Habari za leo msomaji wa KISIMA CHA MAARIFA, karibu kwenye kipengele hiki cha jinsi ya kujijengea tabia za mafanikio. Kupitia kipengele hiki tunajifunza tabia mbalimbali ambazo ni muhimu sana wewe kuwa nazo ili kuweza kufikia mafanikio.
Kama wote tunavyojua ni kwmaba tunajenga tabia halafu baadae tabia zinatujenga. Tatizo kubwa tulilonalo kwenye jamii zetu ni kwamba tunajenga tabia ambazo hazina faida kwetu. Tunajenga tabia kwa sababu kila mtu ndio anafanya kitu hiko, hii inakuwa tatizo kubwa sana kwetu baadae.
Tabia tunazojifunza bila ya kujua zina msaada gani kwetu baadae zinakuwa kikwazo kwetu kuweza kufikia mafanikio. Kila mwezi tumekuwa tunajifunza na kujadili tabia moja muhimu sana itakayokuwezesha wewe kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Mwezi huu wa nne tutajifunza na kujadili jinsi ya kujijengea tabia ya shukrani. Hii ni tabia muhimu sana ambayo watu wote wenye mafanikio wanayo. Ni vigumu sana wewe kufikia mafanikio makubw akama huna tabia ya shukrani. Katika wiki nne za mwezi huu, kila jumanne tutajifunz ayafuatayo;
1. Maana ya tabia ya shukrani.
2. faida za tabia ya shukrani.
3. Jinsi ya kujijengea tabia ya shukrani.
4. Uhusiano kati ya tabia ya shukrani na mafanikio makubwa.
Nini maana ya tabia ya shukrani?
Nafikiri kila mmoja wetu anajua maana ya shukrani. Unapopewa kitu, au unaposaidiwa kitu unategemewa kushukuru kwa kile ulichopewa au kusaidiwa. Kama mtu amekupa au kukusaidia kitu na wewe ukamshukuru, sio kwamba shukrani yako inamlipa alichotoa, bali inamwonesha kwamba umejali kile ambacho amefanya kwako. Na hata wakati mwingine ukiwa na hitaji atakuwa tayari kukusaidia kwa sababu anajua utajali kile ambacho atakufanyia.
Kama mtu akikupa kitu au kukusaidia na wewe usipotoa shukrani, sio kwamba utakuwa umemdhulumu lakini hawezi kujisikia vizuri. Ataona kama juhudi zake za kukusaidia wewe zimedharauliwa na kupuuzwa. Hata wakati mwingine utakapohitaji msaada wake hawezi kuwa tayari kukusaidia kwa sababu anajua hata akifanya hivyo hutojali kle atakachokufanyia.
Sasa hii ni maana ya shukrani kwa uhusiano wa mtu mmoja na mtu mwingine. Hii karibu kila mtu anaifanya na haina changamoto kubwa sana. Ila kuna tabia nyingine ya shukrani ambayo ni muhimu sana kwako kufikia mafanikio. Hii ni tabia ya kushukuru sio tu kwa wale ambao wamekufanyia jambo jema ila kushukuru kwa maisha yako yote ambayo unayo mpaka sasa.
Kwenye swala la mafanikio kwenye maisha tabia ya shukrani imekaa tofauti kidogo. Tabia ya shukrani ili kufikia mafanikio makubwa tutakayojifunza hapa itajumuisha hiyo ya kusema asante kwa anayekusaidia na tabia ya kuwa na shukrani kwa maisha yako kwa ujumla.
Maisha ni magumu, maisha yana changamoto, maisha yana matatizo. Hata mtu awe na fedha kiasi gani, hata mtu awe na ujuzi kiasi gani, bado atakutana na changamoto kwenye maisha yake na bado maisha yake yatakuwa na matatizo. Kwa kifupi ni kwmaba hakuna maisha ambayo hayana matatizo. Lakini pia licha ya maisha kuwa na matatizo bado maisha ni mazuri, maisha yana furaha na hata kama mtu yuko hovyo kiasi gani, kuna vitu kwenye maisha yake anafurahia kuwa navyo.
Mtu anaweza kuwa masikini kabisa, hajui hata kesho atakula nini. Kwa kuamua kutumia umasikini huu kama kigezo cha yeye kuona maisha yake hayafai, ataona maisha yake ni ya hovyo sana na anawez akutamani hata yaishe tu maana hakuna anachofanya hapa duniani. Ila mtu huyu akiweza kuangalia upande wa pili wa maisha yake anaweza kuona vitu vitu vingi sana vitakavyomfanya ayafurahie maisha yake. Kwa mfano mtu huyu anawez akuwa na afya njema, viungo vyake vyote kwenye mwili vinafanya kazi. Anaweza kuwa na familia ambayo inampenda na kumjali vile alivyo. Anaweza kuwa uwezo wa kushawishi wengine kufanya jambo zuri na wakamsikiliza. Kwa kifupi anaweza kuwa na vitu vingi sana.
Sasa kama mtu huyu atatumia muda wake mwingi kulalamikia vile ambavyo anakosa, hawezi kupata muda wa kuangalia vile vizuri ambavyo tayari anavyo n ajinsi anavyoweza kuvitumia. Kwa kukosa tabia ya shukrani mtu huyu anazidi kuharibu maisha yake na kuzidi kupata matatizo zaidi. Wote tunajua kwamba kile unachofikiria sana kwenye akili yako ndio kinachotokea kwenye maisha yako. Hivyo kama unafikiria wewe ni mtu wa matatuzo tu, hayo ndio utakayoyapata maisha yako yote. Ila kama utaweza kuona kwaba licha ya matatizo uliyonayo bado una vitu vingi vizuri vya kufurahia na kuweza kufanya utaona matatizo yako ni madogo sana na hayatakuzuia wewe kufikia mafanikio yako.
Tabia ya shukrani ni tabia ndogo sana lakini ina faida kubwa sana kwenye maisha yako. Ni tabia ambayo ni rahisi kujijengea kwa sababu haihitaji wewe ubadili sana maisha yako kama tulivyojifunza kwenye tabia kama ya kujisomea, kutunza muda au matumizi mazuri ya fedha.
Karibu tuendelee kujifunz ana hakikisha mpaka mwezi huu wa nne unaisha unakuwa umebadilika sana katika kushukuru kw akile ambacho unacho kwenye maisha yako.
ZOEZI LA WIKI;
Katika kijitabu chako cha kuandika malengo, andika vitu vitano ambavyo unafurahia kuwa navyo kwenye maisha yako. Hata kama maisha yako ni magumu kiasi gani, wewe angalia ni vitu gani vitano ambavyo kila ukivifikiria kwenye maisha yako unaona matumaini. Hivi ndio vitakavyokuletea mafanikio makubw akwenye maisha yako. Ukishaandika vitu hivyo unaweza kutushirikisha na sisi hapo chini kwenye maoni. Karibu sana.
Nakutakia kila la kheri katika kujijengea tabia ya shukrani.
TUPO PAMOJA.
Kupata nafasi ya kujifunza tabia hii ya shukrani pamoja na tabia nyingine muhimu kama tabia ya uaminifu, kujali muda, matumizi mazuri ya fedha, kujisomea, kuacha tabia ya kuahirisha mambo na mengine mengi, jiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Bonyeza maandishi haya KUJIUNGA NA KISIMA CHA MAARIFA na utapata maelekezo ya kujiunga. Usikose nafasi hii muhimu ya kubadili na kuboresha maisha yako. Ingia kwenye kisima, jaza fomu na tuma ada ya uanachama na utapata nafasi ya kujifunza vitu muhimu vitakavyokuwezesha wewe kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Nakusubiri kwa shauku kubwa ili twende pamoja kwenye safari hii ya mafanikio makubw akwenye maisha yako. USICHELEWE.