Acha Kuamini Sana Juu Ya Kitu Hiki Katika Maisha Yako, Ili Utengeneze Utajiri Mkubwa Ulionao.

Nakumbuka lilikuwa ni tukio lilitokea mwaka 2007 wakati nipo kidato cha sita kule Dodoma, ambapo jamaa yangu alipata tatizo la duka lake kuungua moto. Pamoja na duka hilo kuungua moto, bado alikuwa na akiba ya pesa kiasi benki ambayo ingemwezesha hata kufungua biashara nyingine mpya na kusonga mbele. Kwa mshangao wetu wengi, huyu jamaa aliamua kujiuwa, siku mbili baada ya tukio hilo.
Mke wake ambaye alichukua fedha zile aliamua kuendelea na biashara ya duka. Alitafuta eneo la biashara na kuanzisha duka jipya kwa mtaji ule mdogo aliokuwa nao. Hivi leo tunapozungumza kutokana na kumudu na kuamini kuwa anaweza kufanya biashara upya mama huyu ana biashara kubwa ya kutosha, zaidi ya ile ya kwanza ambayo iliungua moto.
Nakumbuka pia kuhusu ndugu yangu mmoja ambaye aliwahi kushinda hizi bahati nasibu zinazochezeshwa nchini. Alipata shilingi laki tano. Yule jamaa alishangilia sana na kufanya ‘pati’ ndogo katika kujipongeza. Kwa fedha hizo alianzisha biashara ya mazao. Hivi sasa hali yake imebadilika kiuchumi na amefika mbali kidogo.
Nimetoa mifano ya watu hao wawili ambao ninawafahamu au wananihusu kwa karibu, ili uweze kunielewa vizuri kwa kile ninachotaka kukisema. Hata hivyo kama haitoshi naweza kukuongezea tena mfano mwingine. Mimi nilipofanya mtihani wa darasa la saba mwaka 1999 sikuchaguliwa. Pamoja nami alikuwepo mtoto wa shangazi yangu ambaye tulikuwa tukiishi wote pale nyumbani. 
Huyu naye alianguka mtihani. Mimi nilichukulia kuanguka kule kama kitu cha kawaida. Nakumbuka, bila kufundishwa na mtu, nilikuwa najisemea ‘hivi nilivyo mdogo, wangeenda kunitesa bure sekondari’. Kutokana na kujiambia hivyo, nilihisi kuanguka kule lilikuwa ni jambo lazima litokee kwangu ili kuniokoa.
Yule binamu yangu kwa upande wake, alichukulia tukio lile kama jambo baya sana na alinyon’gonyea sana hadi akaanza kuugua. Mimi nilimsumbua sana baba yangu hadi akanitafutia shule ya kudurusu ambapo nilifaulu mwaka uliofuatia kuendelea na masomo ya sekondari.
Ni kweli, badala ya kusoma, alianza kuvuta bangi na baadae kunywa pombe. Hadi wakati huu ninapoandika makala haya, kutokana na huyu binadamu yangu kuamini sana ana mkosi, bahati mbaya katika maisha kwa sehemu kubwa maisha yake ameyaharibu kutokana na fikra hizo alizokuwa nazo ( Soma pia Hizi Ndizo Fikra Zinazokuzuia Kufikia Viwango Bora Vya Mafanikio )
index
Unaweza ukajiuliza ni wakati gani tuna bahati au tuna bahati mbaya? Bila shaka jibu liko wazi. Tunasema tuna bahati au bahati mbaya kutegemea sisi wenyewe tunayaamulia vipi yale yanayotutokea katika maisha yetu. Tunaitazama na kuipa jina gani hali, ndicho kinachofanya tuamue kama tuna bahati mbaya au nzuri. Je, unakubaliana nami?
Inakubidi ukubaliane nami kwa sababu, hakuna mahali unapokwenda kupata ukweli mwingine zaidi ya huu, katika jambo hili. Hebu fikiria kuhusu yule jamaa ambaye duka lake liliungua. Yeye bila shaka alijua ana bahati mbaya bila kujali kama ana akiba ya pesa benki, ambazo mkewe alizitumia kusimama na kukua kwa kiwango kikubwa zaidi.
Kuna yule ndugu yangu ambaye yeye alifanya sherehe kujipongeza kwa kupata kiasi cha pesa shilingi laki tano! kutokana na bahati nasibu aliyocheza. Kwake alijihesabu kwamba ana bahati sana katika maisha yake. Hii yote inaonyesha jinsi ambavyo wengi wetu tunavyoyachukulia matukio, kama ni kwa bahati au mkosi.
Kusema tuna bahati mbaya na kuamua  kukata tamaa hakutokei kwenye yale yanayotokea, bali zaidi kwenye mitazamo yetu. Usipokuwa makini na mitazamo hii inaweza ikakutesa siku hadi siku na kukufanya kuwa kama mfungwa vile ( Soma Hili Ndilo Gereza Kuu La Maisha Yako ).
Kama tunataka kuiona bahati nzuri inabidi tujue na kukubali kwamba, kila linalotokea  lina maana ambayo sisi hatuwezi kuijua kwa urahisi, lakini ambayo, ni lazima itokee kama ilivyotokea. Mara nyingi tunajishinda wenyewe kabla hatujashindwa na mtu. Kwa kusema tuna bahati mbaya, tunajifungia nia ya kumudu au kushinda.
Hebu fikiria mtu anasema hawezi kufanya biashara kwa sababu hii na hii, je unafikiria nini kitatokea? Ni yeye kushindwa katika maisha, nakujikuta kila mara analaumu ana bahati mbaya. Hivyo ndivyo ilivyo, siku zote tunakuwa ni watu wa kujifungia njia za mafanikio kabla hatujafungiwa.
Unataka kufanikiwa sasa, acha kuamini sana juu ya kitu hiki katika maisha yako, ili utengeneze utajiri mkubwa ulionao. Kumbuka bahati mbaya au nzuri huishi nyumba moja. Ni suala la kuamua unataka kumchukua au kutoka na yupi. Na kama utaendelea kuamini hivi juu ya bahati katika maisha yako, sahau kuhusu mafanikio.
Ili kuondokana na mawazo hayo ya kuamini bahati, endelea kujifunza kila siku. Kwa kadiri utakavyojua mambo mengi, ndivyo utakavyokuwa na ‘bahati’ zaidi. Hii ina maana kwamba, ukiwa na hekima, hutayaacha mambo yako kwa kitu kinachoitwa bahati, bali utayaacha kwako mwenyewe kwa kuamini kwamba, wewe ndiye unayewajibika na maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio.
TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.
IMANI NGWANGWALU – 0767048035/ingwangwalu@gmail.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: