Habari za leo rafiki yangu?
Ni matumaini yangu kwamba uko vizuri sana na upo tayari kwa mwaka 2017. Ni imani yangu kwamba yapo mambo makubwa uliyojifunza kwenye mwaka huu 2016 ambayo utakwenda kuyaboresha zaidi mwaka 2017 ili maisha yako yaweze kuwa bora zaidi.
Kumbuka jukumu letu kuu la kwanza ni kuhakikisha maisha yetu 
yanakuwa bora, yenye furaha na mafanikio makubwa. Mambo haya yakishaanza na sisi wenyewe, basi tunaweza kutoa mchango mkubwa kwa wale wanaotuzunguka.
Rafiki yangu, leo napenda kuchukua nafasi hii kukufahamisha kwamba kwa wiki moja, kuanzia ijumaa ya tarehe 23/12/2016 mpaka alhamisi ya tarehe 29/12/2016 nitakuwa na likizo yangu ya mwaka huu 2016.
Umekuwa ni utaratibu wangu kila mwisho wa mwaka kuchukua wiki moja ya likizo na kuwa mbali kabisa na kazi zangu nyingi. Ndani ya wiki hii siyo kwamba nalala au kuburudika, badala yake napata muda wa kutosha wa kupitia kila ambacho nimefanya kwa mwaka unaoisha na kisha kusuka mikakati ya mwaka unaofuata.
Katika wiki hii moja ya likizo, nimekuwa napata nafasi ya kutosha ya kupitia kwa undani na pia kujifunza kwa undani katika maeneo ambayo nakuwa nimeyachagua. Ni likizo hizi za kila mwaka ambazo zimeniwezesha kuja na wazo la KISIMA CHA MAARIFA, kuja na mawazo ya makala za tofauti na hata mawazo ya vitabu.
Naweza kusema wiki hizi ninazochukua likizo ya kuzama zaidi kwenye maisha yangu na kazi zangu, zimekuwa ni wiki zenye mchango chanya kwenye maisha yangu na ya wale wanaonizunguka.
Mwaka huu nina mambo muhimu ninayokwenda kufanya kwenye wiki hii ya likizo. Ya msingi kabisa ni kuuangalia vizuri mwaka 2016 ulivyokwenda kwangu na kwa kazi zangu. Na pia kuuangalia vizuri mwaka 2017 na kuweka mikakati ya kuufanya kuwa mwaka bora sana.
Licha ya hili pia nitapata nafasi ya kufanya meditation kwa undani zaidi, nitapata siku saba za kufanya meditation ya kuzama kabisa kwenye utulivu. Hii inanisaidia sana kuweza kudhibiti hisia na pia kukua kiroho.
Katika wiki hii ya mwaka huu pia nitajipa changamoto ya kusoma vitabu viwili kila siku. Lengo ni kusoma kurasa 500 kila siku kwa siku saba mfululizo. Kwa kuwa vitabu vya kawaida wastani ni kurasa 200 mpaka 300, kwa lengo la kurasa 500 kila siku ni vitabu 2 kwa siku. Nikiri wazi ya kwamba sijawahi kufanya hili, hivyo nakwenda kulijaribu katika likizo hii ya wiki moja ya mwaka huu. Changamoto kubwa niliyowahi kujipa ni ya kusoma kitabu kimoja kwa siku kwa siku saba mfululizo.
Kwa nini kurasa 500 kila siku?
Siku moja Warren Buffet, bilionea mwekezaji aliulizwa swali na kijana mmoja, kijana huyo alitaka kujua afanyeje ili na yeye aweze kuwa na mafanikio makubwa kwenye maisha yake? Buffet alichukua karatasi akamwambia unaona hii, basi sima kurasa kama hizi zisizopungua 500 kila siku.
Juma lililopita, rafiki yangu Daudi Mwakalinga, kwenye kundi letu la kusoma vitabu, alitushirikisha maandiko ya mfanyabiashara Strive Misiyiwa, huyu ni mfanyabiashara raia wa Zimbabwe ambapo alikuwa akijibu swali la kijana aliyeuliza asome vitabu vingapi, na yeye alimjibu vitabu viwili kwa siku, angalau kurasa 500.
Na mimi naichukua changamoto hiyo, kurasa 500 za vitabu, kila siku. kwa kuanza siku hizi saba za likizo, baada ya hapo utakuwa utaratibu wa kawaida kabisa.
Nichukue nafasi hii kukutakia kila la kheri kwenye sikukuu zinazokuja. Krismasi na mwaka mpya. Nikukumbushe ya kwamba usisherekee na kusahau kwamba maisha yanapaswa kuendelea.
Katika wiki hii moja ya likizo sitakuwa napatikana hewani kwenye wasap, email. Kwa simu nitakuwa napatikana kwa uchache sana.
Katika kipindi hiki cha likizo, makala pekee zitakazokwenda hewani kila siku ni makala za KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO kwenye KISIMA CHA MAARIFA.
Nikukumbushe ya kwamba semina ya 2017 MAFANIKIO MAKUBWA BILA YA MALENGO itafanyika kuanzia tarehe 04/01/2017 na mwisho wa kulipia ili uweze kushiriki semina hii ni tarehe 02/10/2017. Semina itafanyika kwa njia ya mtandao wa wasap. 
Tutakwenda kujifunza mengi na ninakuhakikishia, mwaka 2017 tutakwenda pamoja, bega kwa bega kuhakikisha hupotezi mwaka huu w akipekee sana kwako. Kupata maelezo zaidi ya semina hii bonyeza maandishi haya.
Lipia mapema ili ujihakikishie kushiriki semina hii bora sana kwa mwaka 2017.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.