Unacheza Hadithi Iliyoandikwa Na Nani? Fanya Mabadiliko Muhimu Leo.

Maisha ni kama mchezo wa kuigiza na sisi ndio waigizaji wenyewe. Katika mchezo wowote wa kuigiza kila muigizaji hupewa kipande chake cha kuigiza. Hupewa kila kitu anachotakiwa kufanya na yeye hufuata maelekezo na jinsi anavyotakiwa kuigiza.

Katika maisha yetu kuna mambo ambayo tunayafanya kila siku. Jinsi tunavyoishi maisha yetu inaweza kuathiriwa na sisi wenyewe au kuathiriwa na wale wanaotuzunguka.

katika maisha unayoishi, ambayo ndio igizo unalocheza umewahi kujiuliza ni nani aliyeiandika? Umewahi kukaa chini na kufikiria kwa nini unafanya kazi unayofanya? Kwa nini unafanya biashara unayofanya? Na kwa nini unaishi maisha unayoishi? Kama hujawahi kujipa nafasi hii, baada ya kusoma hapa leo chukua muda kufanya upya tathmini ya maisha yako.

Maisha unayoishi yanaweza kuwa yameandikwa na wewe mwenyewe au umeandikiwa na jamii inayokuzunguka.

Maisha ya kuandikiwa na jamii inayokuzunguka.

Sehemu kubwa ya maisha ya watu wengi yanatokana na kile jamii nzima inachofanya. Maisha haya yanatokana na hadithi iliyoandikwa miaka mingi na ambayo imekuwa ikirudiwa tena na tena na tena. Hadithi yenyewe inakuwa hivi; nenda shule soma kwa bidii, faulu vizuri, utapata kazi nzuri na yenye maslahi na hatimaye utakuwa na maisha mazuri. Hadithi hii ilikuwa nzuri sana kipindi cha nyuma na wengi walinufaika nayo. Habari ya kusikitisha ni kwamba ahadithi hii imepitwa na wakati. Hadithi hii haiendani tena na mazingira ambayo tunaishi. Tunaishi kwenye mazingira yenye changamoto nyingi sana, unaweza kusoma na kufaulu vizuri lakini ukakosa kazi. Unaweza kupata kazi lakini ikawa haina maslahi mazuri, haikupendezi kuifanya na changamoto nyingine nyingi

SOMA; HAKUNA ANAYEJUA ANACHOFANYA KWENYE MAISHA

Sehemu nyingine ya hadithi ambayo watu wengi wamekuwa wakiishi ni hii hapa; wewe umefeli shule, huwezi chochote na maisha yako yatakuwa magumu. Watu wengi wamekubali kucheza hadithi hii na jambo lolote linalotokea kwenye maisha yao wanarudi kwenye mstari waliopewa kwamba wewe huwezi chochote. Hata pale wanapokutana na fursa nzuri ya kuweza kuboresha maisha yako badala ya kuchukua hatua wanarejea mstari waliopewa kwamba wewe ulifeli shule unafikiri hilo utaliwezea wapi?

Kuna mstari mwingine maarufu ambao watu wengi wamekubali kuucheza na umekuwa sehemu ya maisha yao. Mstari huu ni wa kukosa ambapo kila mchezaji anaangalia nimekosa nini. Kwenye mstari huu mtu anaaminishwa kwamba maisha yake hayawezi kuwa bora kwa sababu amekosa vitu muhimu. Anaambiwa hawezi kufanya biashara kwa sababu amekosa mtaji, anaambiwa hawezi kufanikiwa kwa sababu ametoka kwenye familia masikini.

Kuna mistari mingi sana ambayo watu wanaishi bila hata ya kujijua. Tukisema tuiorodheshe hapa hatutafika mwisho.

Ufanye nini sasa?

Leo chukua hatua ya kujitathmini maisha yako, kuwa mwaminifu kwako binafsi na usijidanganye. Angalia kwenye kila eneo la maisha yako je kile unachofanya, au sababu unazotoa zinatoka ndani yako kweli au unafanya wka sababu ndicho ambacho kila mtu anafanya?

Kama utajikuta unacheza hadithi ambayo hujaandika mwenyewe, acha haraka na kaa chini uandike hadithi yako mwenyewe. Kaa chini uweke malengo na mipango ya maisha yako na kisha iofanyie kazi.

Ukishaandika hadithi yako usimsikilize mtu mwingine yeyote anayejaribu kukushirikisha hadithi yake. Tumia muda wako kuifanyia hadithi yako kazi kuliko kukaa na kuanza kuangalia wengine wanafanya nini na maisha yao.

Mfano wa hadithi mpya unayoweza kujiandikia;

Naweza kufanya chochote ambacho naamua kufanya na maisha yangu. Maisha ninayoishi ni yangu na hakuna anayeweza kuyabadilisha bila ya mimi mwenyewe kuwa na ridhaa. Naweka malengo yangu na kuyafanyia kazi kila siku.

Unaweza kutengeneza hadithi yoyote unayotaka wewe. Tengeneza hadithi ya kuwa mfanyabiashara bora kabisa, bila ya kujali unaanzia wapi au una elimu kiasi gani.

SOMA; Sababu 10 Kwa Nini Hutafikia Malengo Yako 2015.

Tengeneza hadithi ya kufikia mafanikio makubwa katika jambo lolote unalofanya kwa sababu una uwezo huo.

Kumbuka kila mtu ana uwezo mkubwa sana ulioko ndani yake. Kikubwa ni kutambua uwezo huo na kuweza kuutumia kufikia mafanikio makubwa.

Kila mara jiulize je hadithi unayocheza ndiyo uliyoandika au unacheza hadithi iliyoandikwa na wengine? Kuwa makini na maisha yako, kimbia mbio zako mwenyewe, usifuate kundi.

Nakutakia kila la kheri katika maamuzi mazuri unayokwenda kufanya kwenye maisha yako.

TUPO PAMOJA.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

kitabu-kava-tangazo4322

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: