Mambo 4 Yanayosababisha Uwe Na Fikra Hasi.

Wengi wetu  mara nyingi tumejikuta tukiwa watu wa fikra hasi sana. Tumekuwa ni watu wa kuwaza na kukusudia mabaya kwa wengine. Tumekuwa ni watu wa vijicho, husuda, choyo, wivu na hata tamaa mbaya. Hizo zote ni mojawapo ya fikra hasi ambazo tumekuwa tukizizalisha na kuwa nazo wenyewe pengine hata bila kujua.

Kutokana na kuwa na fikra hizi zimekuwa zikiwakwamisha na kuwarudisha nyuma wengi pasipo kujua. Pamoja na fikra hizo kuwa kikwazo kwa wengi, lakini kwa bahati mbaya wengi wamekuwa hawajui nini hasa chanzo ama sababu inayopelekea wao kuwa na mawazo hasi. Kwa haraka haraka naomba nikutajie mambo yanayosababisha uwe na fikra hasi katika maisha yako.

1. Maneno unayoambiwa mara kwa mara.
Fikra hasi mara nyingi zinaweza kujengwa ndani yako, kutokana na maneno unayoambiwa mara kwa mara katika maisha yako. Maneno unayoambiwa yanaathari kubwa sana juu ya maisha yako bila ya wewe kujua. Kwa sehemu kubwa, maneno yanayoongelewa juu yako yana uwezo wa kubomoa au kujenga maisha yako, hii yote inategemea na jinsi ama namna utakavyoweza kuyapokea.

Hebu jaribu kufikiria kuna wakati katika maisha yako uliambiwa huwezi hiki au kile na ni kweli uliamini hivyo. Pia kuna wakati uliweza kuambiwa kuwa wewe hufai au huwezi kufanikiwa na ndivyo kweli ulivyoamini kuwa hicho kisemwacho kipo sahihi. Kwa maneno hayo yalikujengea fikra hasi sana na kujiaminisha kuwa kweli huwezi na kitu ambacho kimekuwa kikutesa na kukusumbua.

Ni fikra hizi hasi ambazo wengi wetu tumekuwa nazo bila kujua, lakini ukija kuchunguza chake hasa ni maneno ambayo uliweza kuambiwa pengine ukiwa mtoto mdogo. Ili uweze kutokana na hali hiyo ni muhimu kwako kuweza kukataa na kutokubali kuyapokea maneno hasi uliyoambiwa. Kama uliwahi kuambiwa huwezi ni wakati kujiambia sasa unaweza. Kumbuka maneno uliyoambiwa ni sababu inmayopelekea wewe kuwa na fikra hasi.

2. Mambo unayosoma na kuyaangalia sana.
Kile unachokisoma ama kukiangalia mara kwa mara, kinauwezo wa kubadilisha maisha yako kabisa. Kama wewe ni mtu wa wa kusoma ama kuangalia habari hasi sana, elewa kabisa ndivyo maisha yako yatakavyokuwa. Kumbuka, wewe ni matokeo  ya kile unachokizingatia na kukiingiza katika fikra zako.

Wengi wetu tumejikuta tukiwa na fikra hasi sana kutokana na kujilisha vitu vingi hasi sana visivyotuhusu. Haiwezekani ukawa na fikra chanya kama wewe ni mtu wa kufuatilia na kushabikia habari nyingi hasi kwako ambazo zinaathiri maisha yako moja kwa moja. Wengi wamejenga mitazamo hasi kutokana na ufuatiliaji huu pasipo kujua iwe kwa kusoma au kuangalia Televisheni.

Ili kuweza kuondokana na hali hiyo na kubadili maisha yako, unahitaji kubadili mawazo yako na mtazamo chanya tu kwa kujilisha mambo yatakayoboresha maisha yako. Kama utaendelea kujilisha mambo mengi hasi ni wazi kabisa utaendelea kuwa hasi hivyo hivyo na uelewe kabisa hutaweza kufanikiwa kwa chochote kile.


3. Mazingira yanayokuzunguka.
Hii ni moja ya sababu kubwa sana inayosababisha wengi kuwa na fikra hasi. Mazingira yanayokuzunguka yana athari kubwa sana katika maisha yako. Katika hali ya kawaida ni vigumu sana kujenga mtazamo chanya kama mazingira uliyokulia ama uliyopo hayakupi changamoto yoyote ile ya kuweza kusonga mbele.

Tuchukulie kwa mfano unaishi na umekulia katika mazingira ambayo hakuna maendeleo makubwa. Kwa  kuishi mazingira hayo tu hiyo yote ni sababu tosha inakuyafanye na wewe uzidi kuamini sana kuwa na wewe uko duni kama mazingira hayo uliyopo.

Unaweza ukaliona hili kupitia kwa mtu mmoja mmoja, jamii ama kwa ujumla. Utagundua kuwa mara nyingi watu wanaoishi katika mazingira fulani, mitazamo yao inakuwa iko sawa kulingana na mazingira wanaoishi. Hivyo mazingira ni kitu mojawapo ambacho kinaweza kuharibu ama  kuboresha maisha yako.


4. Watu wanaokuzunguka.
Mara nyingi maisha yako kuna namna ambavyo yanaweza kuathiriwa kutokana na watu wanaokuzunguka. Kama kundi kubwa la watu wanaokuzunguka ni watu hasi ndivyo hivyo na wewe maisha yako ndivyo yatakavyo kuwa. Wote mtajikuta mpo katika usawa huo huo. Kama ni kulalamika na wewe utajikuta tayari ni mlalamikaji.

Kwa hiyo unaweza ukachunguza na kuangalia ni watu gani wanaokuzunguka sasa katika maisha yako. Kama wengi ni hasi tambua kuwa kabisa na wewe upo kwenye njia hiyohiyo. Watu wanaokuzunguka ni njia mojawapo inayoweza kukupelekea wewe kuwa na fikra hasi katika maisha yako.

Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.

TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO,

IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,
                         

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: