Kinachowachosha wafanyabiashara wengi, na kuona biashara wanayofanya haiwezi kufanikiwa, ni pale wanapofikiri ya kwamba kila mtu anapaswa kuwa mteja wa biashara wanayofanya.

Ni kweli unaweza kuwa na biashara ambayo inaweza kumfaa kila mtu, lakini siyo kila mtu anaweza kuwa mteja wa biashara yako. Badala yake wapo watu ambao wanafaa sana kuwa wateja wa biashara yako na ukishakuwa nao utaifurahia mno biashara unayofanya.

Wapo pia wateja ambao watapenda kile unachouza, lakini bado siyo wateja wazuri wa biashara yako. Unaweza kujaribu kuwafanya kuwa wateja lakini msiweze kwenda vizuri.

Unachohitaji kufanya kwenye biashara, ni kuweka mkazo kupata wale wateja wanaoamini kile ambacho wewe na biashara yako mnaamini. Ukiweza kuwapata wateja wa aina hii, utafurahia kufanya nao biashara na kila mnachofanya mtaelewana vizuri.

Kama utapata wateja wanaoamini tofauti na unavyoamini wewe na biashara yako, kila mara mtakuwa mnapishana, kwa sababu tayari imani zetu haziendi pamoja.

Unapofanya biashara na wale wateja wanaoamini unachoamini, uaminifu baina yenu unakuwepo a ushirikiano unakuwa mkubwa.

Dunia ya sasa ni kama kijiji, unaweza kufanya biashara na mtu yeyote, popote pale alipo duniani. Unaweza kuchagua ni aina gani ya wateja unaowataka kwenye biashara yako, kisha weka juhudi katika kuwafikia.

Siyo lazima ukubali kuchukua kila mteja na wala usipendelee wateja wa mara moja pekee. Tengeneza wateja wa kudumu kwenye biashara yako kwa kutafuta wateja ambao wanaamini kile unachoamini na kile biashara yako inachoamini pia.

Hii inakwenda kwa biashara zote, iwe ni uchuuzi, huduma au uzalishaji.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK