Swali muhimu sana kujiuliza kama hutaki kumpoteza mtu ambaye ni muhimu kwako.

Kama wewe ni mfanyabiashara jiulize swali hili kila siku. Je kama mteja uliyenaye sasa ataamua kuacha kufanya biashara na wewe, je atakwenda kwa mfanyabiashara mwenye sifa gani? Kama hutaki kumpoteza mteja huyo basi tengeneza sifa hizo atakazozifuata.

akiondoka
NI KIPI AMBACHO MTU AMECHOSHWA NACHO KWAKO/ KIFANYIE KAZI KAMA HUTAKI KUMPOTEZA MTU HUYO.

Kama umeajiri na mfanyakazi ni muhimu kwako jiulize, kama ataamua kuondoka labda kwa sababu amepata kazi nyingine nzuri zaidi, atakwenda kwenye kazi ya aina gani? Kisha ifanye kazi yake iwe vile ambavyo angeshawishika kuondoka.

Kama umeajiriwa jiulize swali hili muhimu pia; kama mwajiri wako angeamua kuachana na wewe ili achukue mfanyakazi mwingine, je angechukua mfanyakazi mwenye sifa gani? Zijue halafu zitengeneze kwako.

Na pia kama upo kwenye mahusiano ya kimapenzi au ndoa jiulize swali hili muhimu sana; kama mwenzi wako ataamua kuachana na wewe je atakwenda kwa mtu mwenye sifa na tabia gani? Kisha tengeneza sifa na tabia hizo kwako mwenyewe.

Hivi mpaka hapo si maisha ni marahisi? Sio sana lakini unaweza kuzuia vitu vingi kwa kujiuliza swali hilo rahisi sana.

Mara zote huwa nasema kuna dharura chache sana kwenye maisha, vitu vingi tunaviona kabisa vinakuja. Kama ni mteja anaondoka unaona kila dalili, kama ni kazi unafukuzwa unaona kila dalili. Lakini hatuko tayari kuchukua hatua kuzuia jambo lisitokee, bali tupo tayari kulalamika likishatokea.

Anza kujiuliza swali hilo rahisi kila siku na kila mara kwa kila kitu ambacho ni muhimu kwako.

TAMKO LA LEO;

Swali rahisi na muhimu kabisa kujiuliza kwenye jambo lolote ambalo ni muhimu kwangu ni je mtu huyu akiondoka atakwenda kwa nani? Najua hili ni swali ambalo litazuia mambo mengi yasitokee, litahakikisha mahusiano ya kazi, biashara na hata ya kimapenzi yanaendelea kuwa imara kwa sababu mara zote nitatoa thamani inayotegemewa. Kila siku, kila mara na kwakila mahusiano ambayo ni muhimu kwangu nitatumia swali hili ili kuyaboresha zaidi.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.