USHAURI; Mambo 6 Muhimu Ya Kuzingatia Pale Unapokuwa Na Mawazo Mengi Ya Biashara Na Hujui Utekeleze Lipi.

Watu wengi wamekuwa wakikwama kuanza biashara kwa sababu wanakuwa hawajapata wazo zuri la biashara. Mimi huwa nakataa kitu hiki kwa sababu kinachowakwamisha watu sio kukosa wazo bali kutokuwa tayari kuingia kwenye biashara. Kwa sababu mawazo yapo mengi sana na ni mtu tu kuamua kufungua macho na kuchagua ni wazo gani alifanyie kazi.
Kwa upande wa pili kuna watu ambao wana mawazo mengi mpaka wanashindwa kujua ni wazo lipi walifanyie kazi. Hii inaweza kuwa changamoto kwa baadhi ya watu hasa pale unapokuwa hujawa tayari kuingia kwenye biashara au hujaujua vizuri ulimwengu wa biashara.
Leo katika kipengele hiki cha USHAURI WA CHANGAMOTO zinazotuzuia kufikia mafanikio tutajadili hili la kuwa na mawazo mengi na kushinda kujua ni wazo gani mtu ulifanyie kazi. Kabla hatujajadili hili kwa undani, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusiana na changamoto hii.

Nashindwa kufanya maamuzi sahihi ya aina gani ya WAZO Bora la Biashara Kushughulika nalo. Nina mawazo yasiyopungua 3 ya kibiashara na Nayapenda sana hakuna lililomzidi mwenzake. Na yote nimeyapima uzuri ikiwemo la SWOT Analysis zao. Na Yoyote kati ya hizo nina uwezo wa kuianzisha Kutokana na Mtaji mdogo niliokuwa nao. Nashindwa kufanya maamuzi, NIFANYE CHAGUO LIPI?? AU NIFUMBE MACHO NIFUMBUE LOLOTE LITALOKUJA MBELE YANGU NISHUGHULIKE NALO?? S.N

Hivyo ndivyo alivyotuandikia msomaji mwenzetu ambaye anakabiliana na changamoto hii ua kushindwa kujua ni biashara gani afanye kati ya mawazo mengi ya biashara aliyonayo.
Kwanza kabisa niseme ni mara chache sana nimewahi kukutana na watu ambao wana mawazo mengi na hawajui wafanye nini, wengi wamekuwa wakilia kwamba hawana wazo zuri la kibiashara. Sasa tunapokutana na mtu ambaye ana mawazo matatu mazuri na ambayo ameyafanyia upembuzi yakinifu, tunaona kwamba mtu huyu yuko makini.
Lakini pia hii inaweza kuwa ni dalili kwamba mtu hajawa tayari kuingia kwenye biashara hivyo anatumia wingi wa mawazo hayo kama sababu. Kwa sababu mtu mwenye kiu kweli ya kuingia kwenye biashara kwa mawazo hayo angeshaanza zamani na kwa sasa angeshakuwa mbali.
Kwa faida ya msomaji mwenzetu anayesumbuka na changamoto hii na faida yetu sote hapa tutajadili mambo muhimu sana ambayo mtu aliyepo kwenye changamoto hii anapaswa kuyafahamu.
A. Wazo la biashara ni asilimia 1 ya mafanikio kwenye biashara.
Watu wamekuwa wanaweka thamani kubwa sana kwenye wazo la biashara. Watu wamekuwa wakifikiri ukishapata wazo zuri tu la kibiashara basi ndio mchezo umekwisha, unasubiri kuvuna tu. Hii ilikuwa inafanya kazi zamani ila kwa sasa wazo la biashara lina thamani ndogo sana.
Hata kama ungekuwa na wazo zuri kiasi gani la biashara, bado unahitaji kufanya kazi sana ili kuliwezesha kukuletea mafanikio. Hii ni kwa sababu karibu kila wazo limeshafanyiwa kazi na watu wengine. Hivyo kitakachokutoa sio wazo zuri basi jinsi unavyoweza kulitekeleza wazo lako kwa ubunifu na utofauti mkubwa.
SOMA; Ushabiki Unavyokuzuia Kufikia Mafanikio.
B. Kuwa na wazo zuri la biashara hakukuhakikishii mafanikio.
Watu wengi wamekuwa wakichukulia biashara kama pata yote au kosa yote. Yaani ukiwa na wazo zuri umepata yote na ukiwa na wazo baya ni umekosa yote. Sio kweli. Biashara ni katikati ya hapo.
Wazo lolote la biashara utakaloanza nalo ni lazima utakutana na changamoto. Hata kama wazo lingekuwa zuri kiasi gani bado kuna changamoto zake. Hivyo badala ya kupoteza muda ni wazo gani la kuanza ni vyema kuangalia ni wazo lipi unaweza kukabiliana na changamoto zake.
C. Agalia kama unaweza kuwa katikati.
Moja ya njia nzuri za kuboresha wazo lako la biashara ni kuangalia kama unaweza kuwa katikati. Kama una mawazo tofauti ya kibiashara, au kama kuna vitu vingi unavyojua jaribu kuviangalia ni wapi vinaingiliana. Kwa kupata eneo hili ambapo mawazo haya yanaingiliana unaweza kuja na biashara ya kipekee sana ambayo wengine hawawezi kuifikiria.
Hii inahitaji kuumiza kichwa zaidi na kuona ni jinsi gani mawazo uliyonayo yanaweza kuingiliana na ukatoka na kitu cha tofauti. Na kama uko vizuri kwenye mawazo yote basi utakuwa bora sana na wa kipekee duniani.
D. Mipango sio matumizi
Mara zote huwa nasema inapokuja kwenye biashara, mipango sio matumizi. Unaweza kuwa na wazo zuri sana kwenye karatasi, unaweza kupanga vizuri sana utaanzia wapi, wateja ni wakina nani, utauza kiasi gani na faida ni kiasi gani. Lakini utakapoingia kwenye biashara utakutana na uhalisia mwingine na tofauti kabisa na kile ambacho ulipanga kwenye karatasi zako.
Badala ya kupoteza muda ukifikiria ni wazo lipi uanze nalo kwa nini usianze na wazo moja wapo na ukaendelea kujifunza mbele ya safari. Kwa sababu unavyoendelea kusubiri hakuna kipya unachojifunza. Ila kama utaanza kutekeleza wazo moja wapo utakutana na changamoto nyingine na utajifunza zaidi.
SOMA; unalipwa kwa sababu unaonekana au kwa sababu unatoa thamani?
E. Ukishafanya maamuzi usijitie.
Najua kitu kikubwa kinachoweza kumfanya mtu ashindwe kuchagua ni wazo gani anakwenda nalo ni kujutia baadae. Mtu anaweza kufikiri kama akianza na wazo moja na baadae wazo hilo likakwama atajutia kwa nini hakufanya wazo jingine zuri alilokuwa nalo.
Sasa nataka nikuambie kwamba unajidanganya. Hakuna wazo lolote utakalotekeleza uache kukutana na changamoto, hivyo ndivyo maisha yalivyo popote duniani. Hivyo usijutie pale utakapotekeleza wazo moja halafu ukakutana na changamoto kwa kufikiri kwamba kama ungefanya mawazo mengine mambo yangekuwa mazuri zaidi.
F. Amua sasa na usirudi nyuma.
Kitu cha mwisho kabisa ninachopenda kukuambia wewe msomaji ambaye hujui ni wazo gani ambalo utekeleze na kama unayapenda yote na yote uko vizuri, chagua wazo moja na ulifanyie kazi, na wala huna haja ya kufunga macho uchague moja wapo(hivi unaweza kufikiri hivi?) Amua kwa mawazo yako mwenyewe kwamba umeamua kuenda na wazo fulani na hayo mawazo mengine unaweza kuwapatia watu wako wa karibu ambao wanahangaika kutafuta mawazo ya biashara.
Na ukishaamua kwamba unakwenda na wazo fulani ndio hakuna tena kurudi nyuma, hata kama utakutana na changamoto unatakiwa kukabiliana nayo na utakuwa umejifunza kitu kikubwa na muhimu kwenye biashara yako.
Kama utasema uchague wazo moja, ulijaribu na kama likishindwa urudi kwenye wazo jingine, nakuhakikishia mawazo yote yatashindwa. Hivyo amua leo kwamba utafanya wazo moja na hayo mengine wapatie watu wengine wafanya.
Kama wewe utafanya wazo moja na ukakutana na changamoto na ukiangalia uliyempa wazo jingine anakwenda vizuri bila ya changamoto, haimaanishi wazo lile lilikuwa zuri kuliko unalifanya wewe, ila kuna utofauti kati yenu mnaotekeleza hayo mawazo.
Naomba nitumie nafasi hii kukuambia kwamba usiendelee kupoteza muda ukibishana ni wazo lipi ufanyie kazi. Chagua wazo moja kati ya hayo uliyonayo na jitoe kwamba utafanyia kazi wazo hilo mpaka pale utakapoona matunda mazuri kutoka kwenye biashara hiyo. Usipange kujaribu kila wazo, huna muda huo.
Nakutakia kila la kheri kwenye utekelezaji wa wazo lako la biashara.
TUPO PAMOJA
Makirita Amani 
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: