Habari za leo ndugu msomaji wa AMKA MTANZANIA, karibu tena kwenye kipengele cha ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa.

Wiki hii tutajadili changamoto ya kuendelea na masomo au kufanya biashara. Kuna wakati ambapo mtu unajikuta njia panda kati ya kuendelea na masomo au kufanya biashara. Huu ni wakati mgumu sana hasa pale kunapokuwa na shinikizo kutoka kwa watu wako wa karibu. Kabla hatujajadili ni kitu gani unaweza kufanya kwenye hali kama hii tuone maoni ya msomaji mwenzetu.

Mimi Nime Maliza Form4 Mwaka Jana Sikufaki Kuendele Na Masomo. Kwa Sasa Nina Fanya Biashara ya Matunda Uku Shinyanga. Changamoto Nayoipata Ni Mm Nataka Kuwa Mfanya Biashara Wa Matunda Lakini Dada Ya Ngungu Ananishauri Nijiunge Na VETA. na mimi sijapata kitu chochote nitakacho kwenda kukisomea. je ni fanye nini?

Tumeona ugumu ambao anao msomaji mwenzetu kati ya kuendelea na masomo au kufanya biashara. Je ni kipi sahihi kufanya?

kipi

Masomo ni muhimu, tena masomo ya ufundi ni muhimu sana kwa sababu hapo ndio unapojifunza kitu halisi ambacho unakwenda kukitumia kwenye maisha halisi ya baada ya masomo.

Kuanza biashara mapema nayo ni muhimu sana, kwa sababu jinsi unavyoingia mapema kwenye biashara, ndivyo unavyoshindwa mapema na kujifunza mapema pia. Hii inakuweka mbele kwenye nafasi ya mafanikio ukilinganisha na ambao wanaendelea na masomo na kuja kuingia kwenye biashara baadae.

Sasa kama vyote ni muhimu ni kipi afanye kwa sasa?

Ushauri wangu kwa msomaji mwenzetu huyu ni asifanye maamuzi ya haraka. Kaa chini na orodhesha malengo na mipango yako yote kwenye maisha yako. Angalia miaka kumi ijayo unajiona ukiwa wapi? Vipi miaka ishirini ijayo? Baada ya kupata picha kubwa ya maisha yako sasa unaweza kuangalia je kuendelea na biashara kutakufikisha kwenye picha hiyo? Au kujifunza taaluma ya ziada ndio kutakusaidia zaidi?

Kama utachagua kuendelea na biashara hakikisha biashara hiyo ni kitu ambacho unapendelea kufanya kutoka moyoni. Isije ikawa unafurahia biashara hiyo kwa sababu inakupa faida, kwa sababu ikifika wakati ikawa haileti faida utatetereka sana na kujutia nafasi ya kuongeza elimu uliyoiacha.

Ikiwa utachagua kuendelea na masomo utapata ujuzi tofauti na bado unaweza kuutumia kibiashara baadae, hapo ni kama utapata kitu ambacho unapenda kukisomea na kukifanya.

Haya ni maamuzi muhimu sana unayotakiwa kufanya na kisha kuishi nayo. Yaani ukishafanya maamuzi haya hutakiwi kujutia tena baadae kwamba kama ningejua ningefanya hivi kipindi kile.

Mwisho kabisa, nafikiri mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana bado umri wake unaweza kuwa mdogo, chini ya miaka 20. Katika umri huu mdogo ni vigumu sana kuwa umepata kitu ambacho unakipenda sana kukifanya kwa maisha yako yote. Hivyo unaweza kutumia mwaka mmoja au miwili kujaribu vitu tofauti tofauti kuona ni kipi unakipendelea kufanya.

Kwa kuwa elimu ya VETA ni mwaka au miaka miwili unaweza kuingia kusoma kama sehemu ya kujifunza mambo tofauti tofauti ili uweze kujua ni kipi unapendelea kufanya kwenye maisha yako. Hivyo unaweza kuendelea na elimu VETA na ukapata ujuzi ambao baadae unaweza kuutumia kibiashara.

Hayo ndio mambo machache ninayoweza kukushauri katika changamoto hiyo. Kaa chini, fanya tena upembuzi kwa kuzingatia hayo tuliyojadili hapa kisha fanya maamuzi ambayo utayasimamia kwa maisha yako yote. Baada ya kufanya maamuzi hayo usijutie tena baadae, bali fanyia kazi kwa juhudi na maarifa kile ambacho umeamua kukifanya.

Nakutakia kila la kheri kwa kile ambacho utaamua kufanya.

TUPO PAMOJA.

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu.(CHANGAMOTO NYINGI ZINAZOTOLEWA SASA TULISHAZIJIBU HUKO MWANZONI, VITU KAMA KUPATA MTAJI, MATUMIZI YA FEDHA NA BIASHARA GANI MTU UFANYE TULISHAZIPATIA MAJIBU. KABLA YA KUWEKA CHANGAMOTO YAKO TAFADHALI PITIA MAKALA ZA NYUMA ZA KIPENGELE HIKI CHA USHAURI KWA KUBONYEZA HAPA NA KAMA CHANGAMOTO YAKO HAIJAJIBIWA NDIO UIWEKE.) Changamoto yako inaweza kuwa moja makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa kwa email ushauri@kisimachamaarifa.co.tz  au simu 0717396253

kitabu-kava-tangazo432