Sijawahi kuona au kusikia kwamba, wasiwasi umeweza kutatua tatizo la mtu. Siku zote nimeshuhudia na kusikia kuhusu maumivu yatokanayo na wasiwasi ambayo yamekuwa yakiwapata watu. Unazijua hasara za kuwa na wasiwasi? Kama nilivyosema, ni kwamba wasiwasi haukusaidii chochote. Na je, unajua kwamba wasiwasi hautatui tatizo. Lakini pia je, unajua wasiwasi unaweza kuharibu zaidi mambo yako kabisa? 
 

Wasiwasi ni njia ya kutuma ujumbe wa kukata tamaa kwenye akili yako na unachoweza kufanya ni kukufikisha kwenye hali za kukatisha tamaa. Wakati unapoanza kuwa na wasiwasi, unajenga mtiririko wa mawazo ya kukatisha tamaa. Mawazo haya huchukuliwa na mawazo yako ya kina, ambayo hatimaye huubadili ukweli kwa kuegemea kwenye imani zako yaani wasiwasi ulionao juu ya jambo hasa unaloliwaza.
Hivyo, ikiwa una wasiwasi kwamba, huenda ukashindwa kupata fedha za kutosha kulipa madeni yako, mawazo yako ya kina ambayo hufanya kazi kwa maelekezo yako, yatakutayarishia mazingira yatakayofanya usipate fedha za kulipa madeni yako.( Soma Pia Hivi Ndivyo Unavyoweza Kumudu Kuondoa Hofu Zako Za Kesho, Zinazokusumbua  Na Kukutesa )
Ikiwa una wasiwasi kwamba mke au mume wako ana mpango wa kuachana nawe, mawazo hako hayo yatajenga hali itakayomlazimisha mpenzi wako huyo kuachana nawe. Kama una wasiwasi kwamba, hutopata kazi, akili yako itakutengenezea hali ili usiweze kupata. Hii ni mifano michache tu ya namna mawazo yako ya kina yanavyoheshimu wasiwasi na kile unachokiwaza. Kumbuka mawazo haya yanafanya kazi kwa kanuni. ( Soma Kanuni Ya Kupata Kile Unachokihitaji Katika Maisha  )

Msingi mkuu wa kuachana na tabia ya kuwa na wasiwasi ni kwanza, kufahamu kuwa wasiwasi ni mtiririko wa mawazo ya kukata tamaa, mawazo hasi. Sasa unaweza kuamua kuendelea kuwa na mawazo haya ama kuyabadili. Kumbuka wewe ndiye mtawala wa akili yako, hakuna mwingine. Ni muhimu kujua nini hasa kinachokutia wasiwasi, ukishajua anza kuachana na mawazo hayo, wasiwasi utaanza kupotea taratibu.
Hatua ya pili ni kufikiri kuhusu kile unachotaka. Kwa mfano, una wasiwasi kwamba huenda hutopata kazi. Unachohitaji hasa hapa ni kazi. Hivyo anza kuelekeza mawazo yako kwenye kupata kazi, siyo kukosa kazi. Fikiria kuhusu aina ya kazi unayoihitaji. Fikiria kuhusu nini unaweza kufanya katika kupata kazi. Anza kufanya mambo kama mtu aliyekwisha kupata kazi.
Hii haina maana kwamba, uanze kutumia fedha ulizoweka kama mtu aliye na kazi ya kipato unachofikiria. Badala yake, kila unapotembea kuwa na hisia, kuwa na mawazo akilini kwamba tayari una kazi. Iambie nafsi yako kwamba, tayari unayo kazi. Kwa kufanya hivyo, utaanza kuhamisha nguvu zako kutoka kwenye nguvu za kukatisha tamaa, wasiwasi na kukuletea hali ya kuleta matumaini.
Kwa kufanya hivyo pia, unatuma ujumbe kwa nguvu zako za juu kwamba, unaamini utapata kazi na kwamba unaziamini sana kiasi kwamba hivi sasa umetoka na kuanza kufanya kila unachoweza ili kupata kazi. La mwisho lakini la msingi ni kuanza kuishi maisha ya furaha. Huenda isiwe rahisi sana kwako, kwani tayari umezoea kuwa na wasiwasi wakati wote. Lakini lazima uanze kusonga mbele.
Hii ina maana kuwa uanze kuelekeza akili yako si kwenye kile unachotaka tu, lakini pia anza kutazama vitu vizuri ulivyonavyo kwa maisha yako. Ni watu wachache sana wanaoweza kusema hawana hata kitu kimoja kizuri katika maisha yao. Lakini kitu kinachowafanya watu wajione wasio na bahati ni kwa vile wakati wote huwa wanatazama vitu wasivyoviona si vizuri kwa upande wao.
Hali hii huwafanya wajione hawana bahati na kuwaingiza kwenye lindi la mawazo wakati wote. Tazama mambo mazuri uliyonayo na kama una familia au una kazi ama vyote, hayo ni mambo mazuri. Kama una afya njema, hilo pia ni jambo zuri. Kama unao marafiki, na hilo nalo ni jambo zuri na unaweza kutazama vitu vingine vizuri ulivyonavyo na mara utakapozoea kufanya hivyo, bila kujua inavyotokea, utaacha kuwa na wasiwasi.
Baada ya kuchunguza vitu vizuri ulivyo navyo, anza maisha yako upya. Anza kufanya mambo yanayokufurahisha, fikiria kile unachovutika zaidi kufanya na uanze taratibu kujiingiza katika vitu vingine. Ikiwa unapenda kutazama movie, basi unaweza kutazama na rafiki zako. Ikiwa unapenda kucheza mchezo fulani, basi fanya hivyo, ili mradi unaanza kufanya mambo unayoyapenda.
Inaweza ikaonekana ni vigumu, lakini faida ya kufanya hivi ni kubwa sana. Hivyo ndivyo unavyoweza kuishinda hali ya kuwa na wasiwasi na kuishi maisha ya furaha na amani.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, karibu sana katika KISIMA CHA MAARIFAna endelea kutembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa kujifunza zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.
IMANI NGWANGWALU.
0767 04 80 35
0713 04 80 35/ingwangwalu@gmail.com