Karibu mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA kwenye kipengele hiki cha USHAURI WA CHANGAMOTO ZINAZOTUZUIA KUFIKIA MAFANIKIO. Katika kipengele hiki unapata nafasi ya kujifunz ambinu mbalimbali za kupambana na changamoto unazokutana nazo kila siku kwenye kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla na zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa.

Leo tutajadili changamoto ya majungu kwenye eneo la kazi. Majungu kwenye eneo la kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla ni kitu ambacho kimekuwepo kwa muda mrefu. Ni kitu ambacho kimekuwa kikiwasumbua watu wengi na hata kuwasababishia wengine msongo wa mawazo. Hata wahenga walisema penye riziki hapakosi fitina. Hivyo majungu yapo na yataendelea kuwepo.

Kwenye makala hii ya leo hatutaangalia jinsi unavyoweza kukomesha majungu haya bali jinsi gani unaweza kuyaepuka na yasiwe kikwazo kwako kufikia mafanikio unayotarajia. Kabla ya kuangalia ni jinsi gani unaweza kuepuka majungu haya tupate maoni ya msomaji aliyeomba kushauriwa kuhusu jambo hili;

Hello habari za asubuhi Bw. Makirita, Naomba msaada wako kwenye hili: Nipo kwenye Ofisi ya Huduma kwa Wateja(Customer Care) yenye Magombano na Malumbano kila leo nami ndiye Mwanaume pekee kati ya Wanawake 9. Alafu Kiongozi wao Hanipendi hata kuniona, hanipi ushirikiano na kunifanyia Umbea kwa Boss kwa kupeleka maneno ambayo sio sahihi kama kusema mimi sifanyi kazi yangu n.k. Sijui Nifanyeje japo nshamwita tuongee na amekataa.?
Naomba msaada wako wa ushauri tafadhali!!
Ahsante na samahani kwa Usumbufu.

Kama tulivyoona hapo juu, mwenzetu anakutana na wakati mgumu kwenye kazi yake kutokana na malumbano na na majungu kutoka kwa wafanyakazi wenzake.

SOMA; Kauli KUMI Za Confucius Zitakazokuhamashisha Kuboresha Maisha Yako.

 

Ni njia gani unaweza kutumia kuepuka malumbano na majungu haya?

1. Jua majukumu yako ya kazi.

Unapoajiriwa, unapangiwa majukumu ya kazi. Kwamba wewe unaajiriwa katika ngazi fulani na majukumu yako yatakuwa haya. Sasa yajue vizuri majukumu yako ya kikazi na hakikisha unayatekeleza kwa kiwango cha juu sana. Usiangalie wengine wanafanya nini, angalia wewe unatekelezaje majukumu ambayo umeajiriwa kuyatekeleza. Kama hujui namjukumu yako ni yapi, ongea na kiongozi wako au bosi wako akupe ufafanuzi wa majukumu yako ya kikazi ni yapi.

2. Usiwe sehemu ya majungu.

Jambo jingine muhimu sana la kufanya ni kuepuka kwa njia zote kuwa sehemu ya majungu. Usisikilize wala kusambaza umbea wa aina yoyote kwenye kazi yako. Kama mfanyakazi mwenzako atakufuata na kuanz akukuambia mambo ya umbea, mkatishe haraka na badilisha mada mnayozungumzia, kama anaendelea kusisitiza majungu onesha una kazi unahitaji kumaliza. Kwa sehemu kubwa watu wanakujumuisha kwenye majungu kwa sababu na wewe unapenda kusikiliza au kusambaza maneno ya umbeya ya watu wengine.

SOMA; Mambo Kumi Muhimu Kuhusu Maisha

 

3. Jua nini chanzo cha majungu.

Majungu hayatokei tu kwa sababu watu wanapenda kufanya majungu. Bali majungu yana chanzo chake na kulingana na utofauti wa kila kazi, kuna aina mbalimbali za majungu. Jua kwenye eneo lako la kazi chanzo cha majungu ni nini. Wakati mwingine wapika majungu ni wafanyakazi ambao wanaona nafasi yao kwenye kazi ni ya chini sana kuliko wewe na hivyo nafasi pekee ya kukuumiza wewe ni kukusema vibaya. Kwa kujua hili, majungu yao hayatakuumiza tena kwa sababu unajua wao ndio wanaumia kuliko hata unavyoumia wewe.

4. Badili mtizamo wako.

Huwezi kubadili tabia za watu kuhusu majungu ila unaweza kubadili mtizamo wako, unaweza kubadili jinsi unavyopokea majungu hayo. Ona kwamba kinachotokea kwenye ofisi yenu sio kitu kipya na kwamba hakiwezi kuwa na madhara kwako kama utafanya kazi yako kwa ubora wa hali ya juu na kuacha kufuatilia maisha ya wengine. Pia badili mtizamo wako kwamba unafanyiwa majungu kwa sababu wewe pekee ndio mfanyakazi wa kiume na wanawake ni wengi. Chukulia kwamba jambo kubwa kwao ni kuongelea maisha ya wengine na pia jua kwamba maneno yao tu hayawezi kukumiza kwa njia yoyote.

5. Tofautisha maisha yako ya kazi na maisha yako binafsi.

Watu wanapojua maisha yako binafsi kwa kiasi kikubwa ndio wanavyozidi kupata nafasi kubwa ya kukufanyia majungu. Kwa kuwa umeshaona eneo lako la kazi limejaa majungu, hakikisha watu wanachojua kuhusu wewe ni kazi unayofanya pale tu. Usitoe taarifa nyingine za maisha yako binafsi, acha watu wakujue kwenye kazi kwa kazi unayofanya tu. Kwa sababu unavyowapa nafasi ya kukujua zaidi ndivyo watakavyoendelea kukusimanga zaidi.

SOMA; Huu Ni Mwaka Wa Kuacha Unafiki…

6. Usiyachukue majungu moyoni.

Njia nyingine bora ya kuepuka majungu au madhara ya majungu ni kuyachukulia kama kitu cha kawaida. Usiyaweke moyoni kama ni kitu ambacho ni kikubwa sana au chenye madhara sana. Chukulia kama ni mchezo wa watu ambao hawajui kilichowapelekea kazini. Chukulia kwamba majungu hayo ni sehemu ya changamoto za kazi na unahitaji kutoyahusisha na maisha ya kawaida.

7. Angalia tabia za mfanyakazi anayeheshimika.

Katika eneo lolote la kazi huwa kuna mfanyakazi anayeheshimika. Mtu huyu anakuwa na uzoefu mkubwa kwenye kazi hiyo na wengine huenda kuomba ushauri kwake. Jaribu kuangalia tabia za mfanyakazi huyo na jinsi gani ambavyo anaepuka majungu.

8. Usijihusishe kwenye mashindano.

Malumbano yoyote yanatokana na mashindano, kwamba uonekane wewe ni  bora zaidi au kutaka kuonesha kwamba kitu fulani sio sahihi. Sasa wewe usijihusishe na mashindano ya aina hii. Waache watu waseme na wala usijaribu kujisafisha au kuwazuia. Wanasema ukibishana na mjinga anakushusha kwenye ngazi yake ya ujinga halafu anakushinda kwa uzoefu. Hivyo wewe puuzia, na anza kukazana kufanya mambo mengine ambayo yataifanya kazi yako kuwa bora zaidi. Hukuajiriwa kufanya mashindano na maneno ya watu hayawezi kuubadili ukweli, ukweli utabaki kuwa ukweli na siku moja utajidhihirisha.

SOMA; Je Upo Tayari Kupata Unachotaka? Siri Ni Hii Moja…

9. Usipatikane kwa ajili ya majungu.

Njia ya mwisho tutakayojadili hapa ni wewe kutopatikana kwa ajili ya majungu. Kama tulivyosema kwanye njia ya kwanza fanya kazi yako kwa ubora wa hali ya juu na kuwa makini na kazi yako. Muda ambao hufanyi kazi, hakiksha una kitu kinachokufanya uonekane upo ‘bize’ na hivyo kutopatikana kwa ajili ya majungu. Njia moja ya kufanya hivyo ni kuanz akujisomea vitabu. Kuwa na kitabu muda wote unapokuwa kazini na muda wa mapumziko utumie kusoma kitabu chako. Kwa kufanya hivi utakosa muda wa kusikiliza au kujibu majungu yanayoendeshwa dhidi yako.

Fanya mambo hayo na mengine mengi utakayoendelea kujifunza. Hali hiyo ya majungu inaweza isiishe haraka ila kama utaendele akufanya haya tuliyojadili hapa waendesha majungu dhidi yako watakosa jambo jipya la kukupikia majungu na hata wakilipata majungu yako hayatakuwa na raha tena kwao kwa sababu umeshaamua kuyapuuza. Ila unavyokazana kupambana nao ndio wanazidi kutafuta majungu zaidi ili kukushinda.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya kazi yako.

TUPO PAMOJA.

Makirita Amani.

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.

Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

kitabu-kava-tangazo4322