USHAURI; Unapochagua Mtu Wa Kufanya Nae Biashara Kuwa Makini Kuliko Unavyochagua Mke Au Mume.

Habari za leo msomaji wa AMKA MTANZANIA, karibu tena kwenye kipengele hiki cha ushauri wa changamoto zinatotuzuia kufikia mafanikio kwa kile ambacho tunafanya. Ni kweli kwamba njia ya kufikia mafanikio ina vikwazo vingi sana na usipokuwa umejiandaa vizuri ni rahisi sana kukata tamaa. Ndio maana kwenye kipengele hiki tunapeana ushauri kulingana na changamoto mbalimbali ambazo wasomaji mbalimbali wanazipitia.

Siku za hivi karibuni nimekuwa napokea sana ujumbe na simu za watu ambao wamefikia kukata tamaa hasa baada ya kufanya biashara na watu halafu watu hao wakawaingiza kwenye hasara kubwa. Sehemu kubwa ya changamoto hii inatokana na mtu kumwamini mwenzake ambaye ni ndugu au rafiki, wanafanya wote biashara halafu mtu yule anafanya uzembe na wanapata hasara au anatumia vibaya fedha na kusababisha hasara. Pia wakati mwingine mtu huyo anafiki hatua ya kumtapeli kabisa mwenzake.

Je nini cha kufanya ili kuepuka changamoto hii?

Kabla hatujaangalia ni kitu gani unaweza kufanya ili kuepuka changamoto hii kwanza tuangalie umuhimu wa kuwa na mshirika kwenye biashara. Ukweli ni kwamba biashara ni ngumu. Ni ngumu kuanza, ni ngumu kufanya na pia ni ngumu kupata mafanikio. Ndio maana kila siku biashara zinaanzishwa na baada ya muda mfupi zinakufa. Pia kuna watu ambao wanafanya biashara ile ile, kwa ukubwa ule ule kwa zaidi ya miaka kumi sasa.

Moja ya njia ambayo unaweza kutumia kupunguza ugumu huu wa biashara ni kuwa na mtu ambaye utashirikiana nae kwenye biashara. Mtu huyu anakuja kama mshirika na hivyo mnashirikiana kuanza au kukuz abiashara yenu. Kwenye kuanza mnaweza kuchangia mtaji, kitu ambacho ingekuwa changamoto kwa mtu mmoja, kuongeza mawazo na hata kuboresha zaidi mawazo maana vichwa viwili ni bora kuliko kichwa kimoja. Kwa vyovyote vile ushirikiano kwenye biashara ni wa muhimu sana.

Pamoja na umuhimu huu wa ushirikiano kwenye biashara na faida ambayo mshirika anaileta, mtu huyu pia analeta matatizo yake. Ndio kila mtu ana matatizo yake, hivyo atakuja akiwa kama msaada kwenye biashara , ila pia matatizo yake au mapungufu yake atakuja nayo pia. Na hapa ndio changamoto zote za biashara za kushirikiana zinapoanzia.

Nini cha kufanya?

Ili kuepuka changamoto hii inabidi uwe makini sana wakati unaamua ni mtu gani utafanya nae biashara. Ni lazima umjue kwa undani na uone kama anafaa kweli kwenda na wewe mpaka ale mtakapofikia mafanikio kwenye biashara hiyo. Naweza kusema inabidi uwe makini kuliko hata unavyochagua mume au mke. Hii ni kwa sababu mume au mke unaweza kumchagua kwa hisia za mapenzi, amekupenda umempenda mnaoana, hata pale inapotokea changamoto mapenzi yanaweza kuwafanya muishinde changamoto ile. Ila kwenye biashara hisia inabidi zikae pembeni kabisa, hata kama mnapendana kiasi gani, kupendana kwenu hakuwezi kuokoa biashara inayokufa, mtu akifanya makosa mnapata hasara na biashara ndio imekufa.

Ili kupata mtu makini wa kufanya nae biashara fanya mambo haya matatu;

1. Mchunguze na mjue vizuri mtu unayekwenda kufanya nae biashara. Hata kama mtu unayekwenda kufanya nae biashara ni ndugu au rafiki, una kazi kubwa sana ya kumjua vizuri. Unahitaji kupata muda wa kumchunguza na kujua tabia za mtu unayetaka kushirikiana nae kwenye biashara. Jua mtazamo wake kwenye maisha ukoje, jua anaamini nini na jua mipango yake ya mbeleni ikoje. Angalia vitu hivi kama vinaendana na vile ambavyo unavyo wewe. Kama wewe unafikiria baada ya miaka kumi biashara unayofanya iwe imesambaa dunia nzima, na mwenzako anafikiria biashara mnayofanya impatie tu fedha ya kula na kuendesha maisha umeshapotea.

Pia wakati unamchunguza mshirika wako huyo hakikisha ana sifa hizi tatu; 1. anapenda kufanya kazi kwa bidii na maarifa, 2. ni mwaminifu, 3. ni mwadilifu. Kama amekosa hata sifa moja tu kati ha hizo tatu kimbia haraka sana, atakuingiza kwenye matatizo makubwa.

Kujua vizuri kuhusu sifa hizi tatu soma hapa; Misingi mitatu muhimu ya kujijengea mwaka 2015.

Usijidanganye kwamba mtu mzima unayekutana naye kwa ajili ya kufanya biashara atabadilika kwa sababu yako, hata akikuahidi hivyon ni uongo.

2. Yajue mapungufu yako na tafuta mtu ambaye anaweza kuyafunika.

Huwezi kufanya kila kitu, japokuwa biashara inakutaka ufanye kila kitu, kuanzia kupanga wazo zuri la biashara, kununua, kuuza, kufanya mahesabu, kutangaza na vingine vingi. Kuna baadhi ya maeneo ya biashara ambapo unaweza kuwa hafifu sana. Hakikisha mtu unayeshirikiana nae kwenye biashara yuko vizuri kwenye maeneo hayo. Hii itawafanya muweze kufikia mafanikio kwa kukusanya nguvu zenu. Ila kama wote mna mapungufu yanayofanana mnajiandaa kushindwa kwenye biashara hiyo. Kama wewe ni mtekelezaji mzuri ila sio mbunifu mzuri wa mawazo tafuta mtu ambaye ni mbunifu mzuri wa mawazo. Ukitafuta mtekelezaji mzuri kama wewe mtatekeleza nini?

3. Wekeni makubaliano kabla ya kuingia kwenye biashara. Watu wengi wanaingia kwenye biashara kienyeji sana. Kwa sababu tu mnajuana mnaona hakuna tatizo, tunaaminiana tufanye biashara, kosa kubwa sana. Ni vyema mkakaa chini na kuwekeana makubaliano nyie wenyewe kwa wenyewe ni jinsi gani mnakwenda kuendesha biashara yenu na ni maamuzi gani ambayo hayawezi kufanyika na mtu mmoja. Lazima muwekeane mipaka na kila mtu aheshimu makubaliano hayo. Hii itawazuia kuingia kwenye hasara. Kwa mfano mwenzako anakutana na kitu kizuri kinachohusiana na biashara yenu kinauzwa kwa bei rahisi, anaamua kununua halafu anaishia kutapeliwa. Kama mngekuwa mmewekeana utaratibu wa kwamba mtu hawezi kufanya manunuzi makubwa bila ya kumshirikisha mwenzake hasara kama hii mngeiokoa.

Haya ni mambo matatu muhimu sana unayotakiwa kufanya kabla ya kuingia kwenye ushirikiano wa kibiashara na mtu. Hata kama tayari upo kwenye ushirikiano huu na unaona kila siku unakusumbua, fanya hatua hizi tatu na muhimu sana fanya hatua ya tatu. Kaa chini na mwenzako kisha wekeni utaratibu ambao utakuwa na faida kwenye biashara yenu.

Kama utaogopa au kuona aibu kumwambia mwenzako muweke mipango upya, subiri siku utakayopata hasara na biashara kufa ndio aibu itakuisha, maana hakutakuwa tena na biashara na hata ikiwepo utakuwa umeshachoka.

Nakutakia kila la kheri katika mafanikio ya biashara yako.

TUPO PAMOJA,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.

Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

kitabu-kava-tangazo4322

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: