USHAURI; Kama Kitu Hakina Sifa Hizi Tatu Usikisome Na Okoa Muda Wako Ili Ufanye Vyenye Manufaa Kwako.

Makala zako ni nzuri lakini ni ndefu sana, zifanye ziwe fupi ili tuweze kuzisoma.
Haya ni malalamiko ambayo nimekuwa nayapokea kutoka kwa wasomaji wengi, hasa pale ninapowashirikisha makala kupitia mitandao ya kijamii au mitandao mingine. Mwingine amewahi kuandika kwenye maoni chini, japo sijaisoma inaonekana ni nzuri, nikipata muda nitaisoma.
Nikisikia kauli kama hizi huwa nafananisha labda msomaji anamaanisha hivi…
Anaenda hotelini, anapewa chakula halafu anasema chakula chenu ni kitamu lakini ni kingi mno. Au unanunua soda halafu unasema hii soda ni tamu lakini ni nyingi mno. Au ni sawa na mtu kulalamika kwamba maisha ni matamu lakini marefu mno!!
Umeona ni jinsi gani ambavyo malalamiko yanakuwa hayaendani na sababu husika? Sasa leo kwenye kipengele hiki cha USHAURI WA CHANGAMOTO tutajadili kuhusu ni kitu gani usome na kitu gani usisome.
Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kukusalimu, naamini unaendelea vizuri na harakati za kuboresha maisha yako. Kama bado upo kwenye mapambano hongera sana. Sio kitu rahisi na wengi wanaishia njiani na kuamua kuendelea na maisha ya kawaida ambayo kila mtu anayaishi. Ila wewe umeweza kuendelea kukomaa, hakika utakutana na mambo mazuri.
Naomba nikuulize swali moja, ni kigezo gani huwa unaweka kwenye vitu unavyosoma? Je huwa unasoma tu kwa sababu umekutana nacho au huwa una vigezo ambavyo umejiwekea? Kama huna vigezo kuna uwezekano mkubwa sana kwamba unasoma vitu ambavyo vinajaza takataka kwenye akili yako.
Sasa hivi tunaishi kwenye dunia ambayo taarifa ni nyingi sana. Taarifa zinazoingia kwenye mtandao wa intaneti kwa siku moja tu ni nyingi kuliko ambazo mtu aliyeishi karne ya 20 angekutana nazo kwenye maisha yake yote. Unaweza kusema sisi tunaoishi karne hii tuna faida kuliko walioishi karne ya ishirini, lakini huo sio ukweli.
Ukweli ni kwamba pamoja na taarifa hizi nyingi ambazo zinakwenda kwenye mtandao nyingi sana hazina msaada wowote kwako. Lakini ni taarifa ambazo zimeandaliwa kukushawishi ufungue usome na wakati hazitakusaidia kwa njia yoyote ile.
Wingi huu wa taarifa uliopo ndio unawafanya watu wengi washindwe kupata dakika chache za kusoma makala nzuri ambazo zitawasaidia kuwa na maisha bora. Mtu akifungua makala na kuona ndefu anaona akianza kuisoma anapitwa na habari nyingine nyingi ambazo zinaendelea kumiminika kwenye mtandao. Hali hii ya kuona kama unapitwa ndio imekufanya ushindwe kujifunza kupitia taarifa nzuri sana zinazowekwa kwenye mtandao.
Unafungua makala kama hii ambayo kwa kuisoma maisha yako yatakuwa bora zaidi, lakini wakati huo huo akili yako inaruka ruka, haijatulia sehemu moja. Mara unaacha unaenda kufungua facebook, mara unafungua instagram, mara unafungua twitter. Na kote huku hakuna jambo kubwa la maana utakalokutana nalo. Zaidi tu ya kulisha hofu yako uliyojitengenezea kwamba unapitwa.
Tafiti zilizofanywa kwa nchi za wenzetu hivi karibuni zinaonesha kwamba mtu anayetumia simu ya kisasa(smartphone), hasa kijana, hawezi kupita dakika tano kabla hajaigusa simu hiyo. Yaani ni kama watu wamefunga ndoa na simu zao. Kila baada ya dakika chache wanaigusa, na hakuna jambo kubwa la maana mtu anaangalia kwenye kila mara anapogusa, badala yake analisha hofu yake kwamba anaweza akapitwa. Kwamba kuna mtu anaweza akaweka picha yake instagram na wewe ukaikosa!!
Kama Waswahili walivyosema kwamba, miluzi mingi humpoteza mbwa, hivi pia ndivyo ilivyo kwamba wingi huu wa taarifa unawapoteza watu wengi sana. Lengo la makala ya leo ni kukusaidia na wewe usipotezwe na wingi huu wa taarifa, uchague vyanzo vyako vya taarifa ambavyo vitakuwezesha wewe kuboresha maisha yako.
Kwanza kabisa tuweke msingi, kama chochote kinachokuvutia kusoma hakina sifa hizi tatu, achana nacho, ni kelele kwako.
Sifa ya kwanza; kinakuongezea maarifa.
Iwe ni makala au kitabu au jarida au gazeti au blog unasoma, hakikisha kwamba unapomaliza kusoma una maarifa zaidi ya ulivyoanza kusoma. Kama huwezi kupata maarifa ya tofauti na yatakayokusaidia acha kabisa kusoma hiko kitu. Kwa hiyo moja kwa moja habari zote za udaku unaachana nazo. Hakuna maarifa yoyote utakayopata kwa kujua Zari na Diamond, au Wema na Diamond wamefanya nini!! Hizi ni habari za kufuatiliwa na watu ambao sio makini.
Sifa ya pili; kiwe kinakusaidia kuongeza kipato.
Ndio, taarifa yoyote ambayo utaisoma ni lazima uweze kuitumia kwenye maisha yako, kazi yako au biashara yako kuongeza kipato chako zaidi ya unachopata sasa. Kwa mfano ukifuata ninachokushirikisha leo, na kuachana na kelele zote hizo unazopigiwa, utapata masaa mawili ya ziada kila siku. Sasa hebu fikiria ukiyatumia masaa haya kwenye kazi yako, unafikiri utabaki hapo ulipo? Jiulize kila unaposoma kitu, je kinakuwezesha kuongeza kipato? Kama sio achana nacho.
Sifa ya tatu; kifanye maisha yako kuwa bora.
Taarifa yoyote unayoisoma hakikisha inayafanya maisha yako kuwa bora zaidi ya yalivyokuwa mwanzo. Kama unasoma taarifa halafu ukajisikia uko hovyo kuliko ulivyokuwa hujaisoma basi achana kabisa na taarifa ya aina hiyo. Ni sawa na unasoma habari eti freemason watasababisha ajali kubwa sana ili kutoa kafara, hizi ni habari za kijinga, achana nazo.
Vyombo vya habari vya kawaida vimejengwa kwenye misingi ya kutafuta habari ambazo zitakuogopesha sana wewe. Kwa mfano fungulia redio ya bbc idhaa ya kiswahili na hesabu kila habari watakayotoa, utasikia vita kongo, waasi nigeria, waasi somalia, njaa sudani, maandamano sijui wapi. Sasa mambo haya yote yanakusaidia nini katika kuboresha maisha yako?
Usisome taarifa yoyote kama haitakuwa na angalau moja kati ya sifa hizo tatu. Na kwa kipimo hiko hiko kama AMKA MTANZANIA, KISIMA CHA MAARIFA, JIONGEZE UFAHAMU na MAKIRITA AMANI hazikupatii taarifa zenye sifa hizo achana nazo. Sikuvutii usome mitandao hiyo tunayoendesha sisi, ila nakupa mwanga na tumia mwanga huo kumulika kila eneo la maisha yako.
Acha kupoteza muda wako kwa kuruka ruka na habari ambazo hazina mantiki yoyote kwenye maisha yako. Una muda mfupi sana na kila mtu anaupigania. Fanya maamuzi ambayo ni sahihi kwako na yataboresha maisha yako zaidi.
Kwa kumalizia nipende kuwaambia wasomaji wote kwamba AMKA MTANZANIA na mitandao mingine tunayoendesha, tunakazana sana kuwapatia taarifa ambazo zitawaongeza wasomaji maarifa, zitawapa mbinu za kuongeza kipato chao na pia kuwawezesha kuboresha maisha yao. Ni vigumu sana kufikisha taarifa ya aina hii kwa maneno machache ambayo ndio wengi wanapendelea kusoma.
Hivyo kama unajali kweli kuhusu maisha yako, tenga muda wa kutosha kila siku kwa ajili ya kusoma makala nzuri kwenye mitandao hii. Soma ukiwa umetulia na soma ujifunze na sio kukimbia haraka haraka ukawahi instagram, hakuna chochote unachokosa. Usikubali kutumiwa kihisia na kuhangaika na kila habari unayokutana nayo, nyingi ni kelele kwako.
Nakutakia kila la kheri katika kuchagua habari bora kwako kusoma.
TUPO PAMOJA
Makirita Amani 
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

http://www.amkamtanzania.com/p/kuwa-tajiri.html


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: