Kuanzia tumekuwa na kipengele cha USHAURI WA CHANGAMOTO zinazokuzuia kufikia mafanikio, ni zaidi ya mwaka mmoja sasa. Kwa mwaka huu mzima karibu kila wiki umekuwa unapata makala moja yenye ushauri mzuri kuhusiana na jambo ambalo limeulizwa. Kwa muda huu wa zaidi ya mwaka mmoja, kikubwa tulichojifunza ni kwamba changamoto nyingi zinazowazuia wengi kufikia mafanikio ni zile zile na zinajirudia sana. Baadhi ya changamoto hizo ni; ukosefu wa mtaji, kipato kidogo ukilinganisha na matumizi, idadi kubwa ya wategemezi na biashara gani ya kufanya.
Leo makala hii ya kipengele cha ushauri wa changamoto tutaangalia jinsi ya kupata ushauri bora na utakaoiwezesha biashara yako kukua na wewe kufikia mafanikio makubwa.
Kuna kitu kimoja kikubwa sana nataka nikuambie kuhusu ushauri, hasa hapa kwetu Tanzania, ushauri ni kitu ambacho ni rahisi sana kufanya. Na mtu yeyote, bila ya kujali uelewa wake wakati wowote na katika mazingira yoyote anaweza kutoa ushauri. Sema unataka kufanya biashara ya maembe, kila utakayemuambia atakushauri, yaani hata mtu ambaye hajui hata maembe yanapatikana wapi, au hata biashara inaendeshwaje anaweza akakushauri kwa uhakika kabisa. Unakuta mtu huyu naye alisikia watu wanaongea kuhusu biashara ya maembe na hivyo kutoka na kitu cha kuweza kutoa pale jambo lolote kuhusu maembe linatajwa.
Kwa maana hii basi, ushauri mwingi ambao unaupata huko mitaani kuhusu biashara unayofanya au unayotaka kufanya ni ushauri wa hovyo na ambao hutakiwi kuufuata hata kidogo. Kama hutasikia hili unaweza kujaribu na kuona jinsi utakavyojiingiza kwenye changamoto kubwa zaidi. Watu wengi ambao nimekuwa nawasiliana nao na kutaka ushauri wa biashara huwa wanakuwa wameingia kwenye mtego huu wa kuchukua ushauri maarufu na kuufanyia kazi.
Hali hii ya ushauri kupatikana kirahisi mtaani pia imeharibu sana watu wengi. Huwa napata simu na jumbe nyingi kutoka kwa watu ambao wanakuwa wanahitaji ushauri wa kibiashara. Na mtu huyo huwa anategemea kupata majibu ya changamoto yake na ushauri wa kibiashara kupitia ujumbe wa simu au kwa kujibu pale pale tunapozungumza na simu. Pia kupatikana huku kwa ushauri kiurahisi, watu hawajaweka thamani kabisa kwenye kupata ushauri mzuri. Mtu akiambiwa alipie ili kupewa ushauri anaona haiingii akilini kwa sababu akipiga hatua chache tu anaweza kukutana na watu wengi ambao watamshauri bure kabisa. Hali hii imekuwa ikiwazuia watu kupata ushauri bora ambao utawezesha biashara zao kukua.
Unawezaje kupata ushauri bora utakaokuwezesha kufanikiwa kwenye biashara?
Kwa sababu sehemu kubwa ya ushauri unaoupata mtaani sio wa kuaminika, unahitaji kuwa makini sana ili kuweza kupata ushauri bora na utakaokuwezesha wewe kufikia malengo yako kwenye biashara. Ili kupata ushauri bora unaoweza kuisaidia biashara yako kukua, unahitaji kuzingatia mambo haya mawili.
1.     Ushauri bora unahitaji muda.
Hakuna kitu cha kufanyiwa haraka na biashara yako ikabadilika na kuwa nzuri. Watu wengi wamekuwa wakifikiri kwamba kuna muujiza ambao unaweza kufanyika kwa muda mfupi na biashara ikabadilika kabisa. Yaani mtu amekuwepo kwenye biashara kwa miaka mingi, amekuwa anafanya makosa mengi ambayo yameifanya biashara kuingia kwenye changamoto, ila anataka ndani ya dakika tano apate jawabu la matatizo ya biashara yake. Hiki ni kitu ambacho hakiwezekani, na ushahidi kwamba hakiwezekani ni kuangalia wafanyabiashara wengi. Pamoja na ushauri wote unaopatikana kwa urahisi sana lakini bado watu wengi wanapitia changamoto kubwa. Hii ni kwa sababu hakuna dawa ya haraka kwenye kuokoa biashara yako. Na hata kama unataka kuingia kwenye biashara bado hakuna dawa ya haraka ya kukuwezesha wewe kuingia kwenye biashara na kufanikiwa haraka.
Kwenye AMKA CONSULTANTS tunachofanya sio kutoa huduma ya ushauri wa haraka kama ambavyo mtu anataka au alivyozoea bali kumpatia mtu huduma ya ushauri ambayo itamfaa kwa hali ambayo anapitia sasa kwenye biashara yake au kwa jinsi anavyoweza kuingia kwenye biashara na kufanya vizuri. Unapokwenda kwa daktari unategemea akusikilize, akupime na ndio akupe dawa. Utakosa imani na daktari kama unapofika tu na kumwambia kichwa kinauma basi anakuandikia dawa na kukuambia katumie hizi. Hivi ndivyo ilivyo kwenye ushauri wa biashara pia. Unahitaji kupewa muda w akusikilizwa, kujua ni changamoto gani unapitia na kupimwa mtazamo ulionao kwenye biashara na ni kwakiasi gani umejitoa na baada ya yote haya ndio ushauriwe.
Ukinipigia simu kwa ushauri wa kibiashara, tunahitaji muda usiopungua saa moja wa mazungumzo na kukuuliza maswali kabla sijatoa ushauri wowote utakaoweza kukufaa kwenye biashara yako.
2.     Ushauri bora una gharama.
Ukipiga simu na kuuliza unataka kufanya biashara ya maembe. Na mimi nikakwambia sawa, ni biashara nzuri, nenda sokoni, nunua maembe kwa bei ya jumla, yapeleke kwenye eneo lako la biashara na ongeza bei kidogo ili upate faida na anza kufanya biashara. Utaridhika na ushauri wa aina hii? Nina uhakika huwezi kuridhika, kwa sababu hakuna kitu kipya nimekuambia, vyote ulikuwa unavijua na umeona watu wengi wakifanya hivyo ila bado wana changamoto kwenye biashara zao. Hiki ndio kinachofanyika kila siku kwa sababu unapenda ushauri wa bure. Ushauri wa bure hauhitaji mtu afikirie, hauhitaji mtu ajiweke kwenye nafasi yako, na kuichukulia hali yako kama yake na kisha kufanya maamuzi ambayo yupo tayari kwenda nayo. Ushauri wa bure ni kuropoka tu kile ambacho mtu anajisikia kusema na ambacho mtu atapenda kusikia. Ushauri wa aina hii hauwezi kukusaidia hata kidogo.
Kwenye AMKA CONSULTANTS, tunatoa ushauri ambao unaendana na mtu kwa mazingira yake na hali anayopitia. Hakuna ushauri mmoja unaoweza kuwafaa watu wawili tofauti. Kama ulivyoona hapo juu inahitajika sio chini ya saa moja ya kuwana mazungumzo ambayo ndio yatatumika kutoa ushauri. Hivyo ili kupata kilicho bora, unahitaji kukigharamia. Hivyo unapopiga simu kutaka ushauri wa biashara kutoka kwangu, jiandae kabisa kulipia gharama za ushauri. Najua huu sio utamaduni ambao watu wamezoea, ila unahitaji kuufuata kama unahitaji ushauri ulio bora. Watu wengi wamekuwa wakitaka ushauri ila unapowaambia wachangie gharama hupotea kabisa na huwasikii tena.
Mtu mmoja amewahi kuniambia biashara yangu inakufa, halafu bado unataka nikupe fedha ndio unishauri. Nilimjibu kama unaona kuchangia gharama ndogo za ushauri ni changamoto sana kwako, subiri biashara yako itakapokufa kabisa na utaona jinsi ilivyo ngumu kuanza biashara mpya. Hakuna kitu kizuri ambacho hakina gharama katika maisha. Hata kama unaanza biashara, unahitaji uwe umejitoa sana ili kuweza kuwa tayari kuchangia gharama na kupata ushauri ambao ni bora kwako.
Karibu sana upate ushauri bora utakaoiwezesha biashara yako kukua na kuondokana na changamoto. Au kama ndio unataka kuingia kwenye biashara basi utapata ushauri wa biashara gani unaweza kufanya na ikaleta tija kwako na kwa wanaokuzunguka. Kumbuka hiki sio kitu kinachofanyika kwa dakika tano na kuna gharama unahitaji kuingia ili kupata ushauri ulio bora.
Nakutakia kila la kheri katika mafanikio ya biashara yako.
TUPO PAMOJA
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tzau simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.