Naweza kusema fedha ni moja ya neno rahisi sana ambalo kila mtu anaweza kulitamka ila ni msamiati mgumu sana ambao ni wachache sana wanaoweza kuuelewa. Hata mtoto mdogo anaweza kujua hii ni fedha na hata mtu asiyejua kusoma na kuandika, huwezi kumpiga chenga kwenye hesabu za fedha. Kuijua tu fedha sio tatizo, ila kuweza kuitumia vizuri ndio changamoto kubwa sana ambayo imepelekea kuwepo kwa matatizo mengi sana duniani.

Ni ukweli usiopingika kwamba asilimia kubwa ya matatizo tunayokutana nayo kila siku kwenye maisha yetu chimbuko lake ni fedha. Matatizo ya fedha ndio mzizi mkuu unaozaa matatizo mengine. Watu watachukiana, watu watapigana na hata watu wanaweza kuuana kwa sababu ya fedha?

Kwa nini hii fedha ndio ilete haya yote? Hilo sio lengo la makala hii ya leo. Leo hapa kwenye kipengele cha ushauri wa changamoto zinazokuzuia kufikia mafanikio tutajadili jinsi ya kukabiliana na changamoto ya matumizi ya fedha ili uweze kufikia uhuru kwenye maisha yako.

Kabla hatujaendelea na nini cha kufanya ili kuweza kuwa na matumizi mazuri ya fedha, tupate maoni kutoka kwa wasomaji wenzetu;

mimi kitu kinacho nisumbua hela napata lakini sielewi hii hela inaishaje nikiangalia sina matumizi makubwa nilikuwa naomba unisaidia niweze kutunza hela yangu

Mbinu ya kudhibiti chuma ulete hata ikibidi na mtu anaetoa chuma ulete nimjue

Matumizi yangu ni makubwa kuliko kipato, hal hii hunifanya nishindwe kufikia malengo yangu. Msaada tafadhii mkuu!

ninapata pesa lakini nashindwa kuzitunza
nifanyeje?

kila nikipata pesa cjui niitumieje japo hata kiasi kidogo ningeomba mwongozo

Kama tulivyoona hapo juu kuna watu wengi sana ambao wana matatizo ya kifedha.

Kuna ambao hawajui fedha wanayopata inaishia wapi na watu hawa wanashangazwa sana kiasi cha kuamini kwmaba kuna chuma ulete anayewaibia fedha zao. Kama tulivyowahi kusema hakuna chuma ulete, bali chuma ulete ni wewe mwenyewe na matumizi yako mabaya ya fedha.

Pia kuna ambao matumizi yao ni makubwa kuliko mapata yao. Hawa unaweza kusema ni watu ambao wameamua kulitafuta kaburi liko wapi na kuliendea. Hakuna kitu ambacho ni hatari zaidi ya matumizi kuzidi kipato.

Na pia kuna ambao wakipata fedha hawajui waitumieje. Yaani ni sawa na mtu ameamka usingizini na kukutana na burungutu la fedha, anajikuta analitumia tu hovyo na baadae kushindwa kuelewa fedha imekwenda wapi.

Kuna matatizo mengi sana kwenye fedha, hapa tutajadili mambo matano muhimu ya kufanya ili uweze kuondokana na matatizo ya kifedha kwenye maisha yako. Mengi ya yale tutakayojadili leo tulishajadili tena ila tutayarudia kwa sababu elimu ya mara moja tu haitoshi kumponya mtu ambaye amekuwa na matumizi mabovu ya fedha kwa miaka mingi kwenye maisha yake.

Hivyo soma makala hii kila siku, ili kuweza kuingiza kitu fulani kwenye akili yako kuhusu fedha kila siku. Na kidogo kidogo utaanza kuona mabadiliko.

SOMA; Fanya Mambo Haya Matatu Na Usipokuwa Tajiri Ndani ya miaka 10, sahau kuhusu utajiri kwenye maisha yako.

1. Jua mapato na matumizi yako.

Hii ni hatua ya kwanza kabisa ya kuweza kuwa na usimamizi mzuri wa fedha zako. Ni muhimu kujua kipato chako na pia kujua kinatoka wapi. Pia jua matumizi yako na kitu kingine chochote kinachokula kipato chako. Mapinduzi makubwa utakayoyafanya kwenye maisha yako yatakuwa haya; kwanza kupunguza kabisa matumizi yako na kubaki na matumizi yale ambayo ni ya msingi tu. Na pili kuongeza kipato chako, kwa kujua kinatokea wapi unaweza kuangalia ni jinsi gani unaweza kukiongeza zaidi.

Kwa kuanzia na kuongeza kipato angalia ni jinsi gani unaweza kulipwa zaidi. Kama umeajiriwa angalia ni jinsi gani unaweza kuongeza thamani ya kazi yako na ikapelekea wewe kuliwa zaidi. Na kama umejiajiri au unafanya biashara angalia ni jinsi gani unaweza kuikuza biashara yako zaidi na kuwafikia wateja wengi au kuwafanya wateja ulionao kununua zaidi na wewe ukapata faida zaidi. Usijidanganye kwamba haiwezekani, kama utakuwa na nia ya kweli kila kitu kinawezekana.

SOMA; Njia KUMI Za Kubana Matumizi Yako Mwaka Huu 2015.

2. Kuwa na majeti.

Hivi unafikiri kwa nini serikali inakwenda kukaa bungeni Dodoma kwa miezi zaidi ya miwili kujadili bajeti ya taifa? Kwa sababu huu ndio msingi muhimu kwenye matumizi ya fedha(sahau kuhusu matumizi yao mabaya). Bajeti ni muhimu sana kwa sababu kama kitu hakijapangiliwa kitatumika hovyo. Waangalie watu wote ambao wana matatizo ya fedha ni watu ambao hawana bajeti ya matumizi yao ya fedha.

Andaa bajeti yako ya kila siku, kila wiki na kila mwezi. Jua ni kiwango gani cha juu kabisa kwako kutumia na kazana usivukoe kiwango hiko. Ikiwa kwa hali yoyote ile umevuka kiwango hiko, ni lazima ulipe. Kwa mfano kama bajeti yako ni kutumia tsh elfu 20 kwa siku, na siku moja ukajikuta umetumia elfu 30, ina maana kwa siku chache zinazofuata utahitaji kutumia chini ya elfu 20 ili kurekebisha hili deni ambalo umetengeneza hapo.

Hili linahitaji nidhamu kubwa kwa sababu hakuna atakayekushikia fimbo kama usipofuata ila kumbuka unaharibu maisha yako mwenyewe kama unashindwa kusimamia kile ulichopanga.

SOMA; Maazimio Matano Muhimu Ya Fedha Kwa Kila Kijana Kuweka Mwaka Huu 2015.

3. Jilipe wewe kwanza.

Nafikiri hiki ndio kitu kikubwa ambacho nimekuwa nikiongea kwa kujirudia rudia karibu kila mara ninapoandika kuhusu fedha. Jilipe wewe kwanza. Kama unavyopata fedha ukanunua nguo, ukanunua chakula, ukanunua starehe na kadhalika, hawa wote unawalipa, ila unamsahau mtu muhimu ambaye ni wewe mwenyewe. Katika kipato chochote ambacho unapata jilipe wewe kwanza asilimia 10 ya kipato hiko. Zoezi hili lifanye kabla hata hujaanza kufanya matumizi yako ya kawaida. Sitaeleza sana hili maana nilishaliandika na kuandika na kuandika tena. Kama hujaelewa au unapata changamoto kwenye kuweka asilimia hii 10 niandikie email kwenye makirita@kisimachamaarifa.co.tz

4. Epuka kutumika kwa faida ya watu wengine.

Kwa bahati mbaya sana kipato hiko kidogo unachopata, au hata kama ni kikubwa kuna watu wengi sana ambao wanakinyemelea. Kuna mtu atajitokeza tu mbele yako na kukuambia anauza nguo nzuri na ukiziangalia ni nzuri kweli na wewe bado unahitaji nguo nzuri na hivyo unanunua. Unakatiza mtaani unaona sehemu wanachoma nyama tamu kweli, unashawishika kuingia unakula nyama choma na wakati mwingine unashusia na bia. Unatoka hapo unakutana na mtu anakuambia ana wazo zuri sana la kibiashara na kama ukimpatia kiasi fulani atakulipa vizuri sana baadae, unampa kiasi hiko. Baada ya muda umebaki na kiasi gani cha fedha? Hakuna halafu utakuja kushangaa kwamba hujui fedha zako zinaishia wapi.

Kama unataka kujitengenezea uhuru wa kifedha anza kwanza kudhibiti tamaa yako ya matumizi ya fedha. Usishawishike kirahisi kutoa fedha yako, fuata utaratibu ambao umejiwekea kwenye bajeti.

5. Nunua vitu kwa ujumla.

Kama katika manunuzi yako ya kila siku unapoteza tsh elfu moja tu, umeamua kujijengea umasikini mwenyewe. Shilingi elfu moja ni mbegu ya kutosha kabisa ambayo kama ukiipanda vizuri kila mtu atakushangaa jinsi ambavyo utabadilika. Fanya manunuzi yako yote kwa ujumla. Kama unanunua vyakula vya familia, badala ya kununua mchele kila siku kw akilo moja shilingi elfu mbili, unaweza kununua kilo kumi kwa shilingi elfu moja mia nane kwa jumla. Hapo tu umeokoa shilingi elfu mbili. Endelea hivyo hivyo kwenye vitu vingine vyote unavyonunua. Hata kama ni nguo, usinunue tu kwa sababu umekutana nayo, kuwa na wakati maalumu ambapo unanunua nguo kwa pamoja na hivyo kuweza kupunguziwa bei.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.

Kuna mambo mengi sana unayoweza kuyafanya ili kuwa na usimamizi mzuri wa fedha zako na kujitengenezea uhuru wa kifedha. Haya matano tuliyojadili hapa ni yale ya msingi kabisa. Anza nayo leo hii na sasa hivi ili uweze kujitengenezea uhuru wa kifedha. Na kama nilivyosema hapo juu soma makala hii kila siku, ihifadhi au hata ichapishe na uweze kuisoma kila siku. Pia unaweza kumpatia mwenzako wa karibu ili nae ajue kwamba mnahitaji kufanya mabadiliko katika matumizi yenu ya fedha.

Nakutakia kila la kheri katika usimamizi mzuri wa fedha zako ili uweze kufikia uhuru wa kifedha.

TUPO PAMOJA.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.

Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

kitabu-kava-tangazo4322