Daima namshukuru mungu kwa namna ambavyo amekuwa akinipa pumzi pasipo malipo, Baraka hizi ndizo zinazonisukuma niweze kuwatazama wengine kama sehemu yangu ya maisha hapa duniani. Ndugu Mtanzania mwenzangu ambaye umekuwa ukitumia muda mwingi kufikiri namna gani utatoka hapo ulipo na kuweza kufikia ndoto zako, usikate tamaa endelea kusonga mbele kwa kuwa unajua unakoenenda, ni furaha isiyo kifani ikiwa unasafiri na unajua unakokwenda na unatambua lengo la safari hiyo ni nini. Leo naungana na wale wote ambao lengo lao ni uwekezaji katika ardhi na majengo. Napenda kukushirikisha ili upate njia rahisi ya wewe kufikia malengo kwa njia ya ardhi au majengo kwa kuwa nimekuwa katika sekta hii kwa muda na nimewasaidia wengi katika hili.
Kwa nini uwekeze kwenye ardhi na majengo
Katika Tanzania hali ya sasa ni rahisi kwa uwekezaji huu lakini inazidi kuwa ngumu katika siku zijazo kutokana na maendeleo ya kiuchumi na kisiasa, ndiyo; uwekezaji wowote ule hutegemea hali ya uchumi ikiambatana na sheria, sera na taratibu za wakati huo. Idadi ya watu inaongezeka kwa kasi sana tofauti na miaka iliyopita, hivyo ongezeko hilo huenda sambamba na mahitaji ya kibinadamu kama vile makazi na huduma mbalimbali za kijamii, mahitaji hayo hufanyika kwenye ardhi na majengo, hivyo hali ya sasa inahitaji sana ardhi na majengo kwa matumizi mbalimbali nchini kote iwe mijini au vijijini, hali hii ya uhitaji husababisha gharama ya ardhi kupanda kwa haraka sana kwa kuwa bidhaa hiyo ni adimu na ina ukomo (ardhi haiongezeki wala haizalishwi).
SOMA; Njia Kumu(10) Za Kupata Utajiri Na Mafanikio.
Inasikitisha kuona mtanzania anayetaka kujikwamua kiuchumi anakuwa mpangaji kwenye nyumba ya kuishi na hata kwenye ofisi za biashara zake. Wengi Hujikuta wakiyumba pale gharama hizo zinapobadilika mara kwa mara kutoka kwa wamiliki kutokana na uhitaji mkubwa wa makazi na ofisi za biashara. Pia wengi huyumba kibiashara kutokana na kuhamahama kwa ofisi jambo ambalo huwa usumbufu kwa wateja. Amua kumiliki ardhi, amua sasa kujenga ili umiliki ofisi za biashara zako au makazi na kuwapangisha wengine.

 
Fursa zilizopo kwenye ardhi na majengo
Udalali wa nyumba na viwanja
Haijalishi upo wapi na upo katika hali gani ya uchumi kazi hii unaweza kuifanya, uwe mjini au kijijini pia unaweza fanya endapo utaamua kutenda kwa uadilifu. Unaweza kuwa dalali wa viwanja, mashamba na nyumba kwa kununua au kupangishwa, hapa dalali unajipatia fedha kwa kazi ya kuwaunganisha mteja na mwenye mali, kazi kubwa hapa ya dalali ni kuitangaza bidhaa hiyo kwa makubaliano ya mwenye mali na mteja kulingana na hitaji husika. Fungua ofisi yako na uisajili kwa mamlaka husika ili upate fursa kubwa zaidi na hata ufanye kazi na makampuni ya ndani na nje ya nchi yanayohitaji huduma hii. Usifanye kazi hii kwa ubabaishaji bali kwa weledi na ndipo utakapoona mafanikio yako.
Ununuaji na uuzaji wa viwanja na majengo
Katika njia hii unaweza kununua ardhi au nyumba kwa bei rahisi baada ya kufanya marekebisho kadhaa unaweza kuiuza kwa gharama ya juu zaidi tofauti na ulivyonunua. Kwa wale waliopo vijijini wanaweza kununua mashamba/mapori na kuyaongezea thamani/kuyasajili kulingana na eneo husika baada ya miezi au miaka kadhaa unaweza kuuza kwa thamani kubwa zaidi tofauti na ulivyo nunua na huu ndiyo uwekezaji unaolipa zaidi. Watu wengi wamenufaika sana kwa uwekezaji huu na hata wameweza kufanya makubwa zaidi ya walivyotarajia.
SOMA; Hivi ndivyo unavyoweza kununua Hisa katika soko la Hisa la Dar es salaam (DSE)
Kuongeza thamani za viwanja na majengo
Kwa bahati ni watanzania wachache sana wanaoifahamu njia hii ya uwekezaji, miongoni mwa watanzania wachache niliokutana nao walijilaumu sana kuwa wamechelelewa kupata wazo hili na eti wamechelewesha mafanikio yao. Napenda nikueleze msomaji wa makala hii kuwa hujachelewa na wala hujawahi, amua sasa kuwekeza. Katika njia hii unaweza kununua shamba ukaliwekea miundombinu ya kilimo cha aina fulani ya kuboresha shamba hilo baadae ukalikodisha kwa wahitaji wa aina hiyo ya miundombinu uliyoiweka, pia unaweza kununua kiwanja ukaweka miundombinu ya uwekezaji wa aina fulani ili kuvutia wawekezaji wengine katika ardhi hiyo, pia unaweza nunua nyumba kwa bei rahisi ukaiboresha au ukaibadili matumizi kulingana na hali ya uhitaji wa mahali husika. Katika njia hii ya uwekezaji ukishaongeza thamani ya mali yako unaweza kuikodisha au kuiuza kwa wahitaji au wawekezaji wengine. Kwa njia hii watu wengi wameingia ubia na makampuni makubwa hasa taasisi za fedha kwa kuwakodisha na kuwauzia maeneo na majengo yao na hali wao wakiendelea kunufaika ilihali wametulia au wanafanya mengine huku kipato kinaingia kutokana na kodi hizo.
Umiliki wa rasilimali ardhi na ofisi za biashara
Mwisho kabisa, hatimaye utakuwa ni mmiliki wa ardhi ndani ya nchi yako mwenyewe itakayokupa fursa nyingi ya kufanya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Inasikitisha Mtanzania unaishi kama mkimbizi ndani ya nchi yako kwa kuhamahama mahali pasipo na ulazima. Wewe unapanga mambo yako namna utakavyoijenga biashara yako hapo ulipopanga ofisi wakati huohuo pia mmiliki wako anawaza namna gani atakuondoa ili aweke ofisi zake au ampe mwingine mwenye uwezo wa kumlipa zaidi yako. Ondokana na haya masahibu kwa kumiliki makazi na ofisi zako mwenyewe. Kumiliki inawezekana amua sasa ili upange maendeleo yako kwa uhakika na ufasaha zaidi.
Mtaji utapata wapi?
Napenda nikupe habari njema msomaji wa makala hii, tumia akiba yako kutimiza ndoto zako pia taasisi na mashirika mengi hapa nchini yanahitaji watu wenye malengo haya ili iwawezeshe katika kutimiza ndoto zao, pia taasisi nyingi za kifedha na mashirika mengi hapa nchini yameanza kushindana kutafuta watu wenye malengo kama haya ili iwawezeshe katika uwekezaji huu. Pia hata mashirika mengi hapa nchini yameanza kuwasaidia wananchi kwa kujenga na kuwauzia nyumba wafanyakazi wake na hata wadau wengine wanao hitaji. Uwekezaji huu huchochea ukuaji uchumi wa nchi kwa haraka sana tofauti na uwekezaji mwingine. Unachofanya wewe ni kuandika nia na lengo la aina ya uwekezaji unaotaka kufanya na namna gani utakavyonufaika katika uwekezaji huo na taasisi hiyo namna ambavyo utakavyorudisha fedha hizo (business plan). Ni rahisi sana, wengi wametumia njia hizi za kuomba fedha kwa mashirika na taasisi za kifedha kwa masharti nafuu na kuweza kufanya makubwa tofauti na walivyofikiri.
Nakusihi msomaji wa JIONGEZE UFAHAMU, Wekeza kwenye ardhi na majengo upate mafanikio ya kudumu ukuze uchumi wa wako na uchumi wa nchi.
Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma na mshauri wa ujenzi.
Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888, Email: kimbenickas@yahoo.com