Habari za leo mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA  karibu tena kwenye kipengele chetu cha kujadili changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio. Leo katika kipengele hiki tutajadili jinsi ya kuishinda hofu ya kuana biashara.

Watu wengi wamekuwa na mawazo mazuri ya kuanzisha biashara ila inapofika kwenye kuanza utekeleaji wa mawazo yenyewe wanakutana na hofu ambayo inawazuia kuanza. Inawezekana hata wewe umeshindwa kuanzisha biashara yako au kuikuza zaidi kutokana na hofu. Sio lazima hofu hii iwe moja kwa moja, baadhi ya watu hutumia sababu nyingine kama ukosefu wa mtaji au kutokujua biashara nzuri kama kisingizio cha kuficha hofu yako.

Kabla hatujaangalia jinsi ya kuepuka hofu hii ya kuanza biashara, tuone maoni ya msomaji mwenzetu;

Changamoto kubwa inayonikabili ni uoga wa kujaribu kufanya jambo fulani hasa biashara nikihofu kuwa naweza pata hasara na pesa yangu ikawa imeishia katika hasara hiyo.
Unakuta nakuwa na wazo zuri la kuanzisha biashara lakini uoga ndo unaonimaliza nguvu.
Je utanisaidiaje kuepuka uoga ili nisonge mbele???
Kiufupi, mi ni mwajiriwa wa kampuni moja kubwa hapa nchini.

Kama tulivyoona changamoto ya msomaji mwenzetu, yeye anashindwa kuanza biashara kwa kuhofu kwamba anawea kupata hasara. Kupata hasara ni hofu ambayo inawazuia watu wengi sana kuingia kwenye biashara. Hata wale ambao tayari wako kwenye biashara hofu hii inawazuia kutanuka na kukua zaidi.

Ni kweli kwamba kuanzisha biashara yoyote ni kitu cha hatari sana, hii ni kwa sababu kuna vitu vingi sana ambavyo huna uhakika. Na biashara yoyote mpya ina hatari kubwa ya kushindwa kuliko ilivyo na uwezekano wa kufanikiwa. Lakini hofu hii haipaswi kutufanya tusianzishe au kukuza biashara zetu.

Njia za kuepuka hofu ya kupata hasara kwenye biashara.

Zifuatazo ni njia ambazo unaweza kuzitumia kuishinda hofu ya kupata hasara unapoanzisha biashara.

1. Angalia wafanyabiashara waliofanikiwa na jifunze kutoka kwao.

Wafanyabiashara waliofanikiwa wana uzoefu mkubwa sana kwenye biashara wanazofanya. Watu hawa wameshafanya makosa mengi sana na hivyo wanaweza kukusaidia usirudie makosa ambayo yaliwapatia wafanyabiashara hao hasara. Unaweza kuwatafuta na kujifunza kutoka kwao na kama huwezi kuwapata watu wa aina hii soma vitabu vinavyoelezea mafanikio ya wafanyabiashara wakubwa. Hii itakupa mbinu walizotumia wao na pia itakupa moyo pale utapoona kwamba pamoja na mafanikio makubwa waliyonayo waliwahi kupitia kushindwa.

2. Fanyia utafiti wazo lako la biashara.

Kitu kingine kikubwa kinachokufanya uwe na hofu kubwa ya kuanza biashara ni kutokuwa na uhakika na wazo lako la biashara. Hivyo chukua muda wako na fanya utafiti wa kutosha kwenye wazo lako la biashara. Angalia utofauti wa wazo lako na mawazo ya wengine na ambalia ubunifu ambao unaweza kuuweka na kuifanya biashara yako kuwa ya kipekee. Pia angalia changamoto zinazoweza kulikumba wazo hilo la biashara na kujipanga jinsi ya kujikwamua ikitokea changamoto hizo zimetokea.

3. Anza kidogo.

Pamoja na kujifunza kwa waliofanikiwa na hata kufanya utafiti wa wazo lako la biashara, bado hofu ya kushindwa ni kubwa. Hivyo ili kuishinda hofu hii anza biashara yako kwa hatua ndogo ndogo. Hata kama una wazo kubwa la biashara, anza kidogo, angalia hatua ndogo unazoweza kuanzia kisha anza hapo. Tumia sehemu ndogo ya mtaji kuingia kwenye biashara hiyo na jifunze kwa kila hatua unayopiga. Kwa njia hii utajua ni sehemu gani inaweza kukuletea faida kubwa na pia ni sehemu gani yenye changamoto nyingi na hivyo kuhitaji umakini zaidi. Unaposhindwa kidogo inakupa wakati mzuri wa kufanya marekebisho kuliko ambavyo ungeweka mtaji wote na ukaishia kuondoka kwenye biashara.

4. Zungukwa na watu ambao wana ujasiri kwenye biashara.

Kama bado wewe ni muajiriwa na una mpango wa kuanzisha biashara, ukijadili mpango wako huu na wafanyakazi wenzako watakuogopesha sana. Watakupa maneno mengi ya kukutisha, watakwambia huwezi, watakupa mifano ya waliojaribu na wakashindwa na hivyo utakubaliana nao na kuachana na mawazo yako ya kuanzisha biashara. Kitu muhimu wewe kufanya ni kutafuta njia ya kuwa karibu na wafanyabiashara au watu ambao wana ujasiri wa kushinda hofu ya kupata hasara. Tafuta kikundi cha wafanyabiashara na kuwa nao, hawa watakupa moyo wa kuanza na pia watakushauri pale ambapo utakutana na changamoto.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA jiunge sasa kwa uanachama wa GOLD na utapata nafasi nzuri ya kukutana na watu ambao wameweza kushinda hofu kwa namna moja au nyingine.

5. Jua kwamba haupo mwenyewe na dawa ya hofu ni kuanza.

Njia nyingine unayoweza kutumia kushinda hofu yako ya kupata hasara ni kujua kwamba hauko mwenyewe. Kila mtu unayemuona ana hofu zake, kila mafanyabiashara unayemuona haijalishi ana mafanikio kiasi gani naye ana hofu zake. Kinachomtofautisha yeye na wewe ni ule ujasiri wa kuanza na kujifunza kadiri anavyopiga hatua. Hivyo kwa vyovyote vile anza, wanasema dawa ya hofu ni kufanya kile unachohofia kufanya na hofu hufa yenyewe. Kama tulivyosema hapo juu, anza kidogo, anza chochote kinachohusiana na biashara unayotaka kufanya, kidogo kidogo utaona unaanza kupata ujasiri na kuishinda hofu uliyokuwa nayo mwanzo.

Mwisho kabisa kumbuka kwamba hakuna kitu unachoweza kufanya kikakuondolea kabisa hatari ya kushindwa, hakuna. Maisha yenyewe ni hatari, sasa hivi umeajiriwa lakini unaweza kushangaa kesho ajira yako ikaisha, lakini hii haijakuzuia kuendelea na ajira. Unaweza ukapanda gari na mbele likapata ajali na hata ukafa, lakini hiyo haikuzuii kupanda gari. Hivyo hivyo unaweza kuanza biashara na ikapata hasara, lakini hii isikuzuie wewe kuanza biashara. Kila kitu kwenye maisha yetu kina hatari ya kutoweka bila ya sisi wenyewe kujua. Hivyo fanya kile ambacho unafikiria kufanya, huku ukijifunza na kurekebisha kadiri unavyokwenda.

Kauli mbiu yetu kwa mwaka huu 2015 ni kama NIKE wanavyosema, JUST DO IT, CHOCHOTE UNACHOTAKA KUFANYA WEWE ANZA KUFANYA, kama kuna kitakachotokea baadae utajifunza na kufanya marekebisho. Kukaa tu na kuhofu hakutakusaidia chochote.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara unayokwenda kuanza mwaka huu 2015.

TUPO PAMOJA.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.

Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

MUHIMU;

Email za mafunzo ya semina ya siku 21, zimeshaanza kutumwa. Kama ulijiunga na semina hii na hujapata email angalia kwenye email zako vizuri na ukikosa angalia kwenye spam folder au junk emails. Kama hakuna kabisa basi tuma ujumbe wako wa malipo na email kwenda namba 0717396253.

kitabu-kava-tangazo4322