Habari za leo rafiki yangu?

Linapokuja swala la fedha, kila mtu huwa anaona anajua zaidi. Nimewahi kusoma kichekesho kimoja kinasema kwamba hakuna mtu mgumu kushauriwa kama mtu mwenye fedha, hasa yule ambaye amezipata karibuni. Hii ndiyo hupelekea watu wengi kutumia vibaya vipato vyao, kujikuta kwenye madeni na hatimaye umasikini wa kupindukia.

 

Napenda sana kujifunza kuhusu fedha, na tabia za watu juu ya fedha. Hii imenisaidia kuona makosa ambayo wengi wanafanya kwenye fedha, na kujua namna bora ya kuepuka makosa hayo ili kutokuingia kwenye mashimo waliyoingia wengine.

Katika kujifunza kuhusu fedha, nimewahi kusoma mahali, kwenye mtandao wa intaneti, mtu mmoja aliyetoa ushauri rahisi kabisa kuhusu fedha. Mtu huyu alitumia uzoefu wake kwenye maisha yake binafsi, na alisema yeye ana miaka 57, amekuwa masikini na amekuwa tajiri, na yapo mambo 11 ambayo anamshauri mtu yeyote ambaye anataka kuweka sawa maisha yake hasa upande wa fedha. Sikumbuki jina la mtu huyu, wala sikumbuki nilisoma wapi, ila nakumbuka mambo haya 11 kwa sababu huwa nina tabia ya kuandika pembeni yale yote ninayojifunza. Leo katika kupitia mambo ya fedha, nimekutana na haya 11 na nimeona ni vyema nikushirikishe. Sitayaeleza sana, bali nitayataja kama alivyokuwa ameyataja mwenyewe. Yanaeleweka wazi kabisa na ni wewe tu kuchukua hatua.

SOMA; Njia Ya Uhakika Ya Kuondokana Na Madeni Sugu Na Kufikia Uhuru Wa Kifedha Kwenye Maisha Yako.

Karibu sana tujifunze kwa pamoja mambo haya 11 ambayo yataweza kukutoa kwenye madeni, na kukufikisha kwenye uhuru wa kifedha.

Nawasilisha kwako kama nilivyojifunza;

1. Ondokana na madeni yako yote, lipa kila deni unalodaiwa.

2. Usiingie kwenye madeni mapya, usinunue kitu chochote kwa mkopo.

3. Pale unaponunua kitu, kilipie hapo hapo, au haraka iwezekanavyo.

4. Weka akiba kwenye kipato chako, usitumie akiba hiyo kwa matumizi yoyote yale.

5. Achana na njia zote unazoambiwa zitakuletea utajiri wa haraka, ni utapeli na utapotezewa muda.

6. Usimkopeshe mtu yeyote fedha, itaharibu mahusiano yenu na itakupeleka kwenye umasikini haraka sana.

7. Usijaribu kubashiri kwenye soko la hisa, hakuna tofauti na kubashiri kwenye kamari.

8. Puuza hadithi zote za marafiki zako za namna gani maisha yao ni mazuri, asilimia 99 ni uongo.

9. Nunua au jenga nyumba ambayo unaweza kuimudu, usikazane kwa usichokiweza, mara zote jua mambo yanaweza kwenda tofauti na unavyopanga.

10. Fanya kazi unayoipenda, ifanye kwa mapenzi, toa thamani kubwa sana kwa wateja wako au mwajiri wako, na fedha itakuja.

11. Kuwa na mwenza ambaye anajua vizuri kuhusu fedha, na siyo anayefikiria kuzitumia tu.

SOMA; Jinsi Ya Kuondoka Kwenye Madeni Mabaya.

Mwisho kabisa anatuambia iwapo tutafuata ushauri wake, hatutakuwa na matatizo ya fedha kwenye maisha yetu. Na hilo nina ushahidi kwangu mwenyewe, nimekuwa nafuata hayo kabla hata sijayasoma kwake, na naona namna gani ukiwa na msimamo mzuri kwenye fedha, unavyoondokana na hofu za fedha.

Yarudie mambo hayo 11, yaandike mahali ambapo utaweza kuyasoma kila siku, na yaweke kwenye maisha yako. Baada ya muda utajikuta unaondokana kabisa na hofu za fedha, kwa sababu hutakuwa na madeni, utakuwa na akiba na kipato chako kitakuwa kizuri.

Kitu kimoja ambacho hakuweka kwenye orodha yake ambacho nakushauri sana uwe nacho ni kuwa na vyanzo vingi vya kipato. Unahitaji mifereji mingi ya kipato. Hivyo kuwa na biashara, wekeza na njia nyingine nyingi za kuongeza kipato. Ila kama alivyosema kwenye namba 5, epuka sana chochote unachoambiwa kitakuletea utajiri wa haraka. Mwingi ni utapeli na pia vitakupotezea muda. Nunua na usome kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ili uweze kujifunza zaidi kuhusu kuwa na mifereji mingi ya kipato. Kwenye kitabu hichi, ipo mifereji 8 ya kipato ambayo kila mtu anapaswa kuwa nayo. Kupata kitabu tumia mawasiliano haya; 0717396253. Karibu sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.