Hata kama watasema akina nani, bado ukweli unabaki kuwa uleule kwamba, fedha haziwezi kutupa sisi furaha kubwa katika maisha yetu kama tunavyofikiri. Lakini si pesa tu peke yake, hata pia vile vitu tunavyovitaka ambavyo huwa hatunavyo na tunadhani vile vitu tunavyovitaka vitatufanya tuwe na furaha, navyo pia kwa bahati mbaya huwa havina uwezo wa kutupa furaha ya kweli kama tunavyotegemea.

 
Wasomi wa nyanja mbalimbali za maarifa wanasema kwamba, hakuna uhusiano kati ya furaha ya kweli na vitu tunavyovitaka maishani. Hata pia wanazuoni wa uchumi, saikolojia na wanasayansi ya jamii, ambao wamefanya tafiti kubwa na za muda mrefu wamethibitisha hili kuwa, vile vitu ambavyo huwa tunadhani vinaweza kutupa furaha, havina uwezo huo wa kutupa furaha halisi.
Katika kutafuta furaha hii wengi wetu hujikuta wakinunua hiki ama kile kwa kutumia pesa walizonazo. Yote hayo hutokea kwa sababu ya kutafuta furaha ya kweli. Lakini hata hivyo pesa hiyo inapokesekana wengi hukosa furaha. Kwanini unafikiri iko hivi? Hii ni kwa sababu fikra zao huweza kufikiri pesa ni kila kitu, bila pesa mambo yote yatakuwa magumu sana na hawawezi kuwa na furaha kamili.
Kwa kadri, watu wanavyoitafuta furaha ya kweli kutoka kwenye vitu vinavyowazunguka, ndivyo ambavyo inawaponyoka zaidi. Ni ujinga mtu kudhani kipande cha karatasi au sarafu kinaweza kumpa furaha ya kweli. Labda kinachoweza kumpa mtu furaha ni hisia za uhakika na usalama. Huu uhakika na usalama upo kwa kila mtu, bali tunashindwa tu kuutumia. 

 Ni ujinga unaoufanya tuamini kwamba, kipande cha karatasi kiitwacho noti au bati, kiitwacho sarafu, vinaweza kutufanya tuwe na furaha ya kweli. Fedha inachoweza kufanya kwako ni kukupa usalama wa nje na kukuongezea nguvu ambayo inaletwa na fedha. Hii haitoshi kuhesabiwa kuwa ni furaha, kwa sababu siku inategemea tuna fedha kiasi gani.

Kwa kawaida furaha halisi ambayo pengine unaweza ukawa unaitafuta sana kutoka nje yako, ipo na inatoka ndani mwako. Sio pesa, ama vitu unavyovitafuta sana ndivyo vitakavyokupa furaha ya kweli. Mambo mengi unayoyahangaikia ukija kuyapata utagundua kuwa, yatakupa furaha ya muda tu na siyo ya kudumu sana kama ulivyokuwa ukifikiri mwanzo. Bila shaka umewahi kuwaona watu ambao wana pesa nyingi lakini, maisha yao yanaonekana hayana furaha.
Ninachotaka kukwambia hapa sio na maanisha usitafute pesa kwa bidii, ama kutafuta maisha kwa bidii, HAPANA. Ninataka ujue katika harakati zako hizo ulizonazo za maisha jifunze kujenga na furaha kwanza kutoka ndani mwako wewe. Kwa kufanya hivyo, utatafuta pesa na utajiri huku ukiwa na amani. Lakini ukiwa tu unawaza, pesa na vitu vinginevyo ndiyo msingi wako wa furaha, utakuwa unajidanganya mwenyewe.  
Furaha au hali halisi ya kuhisi ukamilifu unaijenga mwenyewe ndani yako. Kwa mfano unaweza ukaona maisha ya watu wengine, ambao wewe kwa nje huwa unayaona maisha yao ni duni na magumu sana. Lakini kitu cha kushangaza watu hao huwa ukiwaona pia wakifurahia maisha yao kama yalivyo na kuamini katika kuwa kwao hivyo.
Hivyo basi, hiyo yote inatuonyesha kuwa maendeleo ya kichumi na pato la mtu, haviwezi kuwa vigezo vya kupima furaha ya kweli aliyonayo mtu. Kitendo cha kuhusisha pato na furaha ni uongo, kama ulikuwa hujui kitu kama hicho.
Kama kweli mtu anataka furaha ya kweli, hana haja ya kujidanganya kwamba, akipata fedha, kujenga nyumba nzuri au kununua gari ya aina fulani ndipo atakapoipata furaha hiyo. Anza kuamini kwamba unapaswa kujifunza kujua furaha iko wapi ndani mwako, badala ya kuitafutia kwenye magari ama vitu vingine ambavyo vitakuumiza kichwa tu.
Kwa makala nyigine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako. 
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.
TUPO PAMOJA,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,