Habari rafiki?

Mwanzoni mwa wiki hii nilitoa taarifa ya semina kubwa tutakayofanya kwa njia ya mtandao ya kwenda kuuanza mwaka 2017. Kama ambavyo kila mtu anajua, tunauaga mwaka 2016 na tunaukaribisha mwaka 2017. Kwenye maelezo ya semina hii, nilisema mwaka 2017 tunakwenda kufanya kitu cha tofauti, kitu ambacho hatujawahi kukifanya na ambacho kitatuwezesha kuwa na mafanikio makubwa sana kwenye maisha yetu mwaka huo 2017.

 

Kitu hicho kikubwa ni kutokuishi kwa malengo mwaka 2017, ndiyo umesoma sahihi kabisa na maneno hayo yanatoka rafiki yako Makirita, kwamba MWAKA 2017 TUNAKWENDA 
KUISHI BILA YA MALENGO. Badala ya malengo tutakwenda kujaribu kitu kipya ambacho kitayafanya maisha yetu yawe na ukamilifu wa kipekee.

Baada ya kutuma ujumbe huu wa semina marafiki wengi wameniandikia wakishangazwa na maamuzi haya. Wengi hawakutegemea kabisa kwamba mimi rafiki yao, ambaye nimekuwa nawahamasisha kila mwaka kuweka malengo na kuyafanyia kazi, leo nakuja kuwaambia wasiweke malengo, yaani waanze mwaka bila ya malengo!

Nimepokea ujumbe kutoka kwa wasomaji wengi juu ya hili, na mmoja ameniambia wazi kwamba nataka kumvuruga, nimeweka ujumbe wake hapa chini;

Asante sana kocha Makirita kwa namna unavyojitoa kutuelimisha. Tunajifunza mengi ya maana kupitia kwako, tuyatekeleze au la wewe umenawa mikono, hakuna aliyesoma makala na mafundisho yako atayakosa mafanikio akarudi kukulaumu kana kwamba wewe ndio chanzo cha kutofanikiwa kwake. Lakini leo unataka kunivuruga. Nimeanza kusoma ushauri, makala na mafundisho yako tangu mwezi wa nne 2016 kama sikosei, ni mmojawapo wa watu nilioishi bila mipango maisha yangu yote, nina miaka 14 kazini, nina miaka 11 katika ndoa, nilioanza nao kazi wengi wana maisha mazuri kuliko mimi, wengine vijana wadogo nimewapokea kazini lakini leo wana maisha ya kupigiwa mfano. Nilijificha kwenye kichaka eti kwamba mimi nina majukumu mengi kuliko wao, hata nimediriki kuwaambia majukumu yangu nikiwakabidhi hawatayaweza, Kumbe nimepoteza muda bure. Nimesema leo umeanza kunikorofisha kwa kuwa kwa ushauri wako nimeshapanga mipango yangu ya kutekeleza mwaka 2017,harafu leo useme tena tutembee 2017 bila kuwa na malengo? Hainiingii akilini, badili wazo la semina. Ni ushauri tu.

Huyu ni mmoja kati ya marafiki wengi mlioniandikia kuhusiana na tangazo la semina ya mwaka 2017 ambapo tunakwenda kuishi mwaka 2017 BILA YA MALENGO.

Naomba leo nichukue nafasi hii kuweka mwanga zaidi juu ya kuishi mwaka 2017 na miaka mingine mingi ijayo bila ya malengo.

Kwanza nianze kwa kusema kwamba, maisha yangu mpaka hapa nilipofika sasa, ni kwa sababu ya utamaduni wa kujiwekea malengo. Kwa mara ya kwanza nilianza utaratibu wa kuwa na malengo ya kujiandikia mwaka 2007, na karibu kila mwaka nimekuwa na malengo ambayo nimeyaandika kwenye kitabu changu cha mwaka.

Mwaka huu 2016 tulianza na semina ya kuweka malengo ya mwaka huu, na mpaka sasa tuna kundi la wasap ambapo kila siku asubuhi tunaandika na kushirikishana malengo yetu ya mwaka mpya. Hivyo nakiri kabisa kuweka na kuishi kwa malengo kumekuwa na faida kubwa sana kwangu.

Lakini kama ambavyo unanijua mimi rafiki yangu, naamini katika kitu kimoja, kwamba kulingana na ninavyopaswa kujua, basi ni sawa na sijui kabisa. Hivyo kila siku kwangu ni siku ya kujifunza. 

Na kama ambavyo nimekuwa nakushirikisha mara kwa mara, kwamba popote nilipo sasa, na hata wewe ulipo, kuna nafasi ya kuwa bora zaidi.
Haya ni mambo mawili ambayo lazima tuishi nayo kila siku rafiki, kwamba;

1. KILA SIKU NI NAFASI NYINGINE YA KUJIFUNZA KITU KIPYA.

2. POPOTE ULIPO SASA, UNA NAFASI YA KUWA BORA ZAIDI LEO KULIKO ULIVYOKUWA JANA.

Ni misingi hii miwili muhimu inatufanya tunapiga hatua kwa pamoja kila siku rafiki. Ni misingi hii miwili ambayo kila siku naiishi na napata fursa za kupiga hatua na mambo mazuri ya kukushirikisha kupitia uandishi wangu na mafunzo mengine ninayotoa.

Kama unakumbuka siku za nyuma nimewahi kukuandikia makala kwamba tafiti zinaonesha kwamba sisi binadamu tunatumia chini ya asilimia kumi ya uwezo mkubwa tulionao ndani yetu. 

Yaani sisi tuna uwezo mkubwa mno, yaani mkubwa sana, lakini kiasi cha uwezo huu tunaokitumia sisi ni kidogo mno, naweza kusema kiduchu kabisa. Yaani ni sawa na unamiliki basi la kubeba abiria 100 kutoka dar kwenda arusha, lakini wewe kila siku unabeba abiria mmoja pekee. 

Unasafirisha basi tupu kabisa lakini wala hujui hivyo. Hivi ndivyo tukilinganisha uwezo wetu na matumizi yake yalivyo.

Sasa rafiki nataka nikupe siri kidogo ya jambo ambalo nimekuwa nalifanya kwa siri. Jambo hili ni kujifunza na kutafiti ni namna gani tunaweza kuongeza matumizi ya uwezo wetu. Yaani badala ya kutumia chini ya asilimia 10 ya uwezo wetu, angalau tufike hata asilimia 10 na zaidi. Ni katika hili ndipo nimekuwa najifunza mengi sana, ambayo nayafanyia kazi kwa uchache na naona matokeo yake ni mazuri.

Moja ya hayo ni hili la kuishi bila ya malengo, japo sijalijaribu kwa mwaka mzima, lakini nimefanya utafiti wa kutosha na kujiridhisha kwamba mwaka 2017 nitakwenda kuishi bila ya malengo. Na kwa kuwa nina marafiki ambao ninaongozana nao kwenye safari hii ya maisha, basi huenda nao wakapenda kujaribu hili. Ndiyo maana nikakushirikisha hili, kwa sababu najua ni kubwa na litakwenda kuleta mapinduzi makubwa kwenye maisha yetu.

Hivyo kwa wale watakaoshiriki semina, tutakwenda pamoja mwaka mzima. Tutakuwa na njia bora mbadala wa njia ya malengo, tutakuwa na namna bora ya kupima maendeleo yetu kwa mwaka huo 2017 na miaka mingi inayokuja. Kwa kifupi, 2017 utakuwa mwaka wa tofauti.

Hivyo rafiki, nikutoe wasiwasi, sina lengo la kumvuruga rafiki yangu yeyote, bali lengo langu ni kuyafanya maisha yetu kuwa bora zaidi. Na ili uweze kupata bora, lazima uikatae nzuri. Si unajua hilo rafiki? Kuwa na MALENGO NI HATUA NZURI, kutumia mbadala wa malengo ni 

HATUA BORA. Sasa chagua, unataka NZURI au BORA?

Kama unataka nzuri endelea na MALENGO kwenye mwaka 2017, kama unataka BORA, basi karibu kwenye semina ya 2017 MAFANIKIO MAKUBWA BILA YA MALENGO.

NAFASI ZA KUSHIRIKI NI CHACHE.

Rafiki yangu, ili kuyafanya mafunzo haya kuwa bora kwa kila atakayeshiriki, nafasi za kushiriki semina hii zitakuwa chache. Nitaweza kuendesha kundi moja tu la wasap kwa ajili ya semina hii. 

Hivyo kundi likishajaa, hutaweza kupata tena nafasi ya kushiriki semina hii. Sikuambii hivi ili kukuhamasisha ulipie mapema, ila nakupa taarifa hii mapema ili nitakapokuja kukuambia kwamba nafasi zimejaa, usiniambie kwamba kwa nini sikukupa taarifa mapema. Hivyo kujihakikishia kushiriki semina hii, lipa ada yako mapema.

JARIBU SEMINA HII BURE KABISA, BILA YA KULIPA CHOCHOTE.

Kama ambavyo nimekuwa nakuambia rafiki yangu, kila ninachofanya nayaweka maisha yangu yote kwenye kitu hicho, hivyo huwa nahakikisha naweka kila ninachoweza kutimiza kile ninachoahidi. Semina hii utalipia ada, kama nilivyoelekeza kwenye taarifa ya kwanza, na nitaeleza pia hapo chini.

Lakini kama wewe uko njia panda iwapo utapata thamani halisi ya fedha unayolipa, nakushauri lipa, shiriki semina halafu mwisho kama utaona haijawa na msaada wowote kwako, niambie na nitakurudishia fedha yako, bila ya kukuuliza swali la ziada. Nasema hili nikimaanisha rafiki, lengo langu ni wewe upate thamani kupitia kile ninachotoa, ili maisha yako yaweze kuwa bora zaidi.

Rafiki, maelezo kamili kuhusu semina pamoja na masomo yatakayofundishwa yapo hapo chini;

SEMINA; 2017 MAFANIKIO MAKUBWA BILA YA MALENGO.

Semina ya siku 10; 04/01/2017 – 13/01/2017

Semina itafanyika kwa njia ya mtandao wa wasap kupitia kundi la KISIMA CHA MAARIFA.

Mafunzo yatatolewa kwa njia ya maandishi na sauti.

Ada ya kushiriki semina ni kulipia ada ya uanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni tsh elfu 50 kwa mwaka (50,000/=).

Mwisho wa kulipa ada na kujiandikisha ni tarehe 02/01/2017.

Masomo ya semina;

Siku ya kwanza; karibu 2017, mwaka wangu wa mafanikio makubwa zaidi.

Siku ya pili; kauli tatu za kutuongoza mwaka huu 2017 na jinsi ya kuzitumia kufanikiwa.

Siku ya tatu; kwa nini malengo ni kikwazo kwa kuwa na maisha bora yenye furaha na mafanikio makubwa.

Siku ya nne; mbadala wa malengo, umuhimu wa mfumo na jinsi ya kutengeneza mfumo wa maisha.

Siku ya tano; mfumo wa mafanikio ya kifedha, ondoka kwenye madeni na anza kuwekeza.

Siku ya sita; mfumo wa mafanikio ya kikazi, fanya makubwa kwenye kazi na/au biashara yako 2017.

Siku ya saba; mfumo wa mafanikio ya kiafya, mwongozo muhimu wa kuwa na afya imara kwa ajili ya mafanikio.

Siku ya nane; mfumo wa mafanikio ya kifamilia na kijamii, wape nafasi wale muhimu kwenye maisha yako.

Siku ya tisa; mfumo wa kuweza kupambana na changamoto yoyote utakayokutana nayo mwaka 2017 ili isikuzuie kufanikiwa.

Siku ya kumi; mambo 10 muhimu ya kuepuka kwa mwaka huu 2017 ili kuweza kuwa na maisha ya mafanikio.

Hivi ndivyo tunavyokwenda kuuanza mwaka 2017 pamoja rafiki, nitahakikisha kwa pamoja tunafanya makubwa sana mwaka 2017.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK