Pamoja Na Vitabu Vingi Kuandikwa Kuhusu Mafanikio, Kwa Nini Watu Wengi Bado Hawana Mafanikio?

Kuna vitabu vingi sana vimeandikwa kuhusu mafanikio na vingine vinaendelea kuandikwa.
Kuna makala nyingi sana zimeandikwa kuhusu mafanikio na nyingine zinaendelea kuandikwa kila siku.
Swali ambalo wengi huwa wanajiuliza pamoja na maarifa haya mengi yanayopatikana kuhusu mafanikio, mbona bado watu wengi hawafanikiwi?
Mtu mmoja amewahi kuniuliza, mbona wale wauza vitabu vimeandikwa how to get rich, wasingesoma vitabu hivyo na wakawa matajiri badala yake wanaendelea kuuza vitabu katika hali ile ile ya chini?

JE UPO TAYARI KUFANYIA KAZI YALE UNAYOJIFUNZA?

 
Kama na wewe unajiuliza swali hili na hupati majibu, basi leo nakukaribisha hapa na kwa pamoja twende ili tuone ni nini kinasababisha hali hii.
SOMA; Nikipata Muda Nitafanya.
Ni kweli kwamba pamoja na maarifa mengi kupatikana kuhusu mafanikio, bado ni sehemu ndogo sana ya watu ambao wamefanikiwa. Swali ni je tatizo liko wapi? Ni kwamba maarifa haya hayafai? Au watu ndio hawawezi kuyatumia?
Kusema kwamba maarifa haya hayafai ni kujidanganya, kwa sababu kila aliyefanikiwa anazungumzia misingi iliyomfikisha pale alipo na misingi hii ndio imekuwa inaandikwa kwenye vitabu na makala mbali mbali.
Hivyo basi tatizo kubwa linabaki kwa watu wanaopokea maarifa haya. Na katika hali hii ya watu kuwa ndio wenye matatizo, hapa kuna baadhi ya maeneo muhimu ambayo watu hawayafanyii kazi;
1. Kusoma tu haitoshi unahitaji kufanyia kazi.
Hata kama ungesoma vitabu vingapi, hata kama utawajua waandishi kwa majina na historia zao, hata kama utaweza kusimulia kitabu mwanzo mpaka mwisho, kama hutafanyia kazi yale ambayo unajifunza ni kazi bure. Hakuna kitakachokusaidia kwenye mafunzo yako kama wewe mwenyewe hutachukua hatua ya kufanyia kazi yale mambo ambayo umejifunza.
Pamoja na kufanyia kazi kuwa ndio kiungo muhimu, ni watu wachache sana ambao wanakuwa tayari kufanyia kazi kile wanachojifunza. Tatizo kubwa ni kwamba ili uweze kufanyia kazi yale ambayo unajifunza, ni lazima ubadili mfumo wa maisha yako na watu wengi hawapendi kubadilika. Hivyo husoma na kusema nitafanya au nikipata muda nitafanya, bila ya kujua kwamba wanajidanganya wenyewe.
SOMA; Kitabu Cha August; Eat Move Sleep(Kula, Kufanya Mazoezi Na Kulala).
2. Ukosefu wa nidhamu binafsi.
Kuna ambao wanasoma vitabu hivi na wanaamua kweli kwamba wanabadilika na kweli wanaanza kubadilika. Na wanachukua hatua za mwanzo kabisa za mabadiliko. Lakini muda sio mrefu wanarudi kule walikokuwa mwanzo na hawaendelei tena na mpango wao wa mabadiliko ili kufikia mafanikio.
Hawa ni wale ambao wamekosa nidhamu binafsi. Nidhamu binafsi ni pale ambapo unafanya kitu ambacho umepanga kufanya, iwe unajisikia kufanya au la. Wengi huanza mwanzo wakiwa na hamasa ila baada ya muda hamasa hii inapotea na wanashindwa kujisukuma kuendelea na mipango yao ya kuleta mabadiliko kwenye maisha yao.
Mwishowe wanarudi kwenye hali yao ya kawaida na kuona kama kuendelea na mabadiliko ni kujitesa. Ukosefu wa nidhamu binafsi ni changamoto kubwa sana inayowazuia wengi kuweza kudumisha mabadiliko wanayoanza kwenye maisha yao.
3. Kukosa uvumilivu.
Hapa kuna kundi kubwa sana la watu. Mtu anataka kwa kuwa ameshajifunza kuhusu mafanikio basi anapoanza kufanya tu aone mafanikio yakimfuata kwa wingi. Hii haijawahi kutokea popote, lakini ndivyo watu wanavyotaka.
Mafanikio hayaji kwa haraka, mafanikio hayaji kwa urahisi. Hata pale ambapo unakuwa tayari umeshapata maarifa sahihi, bado unahitaji kuweka nguvu na kuwa mvumilivu pia.
Utaanza biashara zitashindwa, utajaribu mradi utashindwa, utaingia kwenye ushirikiano na watu na watakudhulumu na mengine mengi kama hayo. Kama huna uvumilivu, hata kama ungekuwa na maarifa kiasi gani hakuna kitakachoweza kukusaidia kufikia mafanikio kwenye maisha yako.
SOMA; Hatua Moja Ndogo Kila Siku Ndio Kitu Pekee Unahitaji.
4. Kutaka maisha yabadilike wakati wewe uko vile vile.
Ni jambo la kushangaza na kuchekesha lakini ndivyo fikra za wengi zilivyo. Yaani mtu anataka kuona maisha yake yakibadilika, ila yeye hataki kubadilika, hebu niambie hili litatokeaje?
Kwa mfano ili upate muda wa kutosha wa kuweka ubora kwenye kazi unayofanya, unahitaji kupunguza muda unaopoteza kwenye mitandao ya kijamii, kuangalia tv, kubishana mambo yasiyo na msingi kwako.
Lakini wewe unataka muda wote uwe kwenye mitandao ya kijamii ili usipitwe na yanayoendelea, unataka uangalie vipindi vyote unavyopenda kwenye tv, bado unataka ubishane kuhusu mpira, kuhusu siasa, na hata kuhusu wasanii, nani ana mimba na ni ya nani. Na hapo tena unataka upate mafanikio, kwa sababu tu umepata maarifa ya mafanikio? Haiwezekani rafiki yangu, unajidanganya.
5. Kushindwa kuzuia tamaa.
Kama kuna kitu kimoja ambacho kinawazuia watu wengi kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao basi ni hiki kimoja, kushindwa kuzuia tamaa.
Mara zote kwenye maisha, kuna kitu ambacho ni rahisi kufanya na kinaleta furaha ya muda mfupi. Halafu kuna vitu ambavyo ni vigumu kufanya lakini vinaleta furaha ya muda mrefu. Unajua watu wanapenda kufanya vitu gani? Hujakosea, wanapenda kufanya vile ambavyo ni rahisi kwa sasa na vinaleta furaha ya muda mfupi. Lakini kwa kufanya vitu hivi moja kwa moja wanajinyima nafasi ya kuweza kufanya vitu ambavyo ni vikubwa zaidi na vingeweza kuleta furaha ya muda mrefu.
Kushindwa kuzuia tamaa ya sasa kwa ajili ya mafanikio ya baadae ni changamoto kubwa sana.
Je kwa mambo haya hakuna vitabu ambavyo vimeandikwa?
Vipo vingi sana, na watu wanavisoma lakini hawachukui hatua, kama tulivyoona kwenye maelezo haya yote.
Je kwa mtu kusoma hapa atabadilika na kuweza kufikia mafanikio kwenye maisha yake? Sijui, labda tuanze kukuuliza wewe, je utabadilika na kuanza kufanyia kazi yale unayojifunza ili ufikie mafanikio? Eh? Jibu tayari unalo.
Sijui kama utachukua hatua, lakini ingekuwa vizuri sana kama ungefanya hivyo leo. usiseme ukipata muda utafanya, huna muda mwingine zaidi ya leo. mafanikio sio kubadili vitu vingi kwa wakati mmoja, bali kuwa na mabadiliko madogo madogo kwa muda mrefu. Je utafanya?
Ningependa sana ufanye, kwa sababu maisha yako yatakuwa bora na tutakuwa na jamii bora, na taifa bora na dunia bora pia. Huoni hii ni nafasi nzuri sana kwako kuwa sehemu ya dunia hii bora? Fanya basi kwa nafasi yako. Achana na tamaa na kuwa mvumilivu, hakuna ambacho kinashindikana.
Nakutakia kila la kheri katika safari hii ya kuboresha maisha yako uliyoamua kuingia. Nikukaribishe kama unapenda kujifunza zaidi kuhusu maisha ujisajili kwenye mfumo wa email ambapo kila jumapili utakuwa unatumiwa makala nzuri kuhusu FALSAFA ZA MAISHA. Kuingia kwenye mfumo huo bonyeza maandishi haya na uweke taarifa zako.
Rafiki na Kocha wako.
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “Pamoja Na Vitabu Vingi Kuandikwa Kuhusu Mafanikio, Kwa Nini Watu Wengi Bado Hawana Mafanikio?

Add yours

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: