Habari za leo mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA, karibu tena kwenye kipengele hiki cha USHAURI WA CHANGAMOTO zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa tunayotazamia kwenye maisha. Ukweli ni kwamba changamoto ni nyingi sana na mtu usipojipanga vizuri ni rahisi sana kukata tamaa.
Leo katika kipengele hiki tutajadili mambo muhimu yakufanya pale ndugu zako wa karibu wanaposhindwa kukuelewa au wanapokuona wewe ni mbaya. Nimekuwa nikiandika mara nyingi kwamba utakapoanza kufanya haya mambo ambayo unajifunza hapa, watu wengi hawatakuelewa. Hawatakuelewa kwa sababu wamezoea kwenye jamii kila mtu anafanya kitu ambacho wenzake wote wanafanya, sasa wewe unapokataa kufuata kundi na kukimbia mbio zako mwenyewe hawaelezi na wengine hawaamini kama inawezekana.
Unahitaji kuwa na mbinu nzuri za kuweza kukabiliana na changamoto hii vinginevyo unaweza kukata tamaa kwa kiasi kikubwa sana. Kabla hatujaangalia ni mambo gani muhimu ya kufanya unapokuwa kwenye hali hiyo, tupate maoni kutoka kwa msomaji mwenzetu anayepitia hali hii.

Habari Amani, Asante kwa makala nzuri unazotupatia. Kuna changamoto mmoja ambayo nafikiri kila mtu anayeamua kubadili na kuboresha maisha yake huwa anaipitia. Changamoto hii imekua ikinisumbua sana. Changamoto yenyewe ni hii; Unapoamua kufanya maisha yako yawe ya tofauti, watu hawatakuelewa au watakuelewa vibaya, watakutafsiri vibaya. Sehemu kubwa ya watu watasema unatumia njia za giza(uchawi), wengine watasema unawatoa watu kafara ndio maana unafanikiwa. Mtu wako wa karibu anapofariki watasema ni wewe umemtoa kafara. Nina ndugu yangu aliwahi kuniambia, huwa ananiona usiku akiwa usingizini nikimsumbua kwa mapepo(kumtoa uhai wake). Alinipeleka kwa uongozi wa ukoo wanilaani nife mapema kama natumia uchawi. Kuna maneno mengi hapa ila nafikiri umeshanielewa. Sasa naomba msaada wa majibu kwa maswali haya; i) Ni nini kinawafanya watu wakutafsiri vibaya? ii) Ni nini kinawafanya ndugu zako wa karibu ndio wanakuwa mstari wa mbele kukusakama ili hali hamna chuki? iii) kwa nini watu hawa hawajitengi na kukuacha japo hawakubaliani na mafanikio yako? iv) Kwa nini ndugu zako hawa wanahitaji msaada wako wa karibu kila wanapokuwa kwenye shida? V) Ni hatua gani uchukue kuwafanya watu hawa wakuelewe?

Kama tulivyoona kwa msomaji mwenzetu hapo juu, ndugu wanaweza kuwa kikwazo kikubwa sana kwako kufikia mafanikio. Wakati wewe unakazana kufanya kazi usiku na mchana ili uendelee, wao wanakesha usiku na mchana kuhakikisha huendelei, unabaki kama wao. Hii ni nguvu kubwa sana ambayo inahitaji maarifa makubwa kuweza kuishinda. Naomba tuende kwa kujibu swali moja moja kama alivyouliza msomaji mwenzetu.
1. Ni nini kinawafanya watu wakutafsiri vibaya?
Kinachowafanya watu wakutafsiri vibaya ni kwa sababu hawajawahi kuona mambo unayofanya yakifanyika. Najua msomaji aliyeomba ushauri huu ni msomaji na mfuatiliaji mzuri wa AMKA MTANZANIA kwa muda mrefu. Amekuwa anajifunza vitu vingi sana na kuvifanyia kazi. Sasa kila anayefanyia kazi vitu hivi anakuwa tofauti kabisa. Wale wanaokuzunguka wanakuwa hawajazoea kuona watu wakiboresha maisha yao wenyewe na kupata mafanikio. Wamezoea watu mnakaa pamoja, mnalalamika, mnapoteza muda, hamuweki ubora kwenye kazi zenu, mkipata fedha mnatumia yote bila ya kuweka akiba na mengine mengi.
Sasa wewe unapoanza kuacha kufanya mambo hayo ambayo walizoea kukuona unafanya, lazima wastuke, lazima wakuelewe vibaya. Na kwa sababu uelewa wao ni mdogo (kwa sababu hawajapata mafunzo haya mazuri unayopata wewe) watasema umeacha kufanya mambo uliyokuwa unafanya zamani kwa sababu umepewa masharti na mganga.
SOMA; Kama Unataka Kumaliza Matatizo Yako Ya Fedha Fanya Kitu Hiki Kimoja.
2. Ni nini kinawafanya ndugu zako wa karibu ndio wanakuwa mstari wa mbele kukusakama ili hali hamna chuki?
Ndugu zako wa karibu ndio wanaofikiri wanakujua vizuri, ndio wanaosema walikuona tangu unakua, ndio wanaofikiri huwezi kubadilika kwa sababu walishakuambia wewe hutaweza kufanya kitu kingine kikubwa. Sasa wanapokuona ghafla unafanya mambo ambayo hawakutegemea ungeweza, wanakuwa mstari wa mbele kukusakama na kuamini kwamba unatumia nguvu za kichawi.
Pia elewa kwamba jamii zetu nyingi zinaamini sana kwenye uchawi, japo ni kitu ambacho hakipo lakini wengi wamejijengea imani kubwa. Na kwa imani hii watu wameaminishwa kwamba mtu anapotumia nguvu za kichawi, huanza kwa kuwaua ndugu zake wa karibu. Hivyo wanachanganya woga wao na imani zao na kukuona wewe sio mtu mzuri.
3. Kwa nini watu hawa hawajitengi na kukuacha japo hawakubaliani na mafanikio yako?
Hawawezi kujitenga na kukuacha kwa sababu wewe umeshakuwa tishio kwao. Labda fikiria wewe ni kijana ambaye huna uzoefu mkubwa na wala hukubahatika kuridhi sehemu kubwa ya mali. Wewe binafsi ukaweka juhudi kubwa sana na ukaanza kuona mafanikio makubwa na wakati huo huo ukaanza kuwazidi hawa watu waliokutangulia umri. Jambo hili hawatalifurahia. Watanzania wengi hujiridhisha wanapopata mafanikio kidogo na kujiona wao ndio wao. Wanapokuona wewe una njaa ya mafanikio hasa na huridhiki na mafanikio kidogo, wanaona sio bure, kuna kitu unatumia.
Watu hawa hawawezi kukuacha kwa sababu wanaona unakuwa tishio kwao.
4. Kwa nini ndugu zako hawa wanahitaji msaada wako wa karibu kila wanapokuwa kwenye shida?
Ni utamaduni wa kawaida kwa maisha yetu ya Kitanzania kwamba mtu ambaye ana mafanikio kidogo kwenye familia au ukoo ndio watu wote wanaweka macho yao pale. Tatizo dogo likitoke akila mtu anakuangalia wewe. Na hata ukitoa kiasi gani bado kuna wengi wanaona ungeweza kutoa zaidi.
Kwa kifupi kuwa na mafanikio kwenye mazingira ya Kitanzania kunaweza kuwa mzigo mkubwa kwako. Wewe umeshajipanga kwamba unapunguza matumizi yako sana ili uweze kuwekeza na kuzalisha zaidi kipato chako. Wenzako wanafikiria wewe una fedha nyingi sana hivyo kuwasaidia ni jukumu lako. Sasa utakapowaambia kwamba huna uwezo wa kuwasaidia kwenye vitu fulani ndio hawakuelewi kabisa na wanazidi kuona kwamba fedha zako ni za masharti na wewe ni mtu mbaya.
SOMA; Mtazamo Wa Kuvuna Na Mtazamo Wa Kujenga.
5. Ni hatua gani uchukue kuwafanya watu hawa wakuelewe?
Natamani ningeweza kukuambia ni hatua gani uchukue lakini hatua hizi zinaweza zisizae matunda. Kwa sababu tatizo hili linasababishwa na ujinga na hivyo kikubwa ni kuwaelewesha ndugu zako. Ila kama hawapo tayari kujifunza wanaweza pia wasikuelewe.
Yafuatayo ni mambo muhimu unayoweza kufanya pale ambapo ndugu zako hawakuelewi au wanakuelewa vibaya.
a. Waelewe kwamba ni watu ambao wanatamani wangekuwa na mafanikio kama yako ila hawajui kwamba inawezekana kuwa na mafanikio hayo bila ya kutumia uchawi. Elewa kwamba wao wamekubaliana na jamii inavyowaambia waishi na ndio maana maisha yao yanazidi kuwa magumu.
b. Waeleweshe kwamba mafanikio yanawezekana kwa kila mtu. Waambie hakuna mtu alizaliwa ili awe masikini tu, waambie hata wao kama wakitaka kubadilika wanaweza kuboresha maisha yao kama ya kwako yalivyokuwa bora.
c. Wasipokuelewa wapuuze na endelea kuweka juhudi. Kwa nafasi kubwa utakavyojaribu kuwaambia kwamba inawezekana wao kuboresha maisha yao hawatakuelewa. Sasa wewe usipoteze muda wako kuendelea kupiga nao kelele, achana nao, waache waendelee kusema na wewe weka juhudi. Wakati wao wanapiga mdomo wewe piga kazi. Wakiendelea kukuwekea vikao waambie wazi kwamba huhusiki na mambo hayo ya uchawi na hata kama ni wazee wa ukoo waambie vizuri kwamba dunia imebadilika na kila kitu kinawezekana. Ukiona bado hawakuelewi na wanaendelea kukuwekea vikao, usiende kwenye vikao hivyo. Ni kupoteza muda na kutaanza kukurudisha nyuma.
d. Waambie wasome AMKA MTANZANIA. Kitu cha mwisho kabisa unaweza kuwasaidia hawa ndugu zako ni kuwaambia wasome AMKA MTANZANIA, wasisitize wasome na waambie waanze kufanyia kazi yale ambayo wanajifunza. Tena kwa kuanza waambie wasome eneo hili la UHUSIANO KATI YA MAFANIKIO NA UCHAWI, ukibonyeza hayo maandishi utakutana na makala zinazoeleza kwa nini watu wanaamini uchawi unaleta mafanikio na kwa nini sio kweli. Na ni jinsi gani yakupata mafanikio makubwa bila hata ya kutumia uchawi. Yote yako kwenye makala hizo. Hata kama hawana simu za kuweza kuingia kwenye mtandao, nenda kachape makala hizo(ZIPO NNE) na wape wazisome, kuna wengi watabadilika.
e. Mwisho kabisa nikuambie kwamba unapoona watu hawakuelewi, unapoona watu wanakuchukia bila sababu jua kwamba umeanza kuwa tofauti na wao. Na hapa jipe hongera kwa sababu umeweza kuishinda nguvu kubwa inayokulazimisha wewe uwe kama kila mtu kwenye jamii yako. Hata litokee jambo gani, nakusihi na kukusisitiza sana usikubali kurudi nyuma. Hata kama watakutishia kukuondoa kwenye ukoo, usirudi nyuma, wengi hawakuelewi sasa lakini watakuja kukuelewa baadae. Unapokuwa masikini kila mtu anakudharau, hata kwenye huo ukoo wanaokuona wewe ni ndugu yao sana wanakuona sio wa maana. Unapokuwa na mafanikio kila mtu anataka umuone yeye ni wa muhimu na watataka kila wanachokuambia ufanye, ufanye. Usikubali kuburuzwa kiasi hiki, tunaishi kwenye dunia yenye uhuru mkubwa, unapaswa kufanya kitu ambacho unafurahia na watu ndio wakuelewe kwa hivyo. Na sio kulazimishwa kufanya vitu kwa sababu tu watu ndio wanataka wewe ufanye.
Nakutakia kila la kheri kwenye safari yako ya kuboresha maisha yako. Ni safari ngumu sio tu kwa wewe kuweka juhudi, bali hata kwa wanaokuzunguka watakuwa kikwazo. Fanyia kazi hayo tuliyojifunza na yatakusaidia sana.
TUPO PAMOJA
Makirita Amani 
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

http://www.amkamtanzania.com/p/kuwa-tajiri.html