muda ujue unapoteza maisha yako na unajitengenezea mwenyewe njia ya kushindwa.
Pamoja na umuhimu wa muda katika suala zima la maendeleo binafsi, watu wengi wamekuwa wakijikuta wakipoteza muda sana katika maisha yao. Ukitaka kuhakikisha hili weka ahadi na mtu ya kukutana sehemu, hapa utapata majibu mazuri ni jinsi gani watu wengi hawajali muda.
Muda wako umekuwa ukipotea katika vitu unavyofanya kila siku iwe kwa kujua au kutojua lakini muda umekuwa ukiupoteza sana. Ni muhimu kujua na kuwa makini na vitu vinavyokupotezea muda wako, vinginevyo utazidi kufanya maisha yako kuwa magumu zaidi kila siku.
Kumbuka ili ufanikiwe zaidi kwa kile unachofanya unahitaji muda, kama utazidi kupoteza muda, hiyo ina maanisha hautaweza kuzifikia ndoto zako. Ni vitu gani hasa vinavyo kupotezea muda wako kila siku?
Hivi ndivyo vitu vinavyo kupotezea muda sana katika maisha yako:-
1. Unapoteza muda wako kwa kujilinganisha na kila mtu.
Acha kuishi maisha ya kujilinganisha na watu wengine, jifunze kukimbia mbio zako mwenyewe. Unapojilinganisha na wengine pasipo kujua unajikuta unaanza kupoteza muda wako kwa kufikiria sana maisha yao ambayo pengine yapo juu zaidi yako.
Usikubali hata kidogo kupoteza muda wako wa thamani kwa kujilinganisha na wengine, elewa wewe ni wa pekee sana hapa Duniani na hakuna mtu mwenye ndoto na malengo kama yako. Jifunze kufata ndoto zako na  kisha songa mbele.
 
2. Unapoteza muda wako kwa kuhofia watu wanasema nini na kufikiri nini juu yako.
Umekuwa ukiishi maisha ya kujali sana watu wengine wanawaza na kusema nini juu ya maisha yako. Haya ni maisha ambayo yamekuwa yakikufanya upoteze muda mwingi kufikiria watu wengine ambao hawakuhusu, badala ya kukaa chini na kutengeneza mipango ya maisha yako.
Kama unaendelea kuishi maisha ya kuhofia watu utazidi kupoteza muda wako kila mara katika maisha. Jifunze kuishi maisha ya kuokoa muda na usiupoteze kwa namna yoyote ile.
3. Unapoteza muda wako kwa kutaka kila kitu ambacho huna.
Katika maisha hauwezi kupata kila kitu unachokitaka. Kama unaishi maisha haya ya kutaka kila kitu unachokiona basi utakuwa unapoteza muda wako sana. Hii ni kwa sababu utakuwa unatumia nguvu na akili nyingi kuhakikisha ni lazima upate hicho unachokitaka hata kama sio cha msingi sana katika kukamilisha ndoto zako.
4. Unapoteza muda wako kwa kujihofia wewe mwenyewe.
Unao uwezo mkubwa sana wakubadili maisha yako jinsi unavyotaka yawe kuliko hata unavyofikiri. Acha kupoteza muda wako kufikiri huwezi kufanya kitu katika maisha yako.
Unao uwezo mkubwa sana wa kufanya lolote unalotaka kwani wewe ni wa pekee, kitu cha msingi jipe moyo na amini unaweza na utaweza. Hakuna mtu atakayekupa taarifa ya kuweza zaidi yako wewe mwenyewe kujiambia unaweza kufanya mambo makubwa.
5. Unapoteza muda wako kuhofia makosa uliyoyafanya.
Kama umefanya makosa Fulani katika maisha yako ni sawa, lakini yasikupotezee muda kwa kuyafikiria sana makosa hayo. Kumbuka kila mtu anakosea na sio wewe peke yako uliyekosea, kitu cha msingi jifunze kutokana na hayo makosa yako. Usikate tamaa, jipe moyo unaweza na acha kufikiria makosa ambayo yametendeka hiyo haitakusaidia sana.
6. Unapoteza muda wako kwa kufikiria upo muda sahihi wa kufanyia kazi ndoto zako.
Kama wewe ni mtu wa kuairisha mambo na unasubiri muda mwafaka wa kufanyia kazi ndoto zako, Nakupa uhakika usipokuwa makini ndoto zako huwezi kuzifikia. Kila kitu hakiwezi kuwa tayari kama unavyofikiri, jifunze kutekeleza na kutimiza ndoto zako hata kwenye mazingira hayo hayo unayoyaona magumu na haiwezekani kutekeleza ndoto zako.
Utakuwa unapoteza muda sana kama utakuwa kila mara unasubiri muda mwafaka wa kufanya kile unachotaka kufanya. Wapo watu ambao wenye  tabia hii ya kupoteza muda na kuendelea kusubiri tena na kusubiri. Fanya kitu katika maisha yako acha kupoteza muda.
Hivyo ndivyo vitu vinavyokupotezea muda sana katika maisha yako, chukua hatua zaidi ya kuishi maisha mapya na kusonga mbele, acha kupoteza muda.
Nakutakia ushindi katika safari yako ya mafanikio na hakikisha unaendelea kutembelea  mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa kujifunza mengi zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA.
IMANI NGWANGWALU-  0767048035/ingwangwalu@gmail.com