Kufikia mafanikio makubwa, kupata kile ambacho hujawahi kupata, ni njia ngumu sana ambayo hujawahi kupita.

Katika ugumu huu kuna wakati unaweza kushawishika siyo tu kwamba njia unayopita ni ngumu, bali kile unachofanya hakiwezekani. Na ukishajishawishi kwamba haiwezekani unajua ni nini kinafuata, unaacha kufanya na malengo yako yote yanakuwa yameishia hapo.

Sisi binadamu ni rahisi sana kujidanganya wenyewe, hasa pale tunapojishawishi kwa hali tunazopitia. Hivyo kwa namna yoyote ile, kama utajiangalia mwenyewe utapata sababu za kutosha za kuunga mkono kile unachotaka kufanya.

Ili kuepuka kujidanganya, hasa kwenye safari ya kufikia malengo makubwa, kuna sehemu unayotakiwa kuangalia kabla hujasema kwamba haiwezekani.

Kabla hujasema kile unachotaka kufanya hakiwezekani, angalia kama hakuna mtu mwingine ambaye ameshakifanya. Kama kuna mtu au watu wengine ambao wameshafanya kile ambacho na wewe unataka kufanya, hali inabadilika na siyo kuwa haiwezekani, bali wewe hujajua njia bora ya kuweza kufanya kitu hiko.

Ukishaona watu ambao wameshafika pale unapotaka kufika wewe, kazi inabaki kwako kujifunza kwamba wao wamefikaje ili na wewe uweze kufika. Na pia unahitaji kujichunguza mwenyewe na kuona ni wapi ambapo unakosea mpaka unashindwa kupata matokeo ambayo ni bora.

Kama kuna watu ambao wameshafika pale ambapo wewe unakazana kufika, inawezekana hata wewe kufika pale, hata kama njia ni ngumu kiasi gani. Na ugumu wa njia ndiyo unaoweka thamani kubwa kwenye kile unachotaka. Ni wajibu wako kuweka juhudi na kujifunza zaidi ili kuweza kufika unakotaka kufika.

Kama hakuna ambaye ameshafika pale unapotaka kufika, unahitaji wewe uwe wa kwanza kufika ili ufungue njia kwa wengine. Kabla ya mwaka 1954 ilikuwa inajulikana kabisa ya kwamba hakuna binadamu anayeweza kukimbia maili moja chini ya dakika nne. Na hivyo hakuna aliyejaribu kufanya hivyo. Lakini mwaka 1954 Roger Bannister aliweza kukimbia maili moja kwa dakika tatu na sekunde 58. Alishangiliwa sana na aliandikwa sana kwamba ni mtu pekee mwenye uwezo wa kukimbia maili moja chini ya dakika nne. Lakini siku 46 baadaye, mtu mwingine aliweza kukimbia kwa muda chini ya ule wa Roger. Na kwa sasa hata watoto wa sekondari wanaweza kukimbia maili moja chini ya dakika nne.

Unajua ni nini kilichotokea, alipoweza kufanya mmoja, wengine walipata uhakika kwamba inawezekana na hivyo kufanya. Hivyo kabla hujajishawishi kwamba haiwezekani, hebu angalia kwanza kama hakuna ambaye ameshafanya. Na kama hakuna, basi wewe uwe wa kwanza kufanya.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

SOMA; WORLD CLASS; Mbinu Za Kisaikolojia Za Kuidanganya Akili Yako Ili Uweze Kufanya Kazi Zaidi Hata Kama Umechoka