Kuna wakati katika maisha yetu tunayoishi, kutokana na jamii tunazoishi huwa tunajikuta ni watu kurushiwa maneno na tuhuma mbaya ambayo pengine hatujazifanya. Hali hii huwa inatokea katika maisha ya kila mmoja wetu kwa namna moja au nyingine, ingawa ni kwa vipindi tofauti.
 

Unapojikuta unarushiwa maneno au habari zako zimeenea ghafla mtaani kwa kile kitu ambacho hujakifanya wengi wetu hali hii inapotokea  huwa tunajikuta ni watu wa kupaniki na kuja juu na kushindwa kujua nini cha kufanya. Unaweza ukasikia umefanya hili, umefanya lile kitu ambacho si kweli. 
Hiki ni kitu ambacho kipo katika maisha yetu, huwezi kukikwepa katika jamii kwani maneno yapo na yataendelea kuwepo  siku hadi siku. Unapokutana na hali hii unaweza ukajikuta una mawazo mengi, ambayo yanakuumiza akili na kujihisi mnyonge kwanini tukio hilo litokee kwako. 
Kitu usichokijua pengine tukio hili la habari zako kuenezwa hovyo si lako peke yako. Wapo watu ambao wamekutana nalo kama wewe, lakini walimudu kupita katika hayo mapito na hatimaye kuwa washindi. Huna haja ya kusononeka sana wala kuwa na mawazo mengi.( Soma pia Wajue Watu Hawa Na Waepuke Katika Maisha Yako )
Unachotakiwa kufanya ni kuchukua hatua juu ya hiki ninachokwenda kukueleza ili kuwa huru na kuachana na hayo mawazo yanayokusumbua. Haijalishi kimesemwa nini hata kama umesikia au umeona habari zako zimetapakaa kwenye magazeti kwamba eti wewe umebaka, hilo litakushitua lakini ipo njia ya kukabiliana na tatizo lako. 
Kama huelewi vizuri kwa hiki ninachokisema, unaweza ukaliona hili kwenye maisha kama ya wasanii au watu maarufu. Mara nyingi huwa wanakutana na matukio kama haya ambayo wakati mwingine huwa  si ya kweli, lakini hukabiliana nayo na kuvuka.
Hiki ndicho kitu nataka kitokee kwako uvuke pia. Achana na fikra hizo zinazokuumiza juu ya ‘skendo’ uliyonayo. Jifunze kuchukua hatua zitakazo kuweka huru zaidi. Unaweza ukawa unajiuliza sana, unatakiwa ufanye nini ili usiweze kuumia huku ukizingatia tuhuma zenyewe sio za kweli ni uzushi tu.
Haya ndiyo mambo muhimu unayotakiwa kufanya ili kukabiliana na maneno mabaya unayoambiwa katika jamii:-
1. Acha kuwa na hasira.
Katika kipindi ambacho tuhuma nyingi zinakuja juu yako, unasemwa kwa kila hali ambayo kwako binafsi siyo kweli, hapa unatakiwa kujifunza  kutokuwa na hasira. Unapotulia na kuwa mtulivu hiyo itawaonyesha wale wote wanaokutuhumu watulie kwanza na kujiuliza vitu vingi.
Lakini kama utakuwa unasemwa na wewe unakuja juu, hili litaonyesha kuwa kile kinachosemwa ni cha kweli umefanya. Ukipunguza hasira hii itakuwa ni njia mojawapo bora ya kukabiliana na maneno mabaya unayoambiwa na watu wanaokuzunguka katika maisha yako.
 
 
2. Jifunze kupuuza.
Kama utakuwa unatega sikio na kusikiliza kila unachoambiwa na watu wengine juu yako, basi utapata shida sana katika maisha yako. Ishi maisha ya kuwa na mtazamo chanya juu ya maisha yako. Kama umesikia maneno au umesemwa juu ya kitu kibaya ambacho wewe unajua kweli hukikifanya, acha waseme jinsi wanavyoweza.
Acha kukaa chini kupoteza muda wako kufikiria sasa itakuwaje, mbona iko hivi wala sio kweli. Hiyo haikuhusu fata mambo yako. Najua pengine unaweza ukawa una hofu, jina lako litachafuliwa kweli, lakini huna namna ya kufanya zaidi ya kutumia njia hii ya kupuuza ili  kuweza kuishi kwa amani. 
3. Jaribu kushirikiana nao.
Kama umeshindwa kupunguza hasira, umeshindwa kupuuza, ili uweze kupunguza mawazo ya kile unachosemwa huna budi kutumia njia hii muhimu ya  kushirikiana na wale wanaokusema ili kupata suluhisho sahihi. Utashirikiana nao tu kwa njia ya maongezi ya ana kwa ana.
Unaweza ukawatafuta na kuwaweka chini na mkayajenga vizuri na kuelewa chanzo hasa nini kinachopolekea wao wakupe tuhuma ambazo hazikuhusu. Kwa njia hii itakusaidia kupunguza mawazo mengi ambayo unayo kutokana na kusemwa kwako.
4. Thibitisha kuwa kile kinachosemwa sio kweli.
Kama unaoushahidi wa kuweza kuonyesha juu ya kile kinachosemwa ni vizuri ukautoa na kuweka wazi. Kwa mfano kama unatuhumiwa hapo mtaani kwako labda umetembea na mume wa mtu na wale wanao kutuhumu unawajua, ni vizuri ukamtafuta yule bwana na kumweleza hali halisi, kisha ukampeleka kwa hao wanao dai tuhuma hizo ambazo si za kweli na zinakera kwako.
Hapo utakuwa umetengeneza dawa ya maneno unayorushiwa kila kona. Na hii itasaidia kuweka wazi ukweli ambao pengine ulikuwa haujulikani upande wa pili juu yako. Ukiweza kuthibitisha kwa ushahidi kuwa kile kinachosemwa si kweli itakusaidia sana kukabiliana na tatizo lako.
5. Fanya vitu vingine tofauti vitakavyokupotezea mawazo uliyonayo.
Hapa ili kupunguza mawazo ya kile kinachosemwa unaweza ukafanya vitu tofauti kidogo, ili kujiweka ‘bize‘ zaidi na kukusahaulisha bila ya wewe kujijua. Unaweza ukatafuta kitabu kizuri na kujisomea au unaweza ukatembelea mitandao mbalimbali inayohamasisha au unaweza ukatafuta muda wa kubadilisha mawazo na marafiki ambao unaona wana mawazo chanya katika maisha.
Hayo ndiyo mambo muhimu unayotakiwa kufanya ili kukabiliana na kupunguza mawazo maneno mabaya unayoambiwa katika jamii unayoishi.
Nakutakia maisha mema yenye amani, endelea kutembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa kujifunza na kuhamasika zaidi.
TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE. 
 
IMANI NGWANGWALU – 0713 048035/ingwangwalu@gmail.com