Mara nyingi wengi huwa ni watu wa kujiuliza zaidi wafanye nini ili waweze kufikia mafanikio makubwa katika maisha yao. Hufikia hatua hii ya kujiuliza swali kama hili pengine baada ya kuona mambo au mipango mingi waliyojiwekea inakuwa haiendi sawia kama walivyokuwa wamejipangia katika maisha yao binafsi.

Pamoja na kujiuliza swali hilo muhimu lakini wengi kwa bahati mbaya huwa hawapati jibu sahihi la nini cha kufanya ili kuweza kufikia mafanikio hayo. Wengi hujikuta tu ni watu wa kuhangaika na kufanya mipango na malengo yao bila ya utaratibu maalum, hali ambayo huweza kupelekea wengi kujikuta wameshindwa katika maisha yao.

Kwa hali ya kawaida ambayo hahitaji uwe umeenda darasa lolote la uchumi au uwe na digirii ya aina fulani, tofauti na kujiwekea mipango na malengo yako vizuri, ili uweze kufanikiwa na kufikia mafanikio makubwa sana katika maisha yako, unahitaji kuwa na kitu hiki cha ziada yaani, kuwa wewe kama wewe katika maisha yako na si vinginevyo.

kuwa wewe

Wengi wetu kutokana na kutokujua mara nyingi hujikuta ni watu wa kufuata mikumbo au makundi bila hata kujua hilo kundi linawapeleka wapi. Kiukweli hutaweza kufanikiwa sana katika maisha yako kama utakuwa ni mtu wa kufuata mkumbo. Maisha yako yatabadilika na kuwa ya mfanikio makubwa zaidi, pale utakapoanza kuamini na kufuata ndoto zako.

Kati ya vitu ambavyo unatakiwa uviepuke kwa sasa ili visiweze kukupeleka kubaya na kujikuta ukishindwa kutimiza ndoto zako ni kufuata kundi fulani. Jifunze kusimamia malengo na mipango  yake mpaka uifanikishe. Acha kuishi kama wengine wanavyoishi ishi maisha yako mwenyewe. Unapoamua kufuata kundi unakuwa ni sawa na kutembelea njia ama ndoto za wengine. Na kwa kutembelea ndoto za wengine hii itakufanya hutafika popote katika maisha yako.

SOMA; Mambo makubwa mawili yanayokuzuia wewe kufikia ndoto zako.

Kuwa wewe kama wewe kwa kufanya mambo ambayo unaamini yatakufikisha mbali kimafanikio kuliko ambavyo unataka kuiga kila kitu. Ni bora ukashindwa kufanikisha mambo yako ukiwa wewe kama wewe kuliko ambavyo ungeshindwa huku ukiwa umefuata kundi au umeiga. Kinachokutokea unaposhindwa huku ukiwa umeiga ni lazima utaanza kujilumu sana kwa kuona kuwa kama kuna mtu aliyekusababisha ukashindwa huko.

Acha kabisa kuangalia wengine ama kujilinganisha na wengine na kutaka kuwa kama wao. Kama kila wakati utataka kung’ang’ania kuwa kama wao, hebu jaribu kufikiri upya tena ni lini utakuwa wewe kama wewe unayejisimamia kiasi kwamba wengine wakufuate au waige mwenendo mzima ulionao kimaisha?

SOMA; Kimbia mbio zako mwenyewe.

Kumbuka pia kila unapojaribu kuwa kama mtu mwingine kinachotokea kikubwa katika maisha yako utaanza kujilinganisha sana, kujikosoa sana na mwisho wa siku utajikuta huwezi kusonga mbele kama ambavyo ulikuwa ukitarajiwa iwe katika maisha yako.

Katika hii dunia acha kusumbuliwa au kubabaishwa na kuiga au kufuata kundi ambalo halikuhusu, utapotea. Kumbuka kila mtu amekuja duniani akiwa na malengo yake. Chukua muda wa ziada, kaa chini, kisha tafakari nini hasa malengo yako unayotaka kuyatimiza ukiwa hapa duniani. Ukishajua hilo anza kuchukua hatua kwa kutekeleza ndoto zako.

Kama utakuwa ni mtu wa kuiga na kufuata mkumbo katika maisha yako na kushindwa kujisimamia wewe kama wewe katika maisha yako uwe, na uhakika hautafanikiwa sana katika maisha yako. watu wengi wenye mafanikio makubwa mara nyingi huwa wao kama wao katika maisha yao bila kuogopa kitu.

Haijalishi watu watasema nini, au wataongea nini juu ya kile unachokwenda kukifanya ambacho umekisimamia wewe mwenyewe na kuwa wewe kama wewe. Kikubwa jiamini, kisha songa mbele, kwani kuwa wewe kama wewe ni hatua muhimu sana kwako ambayo unatakiwa uijue ili uweze kuwa na mafanikio makubwa katika maisha yako.

Kwa kadri unavyoendelea kuwa wewe kama wewe hii inakusaidia sana katika maisha yako kuweza kujiamini, kujua mipaka yako ni ipi na hata kutambua thamani kubwa uliyonayo ndani mwako na kuweza kuitumia kukuletea mafanikio makubwa unayoyahitaji katika maisha yako.

Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.

Nakutakia Kila kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea AMKA MTANZANIA  kila siku kujifunza na kuhamasika.

TUPO PAMOJA,

IMANI NGWANGWALU,

0713 048 035,

Ingwangwalu@gmail.com

dirayamafanikio.blogspot.com