Habari za leo rafiki yangu?
Jana tarehe 02/01/2017 ilikuwa ndiyo siku ya mwisho ya kulipia ada ya kujiunga na semina ya 2017 MAFANIKIO MAKUBWA BILA YA MALENGO. Kama tayari ulishatuma ada na bado hujawekwa kwenye kundi la KISIMA CHA MAARIFA wasap nitumie ujumbe wenye majina yako kamili kwenye namba 0717396253 kwa njia ya wasap. Pia jana kuna baadhi ya watu walipata changamoto wakati wa kulipia na kuambiwa muamala umefeli, kama ilikutokea hiyo tuwasiliane leo. Vinginevyo niwakaribishe sana wale wa semina na niwatakie wengine mwaka mwema na wenye mafanikio makubwa, tutaendelea kuwa pamoja kila siku kupitia AMKA MTANZANIA tukipeana maarifa muhimu kwa mafanikio yetu.

Leo nakwenda kukushirikisha kitu muhimu sana kwa mafanikio yako, huu ni uchawi muhimu ambao unapaswa kuwa nao ili uweze kufanikiwa. Kwa uchawi huu hakuna kitakachokuzuia wewe kufanikiwa. Kwa wale wanaoogopa na kuona labda nataka kukufundisha kuloga, hapana sifanyi hivyo, nataka nikupe mbinu ya kuweza kutumia vizuri akili yako kwa faida zako.

Nimepata wazo hili la uchawi baada ya msomaji mwenzetu mmoja kuniandikia akiniambia kwamba anafikiri yeye ana pepo maana kila akipata fedha ndiyo zinapigwa simu za ndugu wa karibu ambao wana matatizo mbalimbali, hivyo inabidi awasaidie na hivyo fedha anazokuwa amepata zinaisha. Ila anachoshangaa ni kwamba akiwa hana fedha simu nazo hazipigwi.

Nilimjibu kwamba huna pepo wala chochote, bali alichonacho ni nidhamu mbovu ya fedha na maisha kwa ujumla. Hivyo anachohitaji siyo kuondolewa pepo, bali kujijengea nidhamu nzuri ili kuweza kufika kule anakotaka kufika.

Hivyo uchawi ninaokwenda kukushirikisha leo rafiki yangu siyo mwingine bali ni NIDHAMU.

Nimekuwa nikiwasiliana na watu, nikiwashauri na kuwaongoza kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yao kwa karibu miaka minne sasa, na kikubwa ambacho najifunza ni kwamba ukosefu wa nidhamu ni kikwazo kikubwa sana. Maarifa wengi wanayo, hamu ya mafanikio wengi wanayo, wanachopaswa kufanya wengi wanajua, ila tatizo ni nidhamu ya kuweza kufanya.

Watu wengi wanajua ya kwamba njia ya uhakika ya kupunguza uzito wa mwili ni kufanya mazoezi, mara kwa mara. Lakini mbona hawafanyi? Watu kwa makusudi wanachagua kutokufanya mazoezi, au wanachagua kula hovyo. Yote hii ni kwa sababu wanakosa nidhamu ya kufanya kile ambacho ni sahihi au nidhamu ya kutokufanya kile ambacho hawataki kufanya.

Kwenye mafanikio pia, wengi wanajua mafanikio yanahitaji kujituma, kujitoa, uvumilivu na muda. 

Lakini bado wengi hawafanyii hayo kazi. Tatizo kubwa hapo ni nidhamu.

Nidhamu ni muhimu sana kwenye mafanikio yako. Na nidhamu tunayozungumzia hapa siyo ya kunyenyekea na kusalimia, bali ule uwezo wa kufanya kile ambacho unapaswa kufanya, bila kuzuiliwa na sababu yoyote, na kutokufanya kile ambacho hutaki au hupaswi kufanya, bila ya kuruhusu sababu iingilie.

Sijui umenielewa vizuri rafiki, unapanga kile ambacho unahitaji kukifanya, halafu unaanza kukifanya, bila kuruhusu sababu ya aina yoyote ile ikuzuie wewe kufanya ulichopanga kufanya. 

Unapoanza kufanya yale yanayokupeleka kwenye mafanikio, sababu nyingi za kukurudisha nyuma zitajitokeza, unahitaji nidhamu ili kuweza kuendelea kufanya licha ya sababu zinazojitokeza.

Pia kama kuna kitu ambacho hutaki kufanya, hukifanyi. Hili pia linahitaji nidhamu kwa sababu kuna msukumo mkubwa wa kijamii ambao unaweza kukufanya ufanye yale ambayo hutaki kufanya kwa sababu tu kila mtu anafanya. Unahitaji nidhamu ya hali ya juu kuweza kushinda msukumo huu wa kijamii, kwa sababu ni rahisi kuona kwamba wewe ndiye unayekosea na kutamani kujiunga na kundi kubwa. Kwa mfano mara nyingi unajikuta unafanya yale mambo ambayo wanaokuzunguka wanayafanya, hata kama hujui kwa nini unayafanya, au hayana faida kwako.

Hivyo uchawi ambao kila mmoja wetu anapaswa kuwa nao ni nidhamu binafsi, nidhamu ya kuweza kujisimamia kwenye kile unachofanya, nidhamu ya kukuondoa kwenye sababu zinazokuzuia kufanikiwa.

Swali ni je unawezaje kujijengea nidhamu binafsi?

Hapa nako pia hakuna uchawi, bali unahitaji kujijengea tabia ya kufanya. Panga kile unachotaka, na anza kuchukua hatua hata kama ni ndogo sana. Chukua hatua kwa chochote unachotaka, usisubiri mpaka mambo yawe mazuri, mambo huwa hayawi mazuri hata siku moja, kila wakati kuna changamoto zake.

Usikubali sababu yoyote ikuzuie kuchukua hatua. Pale unapopanga kufanya kitu, mara moja zinakuja sababu za kwa nini huwezi kufanya kitu hicho, au unaona vitu vingine muhimu zaidi vya kufanya. usiruhusu hili likutokee, badala yake weka sababu pembeni na fanya. Fanya hata kwa hatua ndogo kabisa, kadiri unavyofanya ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi nzuri ya kuendelea kufanya.

Mwisho kabisa usifanye kitu ambacho hutaki kufanya. Katika kila kitu unachofanya kwenye maisha yako, kwanza jiulize kitu hicho kina msaada gani kwako au kwa wale wanaokuzunguka. 

Halafu jiulize je unataka kufanya kitu hicho? Je ni kitu chenye manufaa kwako na wale wanaokuzunguka? Kama jibu ni hapana, basi usikifanye, hakina faida kwako na kinakuzuia kufanya yale ya muhimu. Hapa panaweza kuwa pagumu kwa sababu utahitaji kuwaambia watu HAPANA, lakini jifunze kutumia neno hilo mara kwa mara, litakupa uhuru mkubwa sana.

Nidhamu ni muhimu mno, bila ya nidhamu huwezi kupiga hatua yoyote kwenye maisha yako.

Nikimalizia kwa kile alichoniandikia msomaji mwenzetu kwamba simu zinakuwa nyingi anapokuwa na fedha, lakini zikiisha simu haziji, ni kukosa nidhamu nzuri ya kifedha. Kwanza kabisa kwenye kila kipato unachopatwa, hupaswi kukitumia chote, asilimia kumi ya kipato unachopatwa unapaswa ujilipe wewe mwenyewe kwanza. Usiruhusu kiwango hicho kiwe na matumizi mengine yoyote, hii ni njia yako ya kununua uhuru wako, usikubali kuingilia kwa njia yoyote ile. Hivyo fanya matumizi yoyote utakayo na ile asilimia 90 ya kipato chako kinachobaki, ikiisha usijaribu hata kidogo kugusa ile asilimia 10. Kama ni watu watalala njaa basi na iwe hivyo, lakini usiguse sehemu ile ambayo umejilipa wewe mwenyewe kwanza. Na uzuri ni kwamba watu huwa wanapata njia mbadala, kama ambavyo kipindi huna fedha wana njia zao mbadala za kufanyia kazi matatizo yao.

Kujifunza zaidi kuhusu kujilipa wewe mwenyewe na ufanyie nini kile unachojilipa, soma hapa;  

Unawalipa Watu Wote Kasoro Huyu Mmoja wa Muhimu

Unahitaji nidhamu binafsi,

Unahitaji nidhamu ya fedha,

Unahitaji nidhamu ya muda,

Unahitaji nidhamu ya kufanya kile unachopaswa kufanya,

Unahitaji nidhamu ya kutokufanya kile ambacho hutaki kufanya.

Huu ndiyo uchawi wa mwaka 2017 ambao nimekukabidhi leo, ufanyie kazi kila siku, na hutabaki hapo ulipo sasa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.