Kuna wakati katika maisha umekuwa ukisubiri baadhi ya mambo yakae sawa ndipo uanze kufanya jambo fulani.  Lakini ukweli kwamba kufanya hivi ni sawa na kusubiri jua lizame nyakati asubuhi, hii ikiwa na maana ya kwamba kusubiri muda fulani ndiyo uanze mpango fulani ni kujidanganya mwenyewe.
Kwani unavyozidi kusubiri, muda nao haukusubiri wewe na pia changamoto juu ya jambo hilo ndivyo zinavyozidi kuwa nyingi, hivyo kila wakati ni vyema kujitoa kwa kufanya jambo ambalo una makusudi mazima ya kulitenda jambo hilo.
Hivyo ila wakati ni vyema  ukapambana na mambo magumu, wakati mambo hayo bado ni rahisi. Vile vile pambana na changamoto zako, wakati changamoto hizo bado ni kidogo.
Pambana na kuitunza afya yako, wakati bado umzima. Pambana na umaskini, wakati bado ukijana mwenye nguvu. Kwani upo usemi usemao usipoitesa akili yako angali u kijana, basi jiandae kuutesa mwili wako pindi utakapozeeka.

Usemi huo ni wa kweli kwa sababu kila changamoto unayokutana nayo kwenye maisha, unaweza kuishinda ikiwa utakabiliana nayo mapema. Acha kusubiri mambo yameharibika ndio uanze kukomaa na changamoto yako. Acha kusubiri nyumba imeungua ndio utafute maji ya kuzimia moto, au usubiri ufa ubomoe ukuta ndipo uanze kujilamu. Kafanya hivi ni sawa na kuzima moto kwa kupiga chafya.

Hivyo kila wakati na kila saa ogopa kuishi maisha ya zima moto. Ishi kwa mipango sahihi, ambayo mipango hiyo mwisho wa siku itakuongoza wewe kuweza kufikia katika mafanikio yako makubwa. Wengi wanashindwa katika maisha kwa sababu ya kuchelewa kuthibiti mambo ambayo walitakiwa wayathibiti mwanzoni.
Labda tu Jiulize kwa pamoja ni mara ngapi umekwama, kwa sababu ya kushindwa kuithibiti hali fulani ambayo ulitakiwa kuithibiti mapema? Acha kuendelea kuharibu maisha yako kwa kusubiri eti mpaka mambo yameharibika ndio utafute dawa yake. Changamka sasa na anza kutekeleza majukumu yako mapema.
Hivyo kila nyakati ni vyema ukatambua  namna ya kutafuta majibu mapema kwa kila changamoto ambayo inakukabili. Kwani kama endapo utaamua kukaa kimya bila kutafuta  majibu ya changamoto ambayo inakukabili utakuwa katika hali ambayo kiukweli utakosa mtu wa kumlaumu hapo baadae.
Hivyo ili kuepuka mtu wa kumlaumu, ni vyema ukijiweka utarataibu wa kutafuta majibu ya changamoto zinazokukabili mapema, itakusaidia wewe kuwa ni sehemu majibu ya changamoto hiyo. Lakini pia pindi ujiwekeapo utaratibu wa kutafuta majibu ya changamoto mapema itakusaidia wewe kuweza kulifanya jambo hilo kabla halijaharibika kwa kiwango kikubwa.
Hivyo tuagane na wewe siku ya leo kwa sema ya kwamba “Endapo wewe ni mfanyakazi wa maofsini, mfanyabiashara, mjasiliamali au ni mwanafunzi kuna mahali unapaona kabisa kwamba mambo hayaendi sawa naomba ujiulize swali hili kila wakati, hivi ni wapi ambapo huwa  nakosea mpaka inakuwa hivi?
Imeandikwa na mwandishi na mshauri katika mafanikio Imani Ngwangwalu.
Jifunze zaidi pia kupitia blogu yake ya dirayamafanikio.blogspot.com kila siku ili kuweza kuhamasika na kuelimika.
Tunakutakia kila la kheri, ifanye AMKA MTANZANIAiwe nyumba yako ya kujifunza mafanikio.
Imani Ngwangwalu,
0713 04 80 35,