Kama Unaweza Kufanya Kazi Yoyote, Hakuna Anayeweza Kukuajiri. Na Njia Bora Ya Kupata Kazi Unayotaka.

Huwa napokea ujumbe mwingi sana kwa siku. Ujumbe huwa kwa njia ya email na hata njia ya simu. Huwa najitahidi kutenga muda wa kusoma ujumbe ninaotumiwa na kujibu kama inanihitaji kufanya hivyo. Inachukua muda, lakini inanibidi nifanye kwa sababu ni moja ya sehemu za kazi hii ya kuwawezesha watu kuchukua hatua ya kuboresha maisha yao.

Katika jumbe nyingi ninazopokea kila siku kuna ujumbe umekuwa unajirudia rudia mara nyingi. Nimekuwa nikijaribu kuwaelewesha watu wanaonitumia ujumbe huo lakini bado naona wengine wanaendelea kutuma. Sasa leo tutajadili aina hii ya ujumbe na ni hatua gani mtu achukue ili kuweza kuboresha maisha yake na kufikia mafanikio.

SOMA; Huyu Ndio Mtu Pekee Anayeweza Kukunyanyasa.

Ujumbe wenyewe huja hivi; Naomba unipe kazi. Mara nyingine huwa na maelezo mengi marefu ya kujieleza ila lengo kubwa la ujumbe ni kuomba kazi. Na mimi najibu ujumbe huu kwa kumuuliza mtumaji; Ni kazi gani unataka? Baadae mtumaji hunijibu kwa kusema; Kazi yoyote utakayonipa nitafanya. Sasa hapa ndio changamoto inapoanzia na ndipo ninapoanza kuwashauri watu japo kwa ufupi. Leo hapa tutalijadili hili kw aurefu kidogo na tuone ni hatua gani unaweza kuchukua ili na wewe usiishie kwenye hali kama hiyo.

Kabla hatujaenda mbali kwenye makala hii, naomba tuite jembe kwa jina lake jembe na hapa nataka kusema kwamba KAMA UNAWEZA KUFANYA KAZI YOYOTE, MAANA YAKE HAKUNA KAZI UNAYOWEZA KUIFANYA.

Kama unafikiri kazi yoyote itakayotokea mbele yako unaweza kuifanya, basi hakuna kazi unayoweza kuifanya kwa ubora wa hali ya juu na hivyo huwezi kuleta matokeo mazuri. Hakuna mtu mwenye uhitaji w akukuza biashara yake atakayeajiri mtu ambaye anaweza kufanya kazi yoyote. Na wale wanaoajiri watu wa aina hiyo hujikuta kwneye matatizo makubwa sana kwa kuwa na wafanyakazi ambao hawawezi kutekeleza majukumu yao na hivyo kuwa mzigo.

Unaposema unaweza kufanya kazi yoyote maana yake unasema unaweza kugusa kitu chochote kinachopita mbele yako, kitu ambacho mtu yeyote anaweza kufanya hivyo.

SOMA; Sifa Sita(6) Unazohitaji Ili Kuwa Mjasiriamali Bora.

Vijana wengi wa kitanzania wamekuwa wakikosa kazi nzuri kutokana na kushindwa kujua ni kazi gani wanayoweza kuifanya kwa ubora wa hali ya juu. Hata kama umewahi kufanya mambo mengi, bado haikufanyi wewe kuwa mzuri wkenye kila kazi. Kuna kazi chache ambazo unaweza kuzifanya vizuri na zikaleta mabadiliko makubw akwneye taasisi unayoifanyia kazi. Na kama unakwenda kwenye usaili wa kazi, kuwa makini sana usije kuropoka neno kama hilo kwmaba unaweza kufanya kazi yoyote, utawafanya wanaokusaili waanze kuwa na mashaka na wewe kama kweli una kitu cha tofauti cha kufanya au unataka tu kazi.

Hali hii ya kutaka kufanya chochote haipo tu kwenye kazi, hata kwenye biashara mambo ni hayo hayo. Mtu anakuandikia ujumbe kwamba nataka kufanya biashara, naomba unishauri. Unamuuliza ni biashara gani unataka kufanya, anakujibu biashara yoyote ambayo itanipa faida, yaani hili ni kosa kubwa kuliko hata hilo la kazi, naomba tusizungumzie leo, ila nitaliandikia siku nyingine ili tulichambue vizuri na kuona ni kitu gani mtu unaweza kufanya.

Ufanyeje ili uweze kupata kazi kwa mtu yeyote unayemuomba?

Kwa mfano mtu angeniandikia kwamba mimi ni msomaji wa blog zako mbalimbali, nilikuwa nafikiria makala zako nzuri hazijawafikia watanzania wengi ambao zinaweza kuwasaidia, nimekuja na njia nzuri ambayo ukiitumia makala zako zitawafikia watu wengi zaidi. Hapa nitakuwa tayari kusikiliza na hata kama ni kazi nitatoa. Hii ni kwa sababu mtu huyu anajua ni kitu gani ambacho kinakosekana na tayari amekuja na jibu. Hivyo hata ukimpa kazi atawajibika vizuri kwenye majukumu yake na hivyo kuongeza thamani.

Kama unataka kupata kazi yoyote, kwanza jua ni kitu gani unachoweza kukifanya vizuri. Kinaweza kuwa kimoja, vinaweza kuwa viwili au vitatu, ila haiwezi kuwa kila kitu. Baada ya kujua ni nini unaweza kufanya vizuri, jua ni mtu gani anaweza kunufaika na kile unachoweza kufanya vizuri. Ukishamjua mtu huyu, jua kile anachofanya na jua mapungufu yake au changamoto anazopitia.

Mwandikie mtu huyu ukijieleza wewe ni nani, unaweza kufanya nini na ni changamoto gani unaziona kwake ambapo anaweza kunufaika na kile unachoweza kufanya. Pia unaweza kumpendekezea kwamba akupe nafasi umuoneshe ni kitu gani utafanya na kama ataona kitakuwa cha thamani kwake ndio akulipe.

Kama utafanya hivi na kutoa thamani ya kweli hakuna mtu atakayekataa kukulipa na atapenda kuendelea kuwa na wewe. Na hata kama mtu huyo atashindwa kuona mchango wako mzuri bado utaondoka na somo kubwa ambalo unaweza kulitumia kwa mtu mwingine utakayemuonesha ni kipi unaweza kumsaidia. Ukifanya hivi kwa watu kadhaa, utapata mtu mmoja ambaye atakupa nafasi nzuri na wewe utampa faida kubwa. Ukiambiwa hapana usiishie hapo, nend akwa mwingine tena na tena na tena.

SOMA; Fanya Mambo Haya Matatu Na Usipokuwa Tajiri Ndani ya miaka 10, sahau kuhusu utajiri kwenye maisha yako.

Tanzania kuna tatizo la ajira, halafu wakati huo huo kuna tatizo la wafanyakazi. Yaani kuna watu wengi hawana ajira na wakati huo huo kuna nafasi nyingi za kazi lakini hakuna wa kuzichukua. Hii yote inaletwa na watu kusubiri mpaka waambiwe tumetangaza nafasi za kazi ndio waombe.

Wewe achana na kundi hili kubwa, kupata nafasi nafasi ya kazi kwenye nafasi 70 zinazogombaniwa na watu elfu 10 ni vigumu sana. Ila ukitumia njia hii tuliyojadili hapa, ukiwaandikia watu 10, watatu watakuita na mmoja anaweza kujaribu kufanya kazi na wewe. Ukiwaandikia watu 100 utakuw akwneye nafasi nzuri zaidi.

Anza leo, orodhesha majina ya kampuni zote ambazo unaweza kuzifanyia kazi na jua ni kitu gani unachoweza kukifanya kwa tofauti, tafuta mawasiliano ya wahusika na kisha waandikie. Au kama unaweza kuonana nao uso kwa uso inakuwa bora zaidi.

Je utalifanyia hili kazi? Au utaendelea kukaa na kulalamika ajira hakuna? Maisha ni yako na uchaguzi ni wako.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kuboresha maisha yako ili uweze kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz 

kitabu-kava-tangazo4322

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s