Na Kimbe Nickas
Mwonekano wa Tanzania ya sasa na ya miaka kumi iliyopita ni tofauti sana, mafanikio haya ni kutokana na msukumo mkubwa wa maendeleo ya sekta mbalimbali ukiwemo uwekezaji wa ardhi na majengo unaoshika kasi kubwa ndani na pembezoni mwa miji mikubwa ya Tanzania. Ndugu msomaji wa makala hii usiachwe nyuma bali uwe sehemu ya mafanikio ya kubadili uchumi wa nchi yetu na uchumi wako binafsi, kama wewe ni miongoni mwa watu wengi wanaojiuliza wawekeze kwenye biashara gani itakayokufanya uwe huru kiuchumi na kijamii, jibu ni rahisi sana, isikilize nafsi yako na itendee haki kwa kuwajibika. Nina mengi ya kukushirikisha lakini Leo nakupa mambo muhimu ya kuzingatia kwenye eneo la uwekezaji kabla hujajenga unachotaka kujenga. Mambo haya yatakusaidia kufanya tathmini na hatimaye kufanya maamuzi sahihi ya aina gani ya uwekezaji uweze kufanya, hapa namaanisha aina na matumizi ya majengo kama vile ofisi, maduka, nyumba ya kuishi, mgahawa, hoteli, zahanati au shule.
Mzunguko wa watu
Mzunguko wa watu huathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya uchumi na jamii katika eneo lolote, mara nyingi maeneo yenye mzunguko mkubwa wa watu ni maeneo yenye huduma bora za kijamii na kiuchumi. Maeneo haya watu huingia na kutoka kutafuta huduma muhimu za kimaisha. Maeneo yenye ofisi za serikali, taasisi mbalimbali, viwanda, makampuni binafsi na umma huwa na mzunguko mkubwa wa watu. Huduma hizo huvuta watu kutoka sehemu mbalimbali kuingia ili kukidhi mahitaji yao ya kimaisha yanayopatikana maeneo hayo. Unapowekeza maeneo kama haya unapaswa kuangalia mapungufu yaliyopo ili kukidhi mahitaji ya watu wa eneo hilo, mfano, kama hakuna hoteli utajenga hoteli, hakuna pakingi utajenga pakingi. Muhimu ni kuangalia namna gani utaondoa tatizo na utakidhi mahitaji ya wengi huku kwa upande wa pili unajijengea uwezo wa kuwa mwenye mafanikio kifedha kwa kuwa umewekeza kilicho sahihi kwa wakati huo.
SOMA; Kama Umewekeza Kwenye Majengo Yafahamu Magonjwa Sugu Yanayo Athiri Majengo.
Aina za nyumba zilizopo
Popote unapotaka kuwekeza nyumba yako lazima utajifunza kitu kutoka kwa waliotangulia kujenga kwenye eneo hilo, mazuri na mapungufu mengi utayaona, yapo mengi ya kujifunza endapo utakuwa makini na kuzingatia ubora, mpangilio na mwonekano wa nyumba za jirani. Lengo la kutathmini nyumba zilizopo ni kuchukua yale mazuri na kuepuka kurudia mapungufu yaliyojitokeza kwa wengine. Mfano, nyumba nyingi za hivi karibuni zimejengewa vyumba vya biashara yaani frem, na wengi wameiga hivyo, lakini wanasahau kuwa wapo wafanyabiashara wengi wanao hitaji aina tofauti ya “fremu” hizo kukidhi mahitaji yao ya kibiashara, tambua kuwa kuna taasisi, kampuni na mashirika mbalimbali yanayohitaji majengo ili kuwafikia wateja wao waliopo sehemu mbalimbali za nchi. Hivyo ili uwe na uwanja mpana wa kupata wateja kwenye majengo ya biashara, lazima ujenge nyumba itakayokidhi mahitaji mbalimbali ambayo pia ni rahisi kwa kubadili matumizi pasipo ubomoaji wowote. Hakikisha ujenzi utakaofanya unaongeza thamani katika eneo hilo, hii ndiyo sababu mojawapo ya wewe kutumia wataalamu kwenye mipango yako ya uwekezaji ili wakushauri namna gani ya kujenga kutokana na mabadiliko makubwa yanayojitokeza kwa sasa. Jitahidi kuwa bora zaidi ya wengine ili upate wateja zaidi na mafanikio zaidi.
Miundombinu iliyopo
Kabla ya kununua ardhi au kuanzisha ujenzi wako ni muhimu sana ukazingatia na kutathmini miundombinu iliyopo ili isisababishe ukinzani wowote wa ujenzi wako unaotaka kufanya. Kwa mujibu wa katiba tuliyonayo, ardhi yote ya jamhuri inasimamiwa na rais wa jamhuri, hivyo kama kuna miundombinu yoyote yenye manufaa kwa wengi jaribu kuikwepa maana kwa namna yoyote ile utaondoka wewe ili miundombinu hiyo iendelee kuwanufaisha wengi. Zingatia sana hifadhi za barabara, misitu, nishati za umeme na miundombinu iliyofukiwa. Miundombinu iliyofukiwa juu ya ardhi huwekwa alama (bikoni) kila baada ya umbali fulani kuonesha mwelekeo wa miundombinu hiyo. Pia maeneo yenye miundombinu ya uhakika huwa ni kivutio kikubwa kwa watu tofauti na maeneo ambayo bado hakuna miundombinu ya uhakika.
Fanya uthamini binafsi
Jijengee utaratibu wa kufanya tathmini kabla ya kufanya uwekezaji wowote ule, kabla ya kununua eneo au nyumba jipe muda wa kutosha wa kufikiri na kufanya tafiti ili uwe na taarifa sahihi la eneo husika. Tathmini yako izingatie ulinganifu wa bei za manunuzi au gharama za ujenzi, matumizi rasmi ya eneo hilo, umiliki rasmi wa eneo hilo, hata ramani ya nyumba yako lazima izingatie mazingira ya eneo husika. Jipe muda wa kutosha kupata taarifa sahihi kabla ya kufanya maamuzi ya kununua au kujenga, Hii itakusaidia wewe kufanya uwekezaji wako kihalali na kwa kufuata taratibu zote, pia utaepuka gharama kubwa kutokana na udanganyifu wa watu au faini kutoka kwa mamlaka husika endapo utakiuka jambo lolote kwa kukosa taarifa sahihi.
Zione mamlaka husika za kisheria na usimamizi
Daima unaponunua au kuwekeza nyumba au kufanya chochote kwenye ardhi zione mamlaka husika ili upate taratibu rasmi za kufuata ili malengo yako yatimie pasipo misuguano na mamlaka hizo za serikali. Hakuna jambo linalokosa taratibu za kimfumo, hata kwenye ujenzi zipo mamlaka zinazosimamia mfumo na vibali kabla na wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi. Pia taratibu hizo hutofautiana kutokana na sera na taratibu za kimfumo za mamlaka za usimamizi wa eneo husika. Watu wengi hawajui kuhusu taratibu hizi, hujikuta wameletewa barua za kusimamisha ujenzi wao (stop order) pasipo kujua nini cha kufanya. Ni muhimu sana ukazifahamu taratibu za mahali husika kabla hujaamua kujenga, tofauti na hivyo utabomolewa na kujikuta umepoteza fedha nyingi pasipo msaada wowote.
Washirikishe wataalam wa Ardhi na ujenzi
Ni muhimu sana kuwashirikisha wataalamu wa fani husika ili wakushauri namna gani uweze kufikia lengo lako huku ukitabasamu kwa furaha. Watu wengi wamejikuta wapo kwenye majuto makubwa baada ya kutapeliwa fedha zao na watu wasio na ufahamu wowote kuhusiana na ardhi na ujenzi wa nyumba. Watafute sasa maana wanapatikana kila mahali, wathamini ardhi (land valuer) watakusaidia namna gani ya kumiliki ardhi yako, wasanifu majengo(Architects) watakuchorea ramani ya nyumba yako, wakadiriaji majenzi (Quantity Surveyors) watakusaidia kupanga na kusimamia gharama za ujenzi wako, wahandisi (ujenzi, umeme na maji) watasimamia ujenzi wa nyumba yako. Hawa wote kwa pamoja ni timu yenye uwezo wa kuhakikisha mjasiriamali unapata ulichotarajia kupata kwa uhalisia wake. Kama unataka mafanikio ya kweli watumie wataalamu kwenye mambo yako.
Tuendelee kuwa pamoja kupitia JIONGEZE UFAHAMU tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.
Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma na mshauri wa ujenzi.
Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888, Email: kimbenickas@yahoo.com