Yale mambo ambayo unayoyaweza kuyaita bahati mbaya, kwa hakika ni uzoefu wa kujifunza na ni mawazo ama mwelekeo wa mtu, hakuna kitu kama hicho katika hali halisi. Baadhi ya watu hulaumu bahati mbaya na kujihukumu kwamba wana mikosi. Wanasahau kwamba mafanikio huwaendea wale wanaojipangia nidhamu na kufanya juhudi. Mambo huwa hayatokei tu, unayatengeneza wewe.

Watu walio na bahati na mafanikio ni wale waliofanya maamuzi ya kubadili maisha yao. Wanatumia uzoefu mbaya kama mafunzo na hukwepa kutafuta visingizio. Kuna wakati huwa ni vigumu kumshawishi mtu kwamba, binadamu anauwezo wa kuivuta bahati ikaja upande wake. Kwa wengi huwa ni kitu ambacho hakiwezekani hata kidogo ingawa kwa namna moja au nyingine huo uwezekano huwa upo.

Umeshawahi kujiuliza au kutamani na wewe uwe na bahati, kama wengine unavyowaona wanabahati? Na ulishafikiri kuwa je, hiyo bahati ipo? Inawezekana umeshawahi kujiuliza hivyo na pengine ukashindwa kupata majibu. Lakini, kiukweli hakuna kitu kinachoitwa bahati wala mkosi katika maisha yetu vyote ni uchaguzi wetu. Hata wewe unaweza ukawa na bahati na kufanikiwa sana, kama hao unaowaona wamefanikiwa. Ki vipi?

Hivi ndivyo unavyoweza kujiletea bahati katika maisha yako:-

1. Jitahidi kubadili mtazamo wako.

Ikiwa utaendelea kulalamika jinsi usivyo na bahati, utajinyima nafasi kubwa ya kufanikiwa. Unahitajika kubadili jinsi unavyoiona nafasi yako na kufuafatilia mambo. Ni lazima ujione wewe ni mtu wa hali ya juu na muhimu na tarajia mambo mazuri kutokea kwako, bila kujali nini kilitokea hapo nyuma au zamani. Fanya hivyo kwa kuelekeza mawazo yako katika vile vinavyokusaidia na ulivyowahi kufanikisha, hata kama ni kidogo sana. (Soma pia Unataka kuwa nabahati fanya hivi)
 

2. Fanya jitihada za kufanikiwa.

Jinsi utakavofanya kazi kwa muda mrefu na kwa bidii kuelekea kwenye njia sahihi, ndivyo nafasi yako ya kufanikiwa inavyokuwa kubwa ya kuwa na bahati. Wakati unapojitahidi kufanikiwa utajikuta katika furaha ya ubunifu na uzaaji matunda wa unayoyafanya. Unatakiwa kukusanya ujuzi mkubwa iwezekanavyo ili kujiongezea uwezo wako. Mawazo yako kuhusiana na ni muda gani na jitihada ulio tayari kutumia kwenye hili, vitaamua matokeo yako. Matokeo mazuri yatakuja wakati utakapojitolea, utakapobaki na matumaini na kufanya kila unachoweza.(unaweza ukasoma pia ni muda kiasi gani unahitaji ili kufikia mafanikio makubwa)

3. Tumia kanuni ya usababisho.

Mara nyingi watu wenye mawazo finyu huamini sana hawana bahati kumbe sio kweli. Watu wenye msimamo huamini katika sababu na matokeo. Kuna msemo usemao ‘njia bora ya kuelekea unapoweza kutabiri hatma yako ni kuitengeneza wewe mwenyewe’. Hivyo unaweza kutabiri kabisa jinsi matokeo ya jitihada zako kama zitafanikiwa. Hiyo ni kwa sababu kanuni ya usababisho inasema, vitu huwa havitokei tu kwa bahati mbaya. Iwe unajua au hujui, kila ulichokifanya ama kukifikiria kukifanya hapo mbeleni, ndicho kinachokupatia kile unachokumbana nacho leo. Kile unachofanya na kukifikiria leo hii ndicho kitakachoamua nini kikutokee hapo baadaye.

4. Tumia muda wako mwingi kufanya kile kitakachokufanikisha.

Karibu kila kitu kinahitaji muda kukijenga na kukikuza. Endelea kufanya jitihada hata kama huoni matokeo ya haraka kutokana na jitihada zako. Ikiwa utatumia muda mwingi kufanya kazi na kujifunza, ni lazima matokeo yake utayapata baadaye. Jikumbushe kwamba utapata faida ya baadaye, itakayokuwa sawa na kiwango cha jitihada na muda uliotumia. Kumbuka kabisa kwamba kinachoitwa bahati au mkosi huwezi kuviona, bali ni nguvu ambazo unaweza kuzitengeneza wewe kulingana na unachfikiri hasa kama ni mkosi au bahati.

Ikumbukwe pia nguvu hizi hutoka kwenye imani zetu, ambazo zipo mawazoni mwetu. Kwa hiyo, ili upate bahati, fikiri kwa njia ya kupata bahati, na ili upate mkosi fikiri kwa njia hiyo pia, kwani yote yako chini ya uwezo wako, ni suala la uchaguzi tu. ukiamini katika mkosi, utaona mikosi tu, ukiamini katika bahati, utaona bahati, bila kujali muda, mazingira, umri, dini wala elimu. Lakini, ingawa kwa kawaida, hutagundua kwa haraka kamba, mkosi au bahati unayoiona inatokana na kile kinachokwenda mawazono mwako. Utasingizia zaidi mazingira na watu wengine.

Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kila siku kupata maarifa bora zaidi.

Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO  kwa kujifunza na kuhamasika.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,