Mtu yeyote anapofanya au anaposhindwa kufanya jambo, anakuwa na sababu mbili.
Sababu ya kwanza ni sababu nzuri ya kwa nini amefanya au ameshindwa kufanya. Hii ni sababu nzuri kwa maana kwamba ndio atakayotumia kuwaambia wengine kuhusu kile alichofanya au alichoshindwa kufanya.
Sababu ya pili ni sababu halisi. Hii ndio ile sababu hasa kwa nini mtu amefanya au ameshindwa kufanya jambo. Sababu hii ndio yenyewe hasa na mara nyingi huwa inauma.

Sasa mtu anapofanya au anaposhindwa kufanya jambo, wewe atakuambia sababu nzuri, lakini usikubali mara moja, jua sababu halisi na hii itakufanya uwe na uhakika kweli na kinachoendelea. Hata wewe mwenyewe unapofanya jambo lolote huwa una sababu hizi mbili, sababu ya sababu nzuri, ambayo watu watainunua na sababu ya kweli ambayo ndio ukweli wenyewe na hutaki watu wajue.
Kwa mfano, wewe ni mfanyakazi na hujatimiza majukumu yako kwa wakati. Sababu nzuri zinaweza kuwa nyingi, umeme ulikatika, nilipewa majukumu mengine kabla ya kumaliza haya ya kwanza na kadhalika. Lakini sababu ya ukweli ni wewe ni mvivu kiasi cha kushindwa kupangilia majukumu yako vizuri na kuhakikisha hayaingiliwi na chochote.
SOMA; Usijaribu Kumbadili Mtu, Utapoteza Muda Wako…
Au umeahidiana na mtu mkutane sehemu fulani katika wakati fulani. Mwenzako anafika na kukusubiri kwa muda mrefu, unafika umechelewa sana na tayari unakuwa na sababu nzuri, kulikuwa na foleni, nilikwama mahali na kadhalika. Lakini hapa sababu halisi ni kwamba mkutano huu haukuwa muhimu kwako kiasi cha kuupa kipaumbele kuliko vitu vingine vyote. Kwa mfano ingekuwa ni hafla ya kukukabidhi zawadi ya milioni mia moja, ungechelewa hata sekunde moja?
Tumalizie na mfano huu wa mwisho, mwanasiasa anahama chama chake wakati wa uchaguzi, atakupa sababu nyingi sana nzuri, chama hiki kimeoza, hakina haki, kimekosa mwelekeo, kina upendeleo na nyingine nyingi. Lakini sababu halisi ni kwamba nahama kwa sababu maslahi yangu kwenye chama hiki yameshaingiliwa na inabidi nitafute sehemu nyingine ambapo maslahi yangu nitaweza kuyapata.
Mara zote unapofikiria kwa upande wa sababu halisi utaweza kuujua ukweli wenyewe na hutadanganywa tena au kuumizwa. Na unapofikiria kwa sababu halisi kwa matendo yako wewe mwenyewe utajisukuma kufanya hata kama ulitaka kuacha kwa kutafuta sababu.
Kuanzia sasa mtu anapokupa sababu jua hiyo ni sababu nzuri, ni jukumu lako kutafuta ipi ni sababu halisi. Na wewe mwenyewe unapotaka kutoa sababu jiulize ni ipi hasa sababu halisi.
TAMKO LA LEO;
Najua ya kwamba mambo yote tunayofanya au tunayoshindwa kufanya ni kwa sababu mbili kuu, sababu nzuri na sababu halisi. Sababu nzuri ndio zile tunazowaambia watu au watu wanatuambia. Sababu halisi ni zile tunazozijua wenyewe ndani ya nafsi zetu. Kuanzia sasa nitakuwa nafikiria ni ipi sababu halisi na hii itaniwezesha kutokuumizwa na wengine na kunifanya mimi kuwa mwaminifu kwa wengine, kwa sababu nitaepuka kutoa sababu nzuri.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.