Ili kuweza kufanikiwa na kuufikia utajiri, ni safari ambayo huwa inahitaji uvumilivu wa kutosha kutokana na changamoto nyingi ambazo huwa tunakutana nazo mara kwa mara. Changamoto hizi huwa ni kama ukuta, ngome ama daraja linawazuia wengi kufanikiwa na kuwa matajiri. Kutokana na changamoto hizi, wengi hujikuta tayari wamekata tamaa na kushindwa kutimiza lengo la kuufikia utajiri katika maisha yao.

Lakini, pamoja na changamoto hizo nyingi huwa ni lazima tuweze kuzivuka ili kufikia mafanikio makubwa na hatimaye kuwa matajiri. Ni changamoto ambazo huwa haukutani nazo wewe tu, kila mmoja hukutana nazo kwa sehemu yake. Unaposhindwa kuzivuka changamoto hizo na kujikuta zimekukatisha tamaa, na huo ndio huwa mwanzo wa kujitoa mwenyewe kwenye safari ya kuelekea kwenye utajiri.
Katika makala hii ya leo tutakwenda kuzungumzia changamoto hizo ambazo huwa zinawazuia wengi kufanikiwa. Ni muhimu sana kwako kuzivuka changamoto hizi hata kama zinaonekana kwako kama ni ukuta ama ngome inayokuzuia kufanikiwa. Hauhitaji kuwa na wasiwasi wala woga makala hii itakusadia kujua jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo ili uweze kufanikiwa. Ni changamoto zipi unazotakiwa kuzivuka ili kuufikia UTAJIRI?
Hizi Ndizo Changamoto Kubwa Unazotakiwa Kuzivuka ili Kufikia UTAJIRI.
1. Wasiwasi wa kuanza jambo jipya.
Hii huwa ni moja ya changamoto kubwa inayowakabili wengi katika maisha yao. Watu wengi sana huwa ni waoga wa kuanza kitu kipya katika maisha yao. Woga huu huweza kuwasababisha wawe watu wa kusita sita kila siku na mwisho wa siku wanajikuta wakiwa ni watu ambao hawajafanya kitu kabisa katika maisha yao.
Kama unataka kubadili mwelekeo wa maisha yako, kitu unachotakiwa kujifunza ni kutokuwa na wasiwasi sana pale unapotaka kuanza jambo jipya. Kumbuka hakuna aliyezaliwa anafanya hilo jambo kila mtu amejifunza, hiyo ikiwa na maana hata wewe unaweza ukajifunza na ukaweza. Jiamini kisha fanya kitu, utafanikiwa.
  
2. Kufanya kazi kwa mazoea.
Haijalishi ni kazi ama kitu gani unachokifanya kwa sasa, kama bado unaendelea kufanya kazi kwa mazoea, kufikia mafanikio makubwa kwako itakuwa ngumu. Hii ndiyo changamoto mojawapo inayokukabili bila kujijua na unaitakiwa uivuke ili uweze kuufikia mafanikio makubwa na hatimaye kuwa utajiri. Watu wengi wenye mafanikio makubwa wanalijua hili, ni watu wa kufanya mambo yao sio kwa mazoea.
Unapokuwa unafanya mambo yako kwa mazoea ubunifu na ufanisi wako unakuwa unapungua na mwisho unajikuta hakuna kikubwa cha maana unachokifanya. Nenda kinyume na utaratibu uliouzoea kama haukuletei matunda unayotaka, vinginevyo hutafanya kitu chochote cha maana katika maisha yako. Kumbuka, kuwa na mafanikio makubwa unahitajika kuwa jasiri na kuvunja  mazoea yanayokukwamisha.
3. Kufanya kazi bila kuona matokeo chanya.
Wengi wetu huwa ni watu wakutaka kuona tunapoanza kufanya jambo tuone matokeo ya haraka na papo hapo. Matokeo ya namna hiyo yanaposhindwa kupatikana kwa wengi huwa ni kama ukuta mnene unaowazuia kufanikiwa. Matumaini walikuwa wamejiwekea yanakuwa yanakufa na kuona kama mwisho wa mafanikio yao kama umefika.
Kiuhalisia, hii huwa ni moja ya  changamoto kubwa inayowazuia wengi kufanikiwa, lakini ambayo ni lazima uivuke ili kuweza kuufikia utajiri. Kuna wakati matokeo kwa kile tunachokifanya huwa hayaji kwa haraka kama tunavyofikiri, huwa tunatakiwa kuwa wavumilivu na kung’an’ania mpaka tuone matokeo tunayoyataka yawe upande wetu.
4. Kutokuliamini sana wazo unalotaka kulifanyia kazi.
Watu wengi huwa ni watu wenye mawazo mazuri sana, ambayo kama wakiyatumia wanaweza kufika mbali sana kimafanikio. Lakini, tatizo kubwa ambalo huwa wanakuwanalo watu hawa, huwa ni watu wakujiuliza uliza sana kweli nikifanya kitu nitafanikiwa? Kwa kujiuliza huko sana hujikuta ni watu wakusitasita na kutokuchukua hatua mapema  za kubadili maisha yao. Hii pia huwa na changamoto inayowakabili wengi na kuwazuia kufanikiwa. Kama unataka kufikia mafanikio makubwa, jifunze kuyaamini mawazo yako na kisha yafanyie kazi  utaona matokeo makubwa.
5. Kukosa ushauri muhimu kutoka kwa wengine.
Hili ni changamoto ambayo huwa inatokea hasa pale unapoanza kufanya  jambo jipya na ukajikuta unakosa ushauri na mwongozo  wa maana kwa kile unachofanya. Wengi hali hii inapotokea huanza kujihisi kama  ni watu wa kupoteza tumaini na kuona hakuna njia. Unapokutana na hali kama hii jipe moyo, na kisha usikate tamaa. Tafuta kitu ambacho kitakusaidia kukupa hamasa ya kusonga mbele na kukutia moyo katika safari yako ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.
6. Kutokujisikia kufanya kitu chochote.
Hii ni changamoto ambayo huwa tunakutana nayo mara kwa mara katika maisha yetu na ni muhimu pia kuweza kuivuka ili kuweza kufika kule tunakotaka tufike. Kuna wakati huwa tunajihisi tumechoka ama hatujisikii kufanya kitu chochote na kujikuta ni watu wa kulala au kuangalia TV mpaka kunapitiliza. Hali hii unapoiendekeza inaweza ikakuletea uvivu ambao mwisho wa siku utakukwamisha kwenye mambo yako mengi zaidi. Unapokuwa unahisi huwezi kufanya kitu, pumzika kidogo kisha anza kufanya tena hata kama ni kwa kulazimisha.
Kila mmoja wetu huwa anakutana na changamoto ambazo huwa zinamzuia kufikia mafanikio yake. Ni changamoto ambazo huwa ni lazima tuzikabili bila ya kuuogopa wala kukata tamaa ili tuweze  kufikia mafanikio makubwa tulijiwekea katika maisha yetu.
Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kujifunza na kuboresha maisha yako zaidi.
Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika kila siku, mpaka maisha yako yaimarike.
IMANI NGWANGWALU,