Katika historia ya dunia, kitu kimoja kinaonekana wazi, kila ambacho kilikuwa kikubwa sana, kiliishia kuanguka. Ukianza na tawala mbalimbali, zilikuwepo tawala kubwa kama Athens, Roma, 

Misri na nyinginezo, lakini zote ziliishia kuanguka. Hata kwa upande wa biashara, zilikuwepo kampuni kubwa sana, ambazo zilikuwa zikiongoza dunia nzima kwa uzalishaji na faida, lakini ziliishia kuanguka.

 

Mwandishi Jim Collins amekuwa akifanya tafiti kwa kuangalia nini kinafanya baadhi ya kampuni kuweza kukua kuanzia chini mpaka juu, kuweza kudumu na kwa nini nyingine zinashindwa kukua au kuanguka zinapokua. Katika kitabu chake hichi cha HOW THE MIGHTY FALL anatushirikisha utafiti aliofanya kupitia makampuni makubwa ambayo yalikufa. Pia ameangalia mengine ambayo yameweza kudumu na yale ambayo yaliweza kuinuka tena baada ya kuonesha dalili za kufa.

Japo kitabu hiki kimeandikwa kwa utafiri wa makampuni, lakini sababu hizi zinapelekea kila kikubwa kuanguka. Kwa mfano kwenye utawala wa nchi, uongozi na hata kujijengea jina binafsi. 

Tumekuwa tunaona wasanii ambao wanapata umaarufu sana wanaishia kupotea kabisa, sababu zinazowapoteza zimeelezwa vizuri kwenye kitabu hichi.

Karibu tujifunze kwa pamoja sababu zinazopelekea wakubwa kuanguka ili na wewe usizirudie kwenye kazi zako, biashara zako na hata maisha yako kwa ujumla.
Yafuatayo ni mambo muhimu niliyojifunza kupitia kitabu hichi;

1. Kila kitu ambacho ni kikubwa, iwe ni taifa kubwa na imara, kampuni kubwa na inayoongoza, mfanyabiashara mkubwa au hata msanii maarufu, unayo hatari ya kuanguka. Na kadiri unavyokwenda juu, ndivyo anguko lako linavyokuwa kubwa. Lakini wengi wanaokuwa juu husahau kuna kuanguka, wanafanya makosa na kujikuta wameanguka.

SOMA; Mambo Kumi (10) Muhimu Ya Kuzingatia Kabla Hujafunga Ndoa Na Utajiri.

2. Kila anguko la taasisi kubwa, linafuata hatua kama ugonjwa. Mtu haanzi kuumwa mara moja na kufa hapo hapo, bali kunakuwa na dalili za awali za ugonjwa, ambazo mara nyingi huwa zinapuuziwa. Kadiri dalili hizi zinavyoendelea kuwepo, ndivyo mwili unakuwa dhaifu na siku moja unaanguka kabisa. Hivyo kujua dalili mapema na kuchukua hatua, kunazuia kifo.

Zipo hatua tano ambazo anguko huwa linapitia, kila hatua ni dalili za kuelekea kwenye kifo. Hatua hizo ni kama ifuatavyo;

3. Hatua ya kwanza; KIBURI CHA MAFANIKIO.
Taasisi kubwa huanza kupata kiburi kwa yale mafanikio makubwa ambayo wanakuwa wameyapata. Kutokana na mafanikio makubwa ambayo wanakuwa wamepata, wanasahau kwamba kuna juhudi kubwa walifanya kufika pale, wanasahau kwamba kuna wakati walipata bahati fulani zinawafikisha pale. Badala yake wanaanza kujisifia kwamba wao ni wao, wao ni wajanja na wamefika pale kwa juhudi zao wenyewe.

Kiburi cha mafanikio kinawafanya waliofanikiwa kusahau kilichowafikisha pale walipo, wanaanza kufanya makosa na kujikuta wakianguka.

4. Hatua ya pili; KUJARIBU MAMBO MAPYA WASIYOYAJUA VIZURI.
Taasisi na wale ambao wanafanikiwa na kufika juu, hupata kiburi cha mafanikio, na kuona kwa kuwa wamefanikiwa kwenye kile wanachofanya, basi wanaweza kufanikiwa kwenye chochote. Wanasahau kwamba iliwachukua muda kujua vizuri kile wanachofanya sasa, wanasahau kwamba kuna mengi ya kujifunza popote pale. Kiburi cha mafanikio kinawafanya waamini wanaweza kufanya chochote na kufanikiwa popote.

Kwa njia hii wanajikuta wakijitanua kwenye maeneo mapya, ambayo hawana uelewa wa kutosha na kuanza kupata hasara au kupoteza. Hatua hii ina madhara zaidi kwenye kampuni au taasisi kuliko hatua ya kwanza.

5. Hatua ya tatu; KUKANUSHA HATARI YA KUANGUKA.
Taasisi au kampuni inapoanza kujitanua zaidi ya uwezo wake, vinaanza kujitokeza viashiria vya hatari ya kuanguka. Mara nyingi viashiria hivi huanzia ndani, wakati kwa nje kampuni inaonekana iko vizuri kabisa. Kwa ndani mambo yanaanza kuonekana magumu, wanakosekana watu muhimu wa kushika nafasi muhimu na changamoto nyingine. Lakini kwa kuwa kwa nje kampuni inaonekana ipo vizuri, basi watu wanakataa na kukanusha hatari ya kuanguka.
Hii ni hatua muhimu sana kama kampuni inataka kujiokoa, lakini wengi huwa hawaoni.

SOMA; Acha Kuamini Sana Juu Ya Kitu Hiki Katika Maisha Yako, Ili Utengeneze Utajiri Mkubwa Ulionao.

6. Hatua ya nne; KUANZA KUTAFUTA UKOMBOZI.
Baada ya hatua ya tatu kwenda kwa muda, hatari inaanza kuonekana mpaka nje sasa. Yale mambo ambayo yalikuwa yanaonekana yapo vizuri yanaanza kuonekana wazi kwamba hayapo vizuri. Na hapa ndipo watu huanza kuhangaika ili kujinusuru.

Tatizo la hatua hii ni kwamba hatua zinazochukuliwa siyo za kutatua tatizo la msingi, bali kubadilisha hali ya nje ionekane vizuri. Hivyo taasisi au kampuni inaweza kuja na njia mpya zinazoonekana ni nzuri, lakini hazisaidii tatizo la msingi ambalo linapelekea kufa.
Pamoja na juhudi hizo za kutafuta ukombozi, taasisi inaendelea kufa.

7. Hatua ya tano; KUINGIA RASMI KWENYE ANGUKO.
Kampuni inayofika hatua ya nne, inaweza kujitahidi na kuja na hatua mpya za kutaka kubadili mwonekano wa nje, lakini ndani bado mambo yanazorota. Hapo ndipo kifo kinapowadia na inakuwa vigumu sana kujinasua kwenye hatua hii. Kufikia hatua hii ni kwamba kampuni au taasisi inaelekea kwenye kifo kabisa, inasahaulika na hakuna namna inaweza kurudi kwenye zama zake.

8. Hatua hizi tano zinapitiwa na taasisi na kampuni nyingi ambazo zinakufa, na hata tawala pia, wasanii na watu binafsi ambao wanakuwa wamefika hatua za juu na kuporomoka. Wakati mwingine siyo lazima hatua hizo zifuatwe moja baada ya nyingine, kuna ambao wanatoka hatua ya tatu na kwenda hatua ya tano moja kwa moja. Pia kwenye kila hatua, kasoro hatua ya tano, kampuni inaweza kubadilika kama ikijua tatizo halisi na kulifanyia kazi.

9. Ili kubaki kwenye mafanikio yoyote ambayo umeyafikia, iwe ni binafsi au kama taasisi, lazima uendelee kuweka juhudi zile zile ambazo uliziweka wakati unaanza. Watu wengi wamekuwa na juhudi kubwa sana wanapoanza, lakini wakishafanikiwa wanajisahau na kupunguza juhudi, hapa ndipo anguka linawajia na kujikuta wakipotea.

10. Tatizo la kuanguka ni kwamba, watu wanaondoka kwenye kile cha msingi walichokuwa wanafanya, wanadanganyika na kujaribu mambo mapya na wasiyoyajua, wanatumia rasilimali nyingi kwenye mambo hayo mapya, wanashindwa kwenye hayo mapya na huku yale ya zamani yakiathirika kwa kukosa rasilimali. Hivyo unapofanikiwa, hata kama utajaribu mapya, usisahau yale yaliyokufikisha pale ulipo sasa.

11. Je ni wakati gani sahihi wa kuacha ulichokuwa unafanya awali na kufanya kipya? Maana kubaki na kile kilichokufikisha hapo pia siyo suluhisho, unaweza kushindwa kwa kung’ang’ana na vilivyopitwa na wakati. Kujua wakati sahihi kwako, jiulize maswali haya mawili;
Swali la kwanza ni je kile unachofanya kina hatari ya kufa na kupotea ndani ya miaka mitano ijayo?

Swali la pili ni je umepoteza ile hamasa uliyokuwa nayo mwanzo kwenye kile unachofanya?
Kama majibu yako ni hapana, basi endelea kufanya. Na kama majibu yako ni ndiyo basi angalia kipya cha kufanya, ambacho unaweza kuwa bora.

12. Jua sababu sahihi zilizopelekea wewe kufanikiwa na usizisahau kamwe. Kwa sababu hatua ya kwanza kabisa ya kuanguka ni kiburi, na kiburi huanza pale unaposahau ulipotoka. Hakikisha husahau ulipotoka, hakikisha husahau juhudi kubwa ulizoweka, hakikisha husahau kuna vitu ambavyo vilitokea kwako kama bahati, hukustahili kupata au juhudi zako binafsi zisingekuletea vitu hivyo. Ukikumbuka hayo kila wakati utakuwa mnyenyekevu na kuendelea kuweka juhudi.

13. Kamwe usiache kujifunza kuhusiana na kile kilichokufikisha hapo ulipo. Kufanikiwa kumekuwa kunawafanya wengi waone wapo bize na hawana tena muda wa kujifunza. Lakini ukweli ni kwamba unapofanikiwa, moja ya vitu unahitaji kuongeza basi ni kujifunza. Hivyo tenga muda wa kuendelea kujifunza na hakikisha hufiki mahali na kujiona tayari unajua kila kitu.

14. Ni muhimu kukua zaidi hasa unapofanikiwa, unahitaji kujaribu maeneo mapya, lakini usifanye hivyo kwa kuamini unaweza kufanikiwa popote. Kufanikiwa eneo moja la biashara haimaanishi unaweza kufanikiwa kila mahali. Na hata kufanikiwa kwenye biashara moja hakumaanishi unaweza kufanikiwa kwenye kila biashara. Ingia maeneo mapya ambayo kweli unaweza kuweka juhudi, na kuwa tayari kujifunza.

15. Unapojiingiza kwenye maeneo mapya baada ya kufanikiwa kwenye maeneo mengine, usisahau yale maeneo uliyofanikiwa. Maana wengi wanaoanguka hupeleka rasilimali zao zote kwenye maeneo mapya na kusahau kule walikofanikiwa. Wanakutana na ugumu kwenye maeneo mapya, na wakati huo kule walikofanikiwa kunakuwa kumeathirika na kukosa rasilimali. Hivyo unaweza kuanza mapya, lakini usisahau msingi wako wa mafanikio.

16. Kitu kingine kinachopelekea kampuni au taasisi zinazokua kufa, ni kukosa watu sahihi kwa maeneo sahihi ya taasisi hizo. Sheria ya Packard inasema kwamba, hakuna kampuni inayoweza kuendelea kukua kwa kasi kama haina watu sahihi wa kuendelea kuikuza kampuni hiyo. Wengi wa wanaokua kwa kasi wanafika wakati wanajikuta hawana watu sahihi wa kufanya majukumu muhimu ya ukuaji. Na hapo watu wasiokuwa na uwezo wanapewa majukumu makubwa wasiyoyaweza na kuishia kufa.

SOMA; Mambo 20 niliyojifunza kutoka kitabu cha The Innovator’s Dilemma

17. Kutumia ongezeko la bei kama kufikia gharama ni kitu kinachoua biashara na taasisi nyingi. Unakuta taasisi imekosa nidhamu na hivyo gharama za uendeshaji zinakuwa kubwa. Badala ya kukaa chini na kujua wapi wanafanya makosa ili kuyatatua na kushusha gharama za uendeshaji, wanachofanya ni kuongeza bei ya kile wanachotoa. Hapa gharama zinazidi kuongeleza, bei inaongezeka na wateja wanapungua, hii inapelekea kampuni au taasisi kushindwa kujiendesha.

18. Kampuni na taasisi nyingi zinapoanza kupata shida za ndani kwenye uendeshaji, lakini nje mambo yanakwenda vizuri, huacha kuangalia ndani na kuangalia nje. Wanaacha kuangalia tatizo lililopo na kujidanganya kwamba mambo yako vizuri, biashara inaenda vizuri, wateja wapo. Hali hii huruhusu yale matatizo ya ndani kukua zaidi na hatimaye kuathiri hali ya nje ya biashara. 

Usiruhusu tatizo lolote unaloliona likaendelea kuwepo, kadiri linavyochukua muda ndivyo linavyoathiri.

19. Kampuni inayoelekea kufa, haina tofauti na mtu anayezama kwenye maji. Wanasema mfa maji haishi kutapatapa. Watu wengi wanapogundua wanazama, basi huanza kutapatapa wakiamini hilo litawasaidia. Hii huwapelekea kuchoka haraka na kuzama kwa urahisi zaidi. 

Kampuni na taasisi pia nazo hutapatapa, hujaribu mambo mengi ya haraka haraka ili kwa nje ionekane mambo yako vizuri. Lakini wakati huo ndani kupo hovyo, na juhudi wanazochukua zinazidi kumaliza rasilimali za kampuni na kuharakisha kifo.

20. Kampuni zote ambazo zinashindwa kuchukua hatua mapema, zinafika hatua ya kifo kisichozuilika. Hapa ndipo inafika hatua kwamba hakuna juhudi yoyote inayoweza kufufua kampuni ambayo imefikia hatua ya kifo. Kama ukiwa unaifuatilia biashara yako kwa karibu, na ukawa makini na kila kinachoendelea, utaiokoa biashara yako isifike kwenye kifo kisichozuilika.

Kama nilivyokushirikisha kwenye utangulizi, kitabu hichi kimeandikwa kwa tafiti za makampuni na taasisi, lakini hatua hizo zinapitiwa na kila kilichopo juu na kuanguka. Chukua mifano ya wasanii, huanzia chini kabisa, wakijituma sana, kuwa tayari kufanya kazi na yeyote. Lakini baada ya kufikia mafanikio ya juu, wanasahau juhudi za mwanzo, wanaanza kujiita wao ndiyo wao na kuanza kudharau wa chini, kinachofuata baada ya hapo ni kifo.

Hali kadhalika kwa wale wanaoanzia kwenye umasikini, wanatajirika halafu wanapoteza utajiri na kurudi tena kwenye umasikini. Wakati wakiwa masikini walikuwa na unyenyekevu, walikuwa tayari kujituma, waliheshimu kila mtu na kujifunza. Inatokea bahati wanapata fedha nyingi, wanasahau kule walikotoka na kuona fedha ni zao na haziishi tena, wanazitumia hovyo kwa kuamini kila kitu wanakijua, wanafanya uwekezaji wa hovyo, wanapoteza kila kitu na kurudi kwenye umasikini.

Hichi ni kitabu muhimu kwa kila mtu kusoma maana kinaakisi kila eneo la maisha yetu.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita