Habari rafiki, ni matumaini yangu waendelea vizuri. Wiki hii tunaendelea na utaratibu wetu wa kushirikishana mambo 20 nilijifunza kwenye kitabu. Leo tunajifunza kutoka kwenye kitabu kinachoitwa DESIGN YourBestYear EVER. Kitabu kimeandikwa na DARREN HARDY.

1. Kwanza fahamu “Kwanini” kabla hujapotea kwenye kufahamu “Namna gani”. Kama Kwanini yako ni kubwa vya kutosha, namna gani ya kufikia malengo itakua rahisi. Wengi tunahangaika kutafuta njia za kufia malengo yetu, mwishowe tunapotelea huko. Know “Why” beforeyougetlostin “How.”

2. Anza kwa shukrani. Unapotaka kutengeneza mafanikio anza kwa kushukuru kwanza kwa wingi wa vitu ulivyonavyo tayari. Ukiwa na shukrani kwa vile ulivyonavyo, vitavutia upatikanaji wa vingine vingi zaidi. Tazama vitu ulivyonavyo, mali ulizo nazo, fursa ulizo nazo, kua na moyo wa shukrani kwanza kwa ulivyonavyo ndipo utakapoona njia nyingine zikifunguka.

3. Huwezi kupiga/kulenga mahali usipopaona. Kama hujui unakokwenda unaweza kuishia popote pale. Kuweka malengo kunakusaidia kuona unakotaka kwenda, kunakusaidia kulenga kisawasawa

4. Weka malengo ambayo yanakupa changamoto. Ukiona malengo uliyojiwekea hayakuumizi kichwa basi rudi jipange upya.

SOMA; Dunia Ya Wingi Na Dunia Ya Uhaba…

5. Andikamalengo yako. Usipoandika ni rahisi kusahau pindi unapokutana na changamoto au matatizo. Hatua ya kuandika ni ya kujasiri kuonyesha umedhamiria. Ukishaandika weka mahali ambapo utaweza kuona kila mara. Isipite siku hujasoma Malengo yako.

6. Jifunze kufanya tathmini ya mwaka uliopita. Kabla ya kuweka malengo mapya hebu fanya tathimini ya wakati uliopita. Orodhesha mambo kama 10 hivi yaliyotokea, na pia andika mambo uliyojifunza kutokana na hayo mambo 10.

7. Janga kubwa la maisha sio umasikini au njaa au kifo. Janga kubwa ni kushindwa kutumia uwezo wetu tulio nao.

8. Acha Mafanikio yako yahamasishe na kua ushuhuda kwa wengine. Mulika njia za wengine kwa tochi ya mafanikio yako ili na wao waone kwamba inawezekana kufanikiwa.

9. Hakikisha malengo yako ni yako kweli. Usiweke malengo kwa kufurahisha marafiki au ndugu. Usikubali mawazo ya watu au wana familia ndio ya kuongoze kuweka malengo hakikisha unafuata kile unachokitaka hasa.

10. Andaa orodha ya mambo/(malengo) 10 kisha kati ya hayo 10 chuja hiyo orodha na ufikishe malengo 3. Anza kuweka mpango wa utekelezaji wa hayo matatu.

11. Anza kwa kuligawa Lengo kubwa kwenye vipande vidogovidogo. Ukilivamia kama lilivyo lengo lako kubwa kwa ukubwa wake utekelezaji unakua mgumu. Ukitaka kumla tembo unamkata vipande vidogovidogo unaanza kutafuna taratibu mpaka anaisha. Vivyo hivyo kwa yale malengo makubwa fanya hivyo.

SOMA; Jambo Moja Muhimu La Kuzingatia Ili Uweze Kufikia Malengo Yako.

12. Anza kufanya kama vile tayari umeshafikia lengo lako. Kama ungekua tayari ni Milionea ungetembeaje, ungeongeaje ungeshikanaje mkono na watu au ungeingiaje nyumbani kwako? Anza kufanya vile ambavyo ungefanya ukiwa umefikia malengo yako

13. Mafanikio ya kweli na utoshelevu wa maisha ni pale unapokua na mafanikio nyumbani, katika masoko, mafanikio katika mwili wako, akili pamoja na roho yako. Mafanikio ya kweli ni yale yenye uwiano (balance).

14. Weka malengo yako katika hali ya sasa. Usiseme nataka kua Bilionea tarehe 14 Feb 2030, bali sema mimi ni Bilionea 14 Feb 2030, kusema wewe ni bilionea kutaumba nguvu ambayo itakwenda kutenda kazi kutengeneza kile ulichokiri.

15. WEWE ndio wakufanyia kazi na sio malengo yako. Unapoweka malengo wengi wetu tunamtazamo wa kufanya kazi kwa bidii ili kuyafikia malengo tuliyojiwekea, na asilimia kubwa hatuyafikii maana kuna kitu hua tunakosea. Swala hapa sio hayo malengo (afya njema, fedha nyingi, ndoa bora, biashara kubwa n.k) swala hapa ni WEWE. Kama utaendelea kufanyia kazi malengo yako halafu ukasahau kujifanyia kazi wewe, utaendelea kukimbizana nayo na hutayashika. Anza kwanza kujifanyia kazi WEWE. Kama unataka kua bilionea, anza kujitengenezea tabia za kibilionea, kusema kwako, kuwaza kwako kufanane na bilionea. Ufahamu wako wa ndani unatakiwa ushawishike kua wewe ni bilionea. Bila hivyo, ukajisumbua tu kukimbizana na malengo utafanikiwa kwa muda tu ila utarudi kwenye hali yako ambayo ndio umeizoea. Na ndio maana maskini akishinda bahati nasibu ya mamilioni baada ya muda anarudia hali yake umaskini. Weka nguvu yako kubwa katika kujiboresha WEWE na mafanikio yatakuja kulingana na kiwango cha ubora wako

16. Andika madhara utakayoyapata pindi utakaposhindwa kufikia malengo yako. Ni muhimu kufahamu sio tu ahadi utakazopata utimizapo malengo, bali ni muhimu vilevile kutambua maumivu ambayo utayapata pale utakaposhindwa kufikia malengo.

SOMA; Mambo 20 niliyojifunza Kwenye Kitabu LITTLE BETS.

17. Ni muhimu kufurahia mafanikio madogomadogo unayoyapata kwenye njia unayoelekea kwenye mafanikio makubwa. Usisubiri mpaka ufikie lengo ndiyo ufurahie, bali katika hatua unazopiga jifunze kufurahia hatua zenyewe. Hii itakupa nguvu kuendeleza mapambano kuelekea kwenye lengo lako kubwa. Jipongeze kwa kila hatua unayopiga

18. Washirikishe wengine (ndugu, marafiki au wafanyakazi wenzio) malengo yako. Pale utakapojua kwamba watu wanaelewa ulichojiwekea ahadi kukifikia, utajisikia kuwajibika zaidi. Ila kama malengo yako unayafahamu wewe tu, hata wakati fulani ukisikia kutokuendelea unaweza kufanya hivyo, maana hakuna anayejua.

19. Tafuta picha zitakazokuhamasisha na uweke sehemu utakapoweza kuziona kila wakati. Mfano tafuta picha ya gari unalotaka au nyumba ambayo unataka kuishi.

20. Hakikisha malengo yako yanaendana na tunu zako za msingi (Corevalues) pamoja na viwango vyako. Kama lengo haliendani na misingi yako au viwango uliyojiwekea basi mara moja weka pembeni, rudi jipange upya

Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com