1. TUMIA WATAALAMU
Maendeleo ya sayansi na teknolojia katika fani mbalimbali duniani yameleta matokeo chanya katika maendeleo na ubunifu katika idara za ujenzi. Karne ya sasa hatujengi kwa mazoea tena, hali hii ndiyo imechochea kuzalishwa kwa wataalamu wa ujenzi duniani kote. Majengo ya kisasa yanajumuisha matumizi tofauti na yenye mifumo mbalimbali kukidhi matumizi halisi ya jengo husika. Ni muhimu sana kupata ushauri wa wataalamu kabla na wakati wa ujenzi wa nyumba ya ndoto zako. Kutokutumia wataalamu kutakuweka katika hatari usiyoijua, hii ni kutokana na wengi kujenga kwa mazoea kwa kujua au kwa kutokujua kuwa wana hatarisha uwekezaji wanaoufanya.
Nayasema haya kwa kuwa napata huzuni sana ninapowaona watanzania wakilalama pale linapotokea janga kwenye nyumba aliyoitegemea kuendeshea maisha yake na familia kwa ujumla ikiangamizwa kwa dakika kadhaa kwa sababu zilizoweza kuzuilika na kufahamishwa endapo angewashirikisha wataalamu wa ujenzi. Nakusihi sana ukumbuke jambo hili kabla hujaanza kutekeleza ndoto zako ili ufanikishe kwa uhakika na usalama zaidi.
2. UJUE MPANGO KAZI KABLA YA UJENZI
Jambo hili nimelisema sana na leo nalisema tena, ujenzi hugharimu fedha nyingi sana tofauti na wengi wanavyotarajia. Mchanganuo wa gharama na Mpango kazi ni dira ya rasilimali katika ujenzi.
Mpango kazi wa ujenzi ni silaha yenye nguvu sana kabla na wakati wa ujenzi, Ni muhimu sana kuunda na kuweka mtaalamu wa kuratibu mpango kazi ili kuepuka matumizi mabaya ya rasilimali ambazo zilipaswa kutumika na kukidhi mahitaji husika. Mpango kazi ni njia pekee itakayo kufanya utoe maamuzi sahihi kwa kila hatua ya ujenzi. Watu wengi wameishia njiani na kutofikia ndoto zao kwa wakati na sababu mojawapo huwa ni kutokuwa na mpango kazi uliyo sahihi. Katika ujenzi muda, fedha na ubora ni ngao na rasilimali pekee inayosimamiwa na wataalamu wa ujenzi kuhakikisha lengo linafanikiwa. Migogoro mingi inayotokana na ujenzi sababu kuu mojawapo huwa ni rasilimali fedha. Jipange vema katika fedha kabla na wakati wa ujenzi kuepuka changamoto zisizo na ulazima.
3. UJUE USIMAMIZI IMARA
Tatizo la usimamizi katika ujenzi limekuwa ni jambo mtambuka katika ufahamu wa watanzania wengi katika kufikia ubora wa majengo. Kwa kiasi kikubwa wengi hutafuta mafundi wenye uzoefu na kuwakabidhi kila kitu kuanzia mipango hadi usimamizi. Lakini changamoto kubwa ni mabadiliko ya haraka yanayotokea katika sayansi ya uhandisi ujenzi, mapinduzi ya usanifu majenzi yanayoendelea kutokea hapa Tanzania si kila mtu anaweza kuyamudu. Umuhimu wa kutumia wataalamu unabaki kuwa ni jambo la lazima katika usalama wa ujenzi wako. Karne ya sasa tunalazimika kufanya mambo kwa weledi zaidi, epuka ubadhirifu, wizi na matumizi mabaya ya rasilimali wakati wa ujenzi kwa kutumia wataalamu wa usimamizi majenzi. Uaminifu na ushirikiano katika ujenzi ni msingi wa mafanikio, hivyo ni lazima uzingatiwe kuepuka migongano isiyo na ulazima. Nayasema haya kwa sababu wengi wameumizwa sana na jambo hili, tatizo kuu ni kuweka wasimamizi wasio na weledi katika ujenzi, msimamizi asiye na weledi katika ujenzi atashauri na kusimamia asichokijua.
SOMA; Ufahamu Ujenzi Wa Gharama Nafuu Wa Nyumba Bora Za Kisasa
4. EPUKA UJENZI HOLELA
Kila jambo ndani ya jamii linaratibiwa na utaratibu fulani katika kukidhi vigezo vya ubora na usalama wa matumizi kwa watumiaji. Hata katika ujenzi zipo kanuni na taratibu mbalimbali zinazoratibu mfumo wa ujenzi ili kuweza kufikia ubora na usalama kwa watumiaji. Zipo bodi mbalimbali na taasisi za serikali zinazosimamia taratibu kuhakikisha ujenzi unazingatia vigezo vilivyowekwa ili kukidhi mahitaji husika. Lakini kwa kiasi kikubwa jambo hili limekuwa changamoto kubwa kwa watanzania wengi, wananchi wengi hawana uelewa mkubwa wa taratibu zinazopaswa kuzingatiwa kabla na wakati wa ujenzi. Katika hili wengi wameumia kwa kujua au kwa kutokujua.
Vilio vingi vimesikika na bado vitaendelea kusikika endapo hakutakuwa na mbinu mbadala wa kuhakikisha kila Mtanzania anajenga na kuishi sehemu salama. Ingawa kwa jambo hili tatizo lipo kwa pande zote, wasimamizi na wananchi kwa ujumla lakini bado tunayo fursa ya kujipanga upya katika kufanikisha tunaishi katika mazingira na makazi salama. Katika hili huna budi kufuata taratibu zote ili ufurahie maisha kwa kuwa ujenzi ni uwekezaji ambao unapaswa kuwa sehemu salama ili kuepukana na hatari zinazoweza kuepukika.
Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.
Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.
Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888
Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com
nawezaje kumjua mtaalamu kwa usahihi
LikeLike