Matatizo yote ambayo tunayapitia kama binadamu, chimbuko lake lipo ndani ya akili zetu wenyewe. Ni mawazo yetu ndiyo yanayotengeneza matatizo tunayopitia. Kushindwa kwetu kuelewa tofauti yetu na mawazo yetu ndiyo kunaongeza matatizo zaidi. Na tabia yetu kama binadamu ya kutafuta njia rahisi ya kupata tunachotaka, na kushindwa kuyaweka mawazo yetu pale tulipo kunatufanya tushindwe kutatua matatizo tuliyonayo.

 

Mwandishi na mwalimu wa kiroho Eckhart Tolle, ametupa suluhisho la chanzo hichi cha matatizo hayo. Na suluhisho ni SASA, kuwa sasa, kuyaweka mawazo yetu pale ambapo tupo sasa, kwa kile tunachofanya sasa, ndiyo suluhisho la matatizo yetu mengi. Kupitia kitabu hichi, Tolle anatuonesha nguvu iliyopo sasa, kwenye wakati tuliopo sasa. Ukiweza kuijua na kuitumia sasa, unaweza kufikia hatua ya juu kabisa katika ukuaji wa kiroho.
Karibu sana tujifunze kwa pamoja nguvu ya wakati uliopo na namna ya kuitumia katika ukuaji wetu wa kiroho.

1. Akili na mawazo yetu ni tatizo kubwa sana kwetu. Mawazo yetu mara zote yanaruka ruka kama kipepeo anaporuka kutoka ua moja kwenda ua jingine. Mawazo yetu yanaruka kutoka jambo moja kwenda jambo jingine. Tunafanya kitu hichi huku mawazo yetu yapo kwenye kitu kingine. Unakula huku ukifikiria kazi, unafanya kazi huku unafikiria mapumziko. Kwa namna hii akili yako haikai sehemu moja na huwezi kufanya vyema kile unachofanya. Suluhisho ni kuweza kuituliza akili, kuiweka pale ulipo sasa, kwa kile unachofanya.

2. Matatizo na hofu zinaanza pale tunapokuwa na mgogoro na nafsi zetu. Pale tunapokataa pale tulipo sasa, kwa kufikiria kule tulipotoka au kuangalia kule tunakokwenda. Akili na mawazo yako yanapokuwa kule ulipotoka na kule unapokwenda, lakini siyo pale ulipo sasa, basi kile unachofanya sasa kinakosa maana kwako. Inakuwa tu ni kama kitu cha kupita, kisicho na maana kwako, na hapo ndipo matatizo yote yanapoanzia.

SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Kinaitwa SELF-IMPROVEMENT 101.

3. Wale ambao hawajaupata utajiri wa kweli kwenye maisha, ambao ni kujitambua, kuwa na amani isiyotikisika, na kuwa na furaha isiyotegemea chochote, hawa bado ni ombaomba, bila ya kujali wana pesa na mali kiasi gani. Hawa huwa wanaangalia nje yao kupata raha za muda mfupi, kununua vitu ili kukubalika na wengine, kuonekana au kupendwa na wengine. 

Watu hawa ni omba omba kwa sababu hata wafanye nini, bado hawataridhika wala kuwaridhisha wengine. Hivyo wanaendelea kukimbiza vitu vya dunia mpaka wanakufa wakiwa hawajapata amani ya mioyo yao. Usiwe mmoja wa watu hawa.

4. Watu waliokomaa kiroho, waliopata maono makubwa ya kiroho, wanajua kitu kimoja, ambacho dunia ni kitu kimoja. Viumbe wote ambao tupo duniani, ni kitu kimoja. Wote tunaungana kiroho. Kwa kujua hili, utampenda na kumheshimu kila mtu na kila kiumbe. 

Hutaua siyo kwa sababu umeambiwa ni dhambi, ila kwa sababu unajua unajiua wewe mwenyewe. Hutabaka kwa sababu unajua unajibaka mwenyewe. Na huu ndiyo umuhimu wa kukua kiroho. Ukuaji wa kiroho ndiyo njia pekee ya kuondoa mateso na matatizo duniani.

5. Tatizo kubwa sana ni kwamba tunajitambulisha kwa mawazo yetu. Vile ambavyo tunafikiri, ndivyo tumejijengea maisha yetu. Kwa maana hiyo, ili utambulisho wetu uendelee kuwepo, lazima tuendelee kuwa kama tulivyo. Sababu kubwa kwa nini omba omba ataendelea kuwa omba omba hata apate nini ni kwa sababu ndani ya mawazo yake, anajitambua kama omba omba, na huu ndiyo utambulisho wake kwa wengine. Hivyo ataendelea kuulinda. Watu wamekuwa wanapata matatizo yale yale mara kwa mara, kwa sababu ndiyo utambulisho wao, ndiyo mawazo yaliyotawala maisha yao.

6. Akili zetu ni kifaa chenye nguvu sana kama kikitumiwa sawasawa, lakini kikitumiwa vibaya, ni kifaa hatari mno kuwahi kutokea. Angalia namna ukuaji wa teknolojia unavyokwenda, tumepata huduma bora sana za kufanya maisha kuwa bora, kutokana na wale wanaoweza kutumia akili zao vizuri. Lakini pia tumepata vitu hatari sana, kama silaha zinazoweza kuiangamiza dunia kabisa.

7. Tatizo la kutumia akili vibaya ni moja, tatizo kubwa zaidi ni kutokutumia akili kabisa. Yaani watu wengi, wanaendesha maisha yao, bila ya kutumia akili zao kabisa. Yaani wao wanaenda tu, wapo kimwili lakini kiakili hawapo kabisa. Watu hawa wanakuwa wametekwa na akili zao, zinawaongoza na kuwatumia, badala ya wao kuzitumia. Wanajikuta wakifanya mambo ambayo hata wao wenyewe wakitulia wanajiuliza hivi nilikuwa nawaza nini mpaka nikafanya vile. Kama umewahi kujikuta kwenye hali kama hiyo, jua akili ilikuwa inakutumia na siyo wewe kuitumia akili yako, kitu ambacho ni hatari sana.

8. Habari njema ni kwamba, unaweza kupata uhuru wa akili yako, unaweza kuikomboa akili yako na kuweza kuitumia badala ya yenyewe kukutumia wewe. Unaweza kuchukua hatua ya kwanza sasa, ambayo ni kuanza kusikiliza mawazo yako. Sikiliza sauti zinazopita kichwani kwako, kaa mahali utulie na ona namna mawazo yanavyopita kwa kasi kwenye akili yako. Usihukumu wala kujizuia, wewe sikiliza, na utaona namna akili yako inavyoruka ruka na kushindwa kutulia sehemu moja. Ukifanya zoezi hili utaanza kujitofautisha wewe na mawazo yako, na kuweza kurudisha umiliki wa akili yako.

9. Hatua ya kwanza na muhimu ya kuelekea kwenye ukuaji wa kiroho ni hii; jua kujitofautisha wewe na akili yako, jitofautishe wewe na mawazo yaliyopo ndani ya akili yako. Kila unapoweza unapoweza kuweka nafasi kati yako na mawazo yako, mwanga wa utambuzi unaingia ndani yako.

10. Kinachofanya akili na mawazo yetu kutengeneza matatizo kwenye maisha yetu, ni ule ufahari ambao tunakuwa tumejitengenezea, kitu kinachoitwa EGO. Mara nyingi unaumia siyo kwa sababu umeumizwa, ila ego yako inakuaminisha umeumizwa. Kwa mfano iwapo mtu amesema amekuambia kitu na hukusikia alisema nini, hutajali sana, utaendelea na yako. 

Lakini kama mtu huyo huyo atakuambia kitu na ukakisikia, na ukagundua amekutukana, itakuumiza sana. Kwa nini akutukane, amekuchukuliaje, anakudharau na mengine mengi. 

Hapo ego inakuwa kazini, kwa kuwa unajitambulisha kwa akili na mawazo yako basi unaona mtu kakuumiza.

11. Dawa ya ego ni kukua kiroho, na kuweza kukua kiroho, unahitaji kuweka mawazo yako pale ulipo sasa. Usiruhusu wewe kuwa sehemu moja na mawazo yakawa sehemu nyingine. Ukishaweza kuitumia akili yako, na kuyadhibiti mawazo yako, basi hakikisha yanakuwa pale ulipo, wakati wote.

12. Akili zetu zimetengenezwa kwenye mfumo wa kuweza kuishi, hivyo mara zote hufanya kazi ya kuhakikisha maisha yanaendeleaje. Mara nyingi mawazo yako ni kwenye wakati uliopita, ambapo unafikiria yale uliyofanya vibaya, kushindwa au kuharibu. Na pia unafikiria wakati ujao, mambo yatakwendaje na kama yatakuwa magumu zaidi. Kwa njia hii inakuwa vigumu kuwa pale tulipo kwa wakati huo. Hichi kimekuwa chanzo kikuu cha kukosa furaha na kushindwa kufanya vizuri chochote tunachofanya.

SOMA; The Most Successful Small Business In The World (Kanuni Kumi Za Kuwa Na Biashara Ndogo Yenye Mafanikio Makubwa.)

13. Kutumia wakati wa sasa haimaanishi unapuuza kabisa wakati uliopita, au huweki kabisa malengo na maono ya siku zijazo. Tumia yaliyopita kujifunza, ili usirudie makosa yale yale, lakini kuendelea kufikiria makosa uliyofanya, hakuna unachoweza kubadili. Na kwa siku zijazo, weka malengo, weka maono yako makubwa, lakini usiache kuishi sasa kwa sababu unaangalia maono ya siku zijazo. Usijiambie kama nikipata hicho ndivyo nitafurahi au maisha yangu yatakamilika. Hapo ulipo sasa tayari umeshakamilika, unapaswa kuwa na furaha popote pale ulipo, na ukiweza kuyaweka mawazo yako pale ulipo, utakuwa umekamilika.

14. Akili tunayozungumzia hapa siyo tu mawazo, bali hata hisia ambazo tunakuwa nazo. 

Hisia huzaliwa pale mawazo na mwili vinapokutana. Hisia ni mwitikio wa mwili kwenye mawazo yako, au taswira ya mawazo yako kwenye mwili wako. Kwa mfano mawazo ya kushambuliwa hutengeneza nguvu ya mwili kupambana na hili huzalisha hisia za hasira. 

Tafiti zinaonesha hisia kali zinatengeneza mabadiliko makubwa kwenye miili yetu, ikiwepo mwili kujiandaa kwa lile tunalotegemea litokee. Njia pekee ya kudhibiti hisia zetu, ni kudhibiti mawazo yetu. Na kama tutaweza kuyaweka mawazo yetu pale tulipo sasa, hisia hazitakuwa changamoto kwetu.

15. Mapenzi, furaha na amani ndiyo hali kuu ya ndani ya maisha yetu. Yaani hivi ni vitu ambavyo tayari vipo ndani yetu, siyo vitu vya kutafuta, bali ni vitu vya kujua tunavyo na tunawezaje kuvitumia. Kwa kuwa akili zetu hazipo katika wakati uliopo, hatuwezi kutumia hali hizi zilizopo ndani yake. Na badala yake tunadanganyika na kuhangaika kutafuta pa kupata vitu hivi. Na huwa tunadanganyika, kwa mfano kwenye kutafuta furaha, tunaishia kutafuta raha, ambayo huwa ni ya muda mfupi. Tatizo la raha ni kwamba, chochote kinachokupa raha sasa, kitakuletea maumivu baadaye. Lakini furaha ni kitu cha ndani, huhitaji kutafuta, bali unaanza kutumia, pale unapoweka akili na mawazo yako pale ulipo.

16. Maumivu ambayo unayo kwenye maisha, kwanza siyo muhimu, na ni zao la akili na mawazo yako. Maumivu uliyotengeneza sasa ni mfumo wa kutokukubali hali kama ilivyo, kutokujua hasa kile unachopitia kwa sasa, kwa sababu mawazo yako wala hayapo pale. 

Kwenye ngazi ya hisia, maumivu ni mfumo wa hali ya uhasi. Ukali wa maumivu unategemea ukubwa wa upinzani ulionao kwenye hali ya sasa. Yaani kadiri unavyopinga na kukimbia pale ulipo sasa, ndivyo unavyozidi kuumia. Akili yako inajaribu kutoroka hali ya sasa, inapenda zaidi siku zilizopita na zijazo, na kwa kuwa huwezi kufanya lolote kwenye siku hizo, unabaki kuumia.

17. Maumivu tuliyonayo ni kutokana na muda tunaotengeneza. Kuna aina mbili za muda, upo muda wa saa, hapa ni sekunde, dakika, saa, siku, mwezi na hata mwaka. Na pia upo muda wa kisaikolojia, huu ni muda uliopita muda uliopo na muda ujao. Muda wa kisaikolojia ndiyo muda unaoumiza zaidi, kwa sababu muda huu umeunganika na matukio ya maisha yetu.
 

Tunapoweka mawazo yetu kwenye muda uliopita, tunaumia kwa kukumbuka mabaya yaliyotutokea na hatuwezi kubadili chochote. Tunapokazana na wakati ujao, tunaumia na kuwa na hofu wakati hatuwezi kufanya chochote. Uhuru halisi upo sasa, kwenye muda ulionao sasa pale ulipo.

18. Kubali kile unachofanya. Hali yoyote ile ambayo wakati wa sasa inakuletea, unapaswa kuikubali na kuifanyia kazi. Usikazane kukimbia kufikiria wakati uliopita, au ujao, hutabadili chochote. Weka mawazo yako pale ulipo sasa, na fanya kile unachofanya sasa. Kumbuka hicho nacho kitapita na kuja kingine. Kwa kukubali kile kinachokuwa kwako kwa wakati uliopo, na kukifanyia kazi, hutakuwa na maumivu na pia utatengeneza njia bora zaidi kwa siku zijazo, bila hata kujiumiza.

19. Mahitaji ya ufahari wetu (ego) huwa hayana mwisho. Mara zote ego hujiona katika hali ya hatari na hivyo kuishi kwenye hali ya hofu na kuhitaji zaidi. Utaona unataka hichi, ukishakipata unaona unahitaji zaidi. Hili linaleta maumivu na maisha yasiyo na maana. Maisha ambayo hujui kwa nini unaishi, kwa sababu unaishia kukimbiza vitu ambavyo huvifikii. 

Kumaliza tatizo hili la ego, ni kuweka mawazo yako pale ulipo. Unajua, ukiwa pale ulipo, hakuna kingine ambacho kina umuhimu. Hutafikiria wengine wanakuchukuliaje, hutakazana kuwafurahisha wengine, bali utafanya kile ambacho ni muhimu kwa wakati huo, na utakuwa na mapenzi, amani na furaha.

20. Katika hali ya tahadhari, ndiyo sehemu pekee ambayo mtu anakuwa kweli pale alipo, kwa sababu kuwa pale ulipo kwa wakati huo ni muhimu sana kwa uhai wako kwa wakati huo. Chukulia mfano kama umewahi kukimbizwa na mbwa mkali, hata kama ni mbele ya watu, hutaona aibu wala kufikiria watu wanakuchukuliaje, unachokuwa unawaza kwa wakati huo ni kunusuru maisha yako, na utafanya kila linalowezekana kwa wakati huo. 

Hutafikiria wakati uliopita wala unaokuja, hayo yote hayana msaada kwako kwa wakati huo, kitu pekee chenye msaada, ni kuwa pale ulipo sasa, akili na mawazo yako kuwa pale ulipo, ili kuokoa maisha yako. Na hapo unaweza kuruka ukuta ambao hutakuja kuweza kuuruka tena kwenye maisha yako, na hivyo ndivyo nguvu ya SASA. Ambayo ukiweza kuitumia kila siku kwenye maisha yako, utaweza kuwa na maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa.

Popote pale unapokuwa, hakikisha upo pale kweli, kimwili, kiroho na kiakili. Usiweke mwili pale na kuruhusu akili yako iruke ruke kama nyani au kipepeo. Badala yake jifunze kuitumia akili yako, na itaweza kukusaidia kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita