FEDHA: Huu Ndiyo Ukweli Kuhusu Pesa Unaotakiwa Kuujua Mapema, Ili Uwe Tajiri.

Ni ukweli usiopingika kuwa pesa ni moja ya kitu kinachompa changamoto binadamu  katika maisha yake kila siku. Kama tulivyosema katika makala uliyopita, pesa imekuwa ni sehemu ya maisha yetu na imekuwa ikizidi kupewa kipaumbele siku hadi siku kutokana na umuhimu wake kwa kila mtu.
 

Pamoja na umuhimu huo wa pesa kutafutwa usiku na mchana, wengi wetu tumekuwa tukiitafuta pasipo kujua kanuni fulani au ukweli kuhusu pesa ambao tunatakiwa kuujua mapema ili tuwe matajiri. Kwa kadri utakavyozidi kuujua huo ukweli juu ya pesa na kuufanyia kazi utajikuta ndivyo pesa inazidi kukaa mikononi mwako na kujenga uwezo wa kuipata zaidi na zaidi.
Wengi waliofanikiwa kifedha wanaujua ukweli huo na ndiyo unawasidia kuvuta pesa zaidi katika maisha yao. Kwa upande mwingine, wanaoshindwa kumudu kuutumia na kuujua ukweli huu kuhusu pesa hujikuta maisha yao ni ya kukosa pesa mara kwa mara. Pengine, unaweza ukawa umeshaanza kujiuliza, ukweli upi ambao huujui kuhusu pesa? Kwa haraka naomba nikutajie ukweli unaopaswa kuujua kuhusu pesa.
Huu ndiyo ukweli unaotakiwa kuujua mapema kuhusu pesa ili uwe tajiri:-

1. Pesa yoyote unayoipata ni lazima ujilipe kwanza wewe mwenyewe.

Huu ni ukweli muhimu sana kuhusu pesa unaotakiwa kuujua na kuutumia katika maisha yako. Kila pesa unayoipata hakikisha unajilipa wewe kwanza hata kama ni kidogo vipi. Ukishajilipa mwenyewe pesa hiyo itakusaidia  itakapokuwa nyingi utaweza kumudu kuwekeza katika miradi yako mbalimbali kwa hapo baadae.

Jenga tabia hii ya kujilipa wewe kwanza , kumbuka unawalipa watu wote kasoro mtu mmoja wa muhimu ambaye ni wewe. Jiulize mwenyewe kwanini ushindwe kujilipa? Acha visingizio ‘oooh’ kipato changu ni kidogo, chukua hatua nakupa uhakika inawezekana. Ukiweza kumudu hili na kuweza kujilipa kwanza, baada ya muda ya muda utakuwa mbali sana katika maisha yako kimafanikio.
 

2. Kila pesa uliyonayo ina thamani kubwa sana.

Acha kudharau au kujiona kuwa pesa uliyonayo ni ndogo na ukaamua kuitumia vibaya, kwa kuamini ni kidogo sana haitaweza kukusaidia kitu. Pesa hiyo unayoiona ni kidogo ukiitunza kwa muda mrefu itakuwa nyingi mwisho itakusaidia kufanya mambo makubwa ikiwemo kufungua miradi.

Tunza pesa zako, na jitengenezee bajeti itakayokuongoza kwenye matumizi yako ya kila siku. Acha tabia ya kutumia pesa hovyo eti kisa kwa sababu zipo mfukoni. Jijengee uwezo wa kutunza pesa zako hata kama ni kidogo zitakusaidia. Heshimu pesa yako,nayo itakuheshimu na kuwa nyingi hiyo ndiyo nidhamu ya pesa unayotakiwa kuwa nayo.
3. Pesa itakuja kwako kama unafanya vitu vinavyovuta pesa na si vinginevyo.
Huu pia ni ukweli muhimu unaotakiwa kuujua unaohusiana na mambo ya pesa. Ni ukweli usiofichika yapo mambo katika maisha ukiyafanya yatavuta pesa kwako, na yapo mambo pia ukiyafanya yatafukuza mafanikio ikiwemo na wewe kujikuta kukosa pesa katika maisha yako.  
Jifunze kufanya vitu leo ambavyo vitakufanya upate pesa zaidi kesho. Kama huna pesa za kutosha sasa, acha kupiga kelele chukua hatua muhimu ya kufanya vitu vitakavyosababisha utengeneze pesa baadae. Kumbuka hutaweza kupata pesa kama hutafanya mambo yanayovuta pesa kwako. Uwezo wa kuwa na pesa zaidi unao ikiwa utachukua hatua, huu ndiyo ukweli.
4. Pesa ina kanuni zake maalum.
Kama vile ilivyo Kanuni ya kupata kile unachokihitaji katika maisha yako,pia pesa hii tunayoitafuta kila siku inakuwa ipo kwenye kanuni zake ndogo ndogo. Inapotokea kuvunjwa  kwa kanuni hizi kuharibiwa au kukosa pesa kwa mtu husika hutokea na hujikuta kuishi maisha ya utupu yasiyo na pesa siku zote.
Moja ya kanuni muhimu katika pesa ambazo ukizitumia zitakusaidia kusonga mbele ni kuweka akiba, kuweka kumbukumbu na kuwekeza. Unapoweka kumbukumbu juu ya pesa zako inakuwa ni rahisi kwako kujua pesa unayoipata inakwenda wapi na inafanya nini. Hii ni kanuni muhimu sana kwako ili kujenga utajiri.( Soma  pia Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutengeneza Pesa Zako Na Kuwa Tajiri )
5. Ni muhimu kubadili imani uliyonayo juu ya pesa ili utengeneze pesa zaidi.
Kama imani yako unaamini utapata pesa, nakuhakikishia hilo litawezekana kama utachukua hatua. Kama unaamini wewe ni mtu wa ‘kupigika’ siku zote katika maisha yako, hicho kweli ndicho utakachopata.
Unapozidi kuamini wewe huna pesa, maskini, kitakachokutokea ni kwamba utashindwa kuchukua hatua muhimu kwa vitendo zitakazo badili maisha yako. Jifunze kubadili imani yako juu ya pesa ili ujenge utajiri unaotaka, kwani Hii ndiyo imani unayotakiwa kuwa nayo juu ya pesa ili ufanikiwe zaidi.
Ukiwa na maarifa sahihi juu ya pesa maisha yako yatabadilika kwa kiasi kikubwa sana. Huo ndio ukweli kuhusu pesa unaotakiwa kuujua ili uwe huru kifedha na hatimaye kuwa tajiri. Ili kupata maarifa haya ya pesa na mengineyo zaidi, endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kwa kuhamasika zaidi.
Nakutakia ushindi katika safari yako ya uhuru wa kifedha.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA UFANIKIWE.
IMANI NGWANGWALU- 0767048035/ingwangwalu@gmail.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: