Uchambuzi Wa Kitabu; From Poverty To Power (Utambuzi Wa Mafanikio Na Amani).

Kila mtu anapenda kuwa na maisha mazuri, kila mtu anapenda kuwa na mafanikio kwenye maisha yake. Lakini ni wachache kwenye jamii zetu ambao wanaishia kuwa na mafanikio kweli, ni wachache ambao wanaishi yale maisha ya ndoto zao, huku wengi wakisumbuka na maisha mpaka siku wanaondoka hapa duniani.

Watu wengi wamekuwa wakijiuliza ni kipi kinawatofautisha wale wanaofanikiwa na wale wanaoishia kuwa kawaida. Wengi walifikiri ni asili, lakini kwa watu wa asili moja bado wapo waliofanikiwa na wapo walioshindwa. Wakafikiri huenda ni mazingira, lakini ndani ya mazingira sawa, kuna waliofanikiwa na wapo walioshindwa.

 

Ni baada ya uchunguzi na ufuatiliaji wa muda mrefu ndipo imekuja kugundulika tofauti ya wanaofanikiwa na wanaoshindwa inaanzia kwenye akili zao, inatokana na mawazo yao. Ukichukua mawazo ya wanaofanikiwa, ni tofauti kabisa na ya wale wanaoshindwa.
Hapa ndipo mwandishi James Allen, anapotuonesha namna mawazo yetu yalivyo na nguvu ya kutengeneza maisha yetu. Karibu tujifunze kupitia kitabu chake cha FROM POVERTY TO POWER.

1. Hakuna mtu ambaye hajawahi kupitia magumu kwenye maisha yake, hakuna mtu ambaye hajawahi kukutana na majaribu. Hakuna moyo ambao haujawahi kuvunjwa, hakuna akili ambayo haijawahi kukutana na usumbufu wa mawazo. Hakuna nyumba ambayo haijawahi kukutwa na magonjwa na misiba. Kuwepo kwetu hapa duniani ni sababu namba moja ya kukutana na haya, na hivyo tunahitaji kujua njia sahihi ya kuondokana nayo.

2. Mabaya yote tunayokutana nayo kwenye maisha yetu, yanarekebishika. Mabaya haya siyo ya kudumu, labda kama sisi wenyewe tutayafanya yadumu. Hivyo unapopitia mabaya, usikate tamaa na kuona ndiyo mwisho wa safari, badala yake jua ni mapito tu na safari itaendelea.

3. Msingi wa mabaya na maovu yote ni ujinga. Kwa kukosa uelewa watu wamekuwa wakichukua hatua ambazo zinawafikisha kwenye mabaya, au kushindwa kuchukua hatua za kuwaondoa kwenye mabaya wanayopitia. Hivyo dawa ya uhakika ya kuondokana na mabaya na maovu ni kujielimisha na kuondokana na ujinga.

4. Kila mtu ana dunia yake, na dunia ya mtu imetengenezwa kwa mawazo yake, tamaa na msukumo alionao ndani yake. Kutokana na hivi vinavyotengeneza dunia ya mtu, mtu anaweza kuona dunia yake ni ya uzuri na furaha au akaona dunia yake ni ya mabaya, uovu na maumivu. Dunia unayoiona na kuiishi umeitengeneza wewe mwenyewe kwenye mawazo yako.

5. Hakuna kinachotokea nje ya mtu ambacho kinajenga au kuharibu maisha ya mtu. Maisha ya mtu yanajengwa au kubomolewa na kile ambacho kipo ndani yake. Na hapo tunaanzia kwenye mawazo yake. Kama yanayotokea nje ya mtu yangekuwa na nguvu, tungetegemea watu wote waliopo kwenye mazingira sawa basi maisha yao yawe sawa. Lakini hali haipo hivyo, hii ikimaanisha kwamba licha ya yale yanayotokea nje ya mtu, maamuzi hasa yapo ndani yake.

6. Watu huamini kwamba zile tabia walizonazo ndizo ambazo wengine wanazo. Hivyo mtu ambaye ni mwongo, huamini kila mtu ni mwongo, mwenye wivu anaona kila mtu anamwonea wivu. Hali kadhalika kwa tabia nyingine zote, ziwe nzuri au mbaya. Hii ina maana kwamba kama unataka wengine wawe na tabia tofauti, anza kujiangalia kwanza wewe una tabia gani.

SOMA; Mambo Sita(6) Muhimu Ya Kuzingatia Ili Kuwa Na Maisha Yenye Furaha Na Mafanikio Makubwa.

7. Sheria kuu ya asili ni ile ya SABABU NA ATHARI. Sheria hii inasema kwamba kila ambacho kinatokea, kimesababishwa. Kila unachokiona ni athari za mambo yaliyosababishwa. Unavuna kile ulichopanda ni upande mwingine wa sheria hii. Hii ina maana kwamba upo hapo ulipo sasa kutokana na mambo uliyofanya huko nyuma. Na matokeo ya kesho yatategemea utakachofanya leo.

8. Hakuna nafasi ya walalamikaji kwenye dunia hii. Kwa sababu walalamikaji ni watu ambao hawapendi kuchukua hatua, bali wanatafuta wa kuwasingizia. Walalamikaji hawana nafasi kwa sababu wanakwenda kinyume na sheria ya asili. Wao wanakataa ya kwamba hawajasababisha ile hali waliyonayo sasa, wakati kwa asili wao wenyewe wamechangia kuwa pale walipo sasa.

9. Watu wengi wamekuwa wakiishi maisha ya kujidanganya (delusion), kwa kuamini vitu ambavyo haviendani na sheria ya asili. Watu hawa wamekuwa wakijikuta wanaumia kila mara kwa sababu wanakataa kukubaliana na sheria hii. Hawataki kukubali pale ambapo walikosea, au kuepuka kuchukua hatua ambazo zinawapelekea kwenye matatizo zaidi.

10. Hakuna kitu kibaya, cha kujiharibu kama kujidharau wewe mwenyewe. Kujidharau kunawafanya watu wengi kushindwa kuchukua hatua na kushika hatamu ya maisha yao. Watu wamekuwa wakijiona wao ni waathirika na hawawezi kuchukua hatua kwa lolote wanalopitia. Hii inawafanya kuendelea kuwa kwenye hali ngumu na kuishia kuwa na maisha mabovu.

SOMA; Huu Ndio Msingi Mkuu Wa Maisha Ya Furaha, Amani Na Mafanikio Makubwa.

11. Njia ya uhakika ya kuondoka kwenye umasikini au hali yoyote mbaya ni kuachana na mawazo hasi na ubinafsi ambao upo ndani ya mtu. Ubinafsi umewafanya wengi kuwa kwenye gereza la umaskini na matatizo yao wenyewe. Unapoachana na ubinafsi, na kuacha mawazo hasi, unaanza kuona mchango wako kwa wengine na kuziona fursa zaidi.

12. Utajiri na mafanikio ya kweli havipimwi kwa fedha pekee, bali kwa maisha ambayo mtu anaishi. Kama mtu ni mwema, atakuwa na maisha mazuri na wale wanaomzunguka, na atakuwa na mafanikio, hata kama hana fedha nyingi. Kama mtu amekosa wema, hata kama ana fedha nyingi kiasi gani, hana mafanikio ya kweli.

13. Ili kupata mafanikio ya kweli, ni lazima uweze kujidhibiti wewe mwenyewe. Ni lazima uweze kuyadhibiti mawazo yako, uondokane na mawazo hasi na ubinafsi na ukaribishe mawazo safi ya mafanikio. Kama huwezi kujidhibiti wewe mwenyewe, utatoa nafasi kwa vitu vingine kukudhibiti. Hakuna mafanikio kama huwezi kujidhibiti.

14. Imani na kusudi ndiyo nguvu kuu inayoendesha maisha ya mtu. Hakuna kitu ambacho imani thabiti na kusudi imara vinashindwa kukamilisha. Unahitaji kuwa na umani kwamba unaweza, kuwa na imani kwamba inawezekana, pia unahitaji kujua kusudi la maisha yako. Ukilifanyia kazi kusudi hili kwa imani, mafanikio ni yako.

SOMA; Mbinu Moja Rahisi Sana Ya Kufanikiwa Kwenye Kazi Yoyote Unayofanya.

15. Haijalishi kusudi la maisha yako ni nini, fanya kusudi hilo kwa akili zako zote, moyo wako wote na nguvu zako zote. Yaweke mawazo yako yote kwenye kufanya kusudi la maisha yako na utaweza kuvuka magumu yoyote unayokutana nayo. Kila siku unahitaji kuyatuliza mawazo yako na kuhakikisha yapo kwenye kusudi la maisha yako, usiyaruhusu yakutoroke na uanze kufikiria vitu vya kukuondoa kwenye kusudi hilo.

16. Mwili wako ni zao la akili yako, afya yako ni matokeo ya mawazo yako. Magonjwa na changamoto nyingine za kiafya unazopitia, zinatokana na mawazo ambayo umeruhusu yatawale akili yako. Ukiweza kudhibiti mawazo yako, na ukajenga nidhamu ya maisha yako, afya yako itakuwa imara.

17. Kama unalalamika kwamba kazi yako inakuchosha, basi jua unafanya kazi ambayo siyo kusudi la maisha yako, na sahau kuhusu mafanikio. Unapofanya kazi inayotokana na kusudi la maisha yako, hakuna kitu kinaitwa kuchoka, utashangaa muda unapita lakini bado una hamasa ya kufanya. Uchovu tunaoupata kwenye kazi unatokana na mioyo yetu kuwa kinyume na kile tunachofanya, na hivyo kushawishi miili yetu ikatae kufanya kitu hicho, hapo ndipo unapata uchovu.

18. Mbingu na kuzimu ni hali ambazo zipo ndani ya mtu. Mtu anapokuwa mbinafsi na kujifikiria yeye mwenyewe, anayaona maisha yake kama kuzimu. Lakini mtu anapoachana na mawazo hayo, na kuanza kuona maisha ya wengine ni muhimu, anayaona maisha yake kama mbingu. Hivyo hali yoyote unayopitia sasa, hebu kaa chini na yakague mawazo yako. Ukishajua basi dhibiti mawazo yako ili maisha yako yawe mbingu na siyo kuzimu.

19. Mafanikio ya kweli kwenye maisha yanaenda kwa wale ambao ni WAADILIFU, WAAMINIFU, WENYE SHUKRANI NA UPENDO. Ni vitu vinne ambavyo vinaanzia ndani yako, haijalishi kama umetokea familia masikini au tajiri, haijalishi una elimu kubwa au ndogo. Unachohitaji ili kufanikiwa kwenye haya maisha ni UADILIFU, UAMINIFU, SHUKRANI NA UPENDO. Ukiweza kufanya maisha yako kuwa tabia hizi nne, ni lazima utafanikiwa, lazima.

20. Dunia inatupa sisi kila kitu, lakini bado dunia imejaa utajiri wa kutosha, hatuwezi hata kuumaliza. Lakini baadhi yetu tumekuwa tunakazana kupata kila kitu, lakini tunaishia kuwa masikini wakubwa. Hivyo siri ya utajiri ni sheria ya asili, toa kile ambacho unacho. Unapotoa kile ulichonacho, unatengeneza deni, na dunia lazima ikulipe kwa kile ambacho umetoa. Ni sheria, inafanya kazi mara zote na kwa kila mtu.

Nimalize uchambuzi huu kwa kukupa wazo moja muhimu ambalo hupaswi kulisahau wakati wowote ile. Mawazo yako ndiyo yanajenga au kubomoa maisha yako, hakuna bahati wala hakuna mchawi. Unapoona mambo hayaendi vizuri, anza kuyakagua mawazo yako, anza kuangalia mambo ambayo umekuwa unafanya, na utaona sehemu unayopaswa kurekebisha.
Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: